Gwiji Brazil agusia ishu ya Neymar Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika kipigo hicho ambacho Brazil ilitanguliwa kwa mabao 2-0 na Ufaransa yaliyofungwa na Kylian Mbappe na Hugo Ekitike kabla ya kufunga bao la kufutia machozi kupitia kwa Gleison Bremer, ilishuhudiwa mashabiki wakiliimba jina la Neymar kuonyesha kwamba kikosi hicho kinamhitaji mchezaji huyo.
BRASILIA, BRAZIL: SIKU chache baada ya timu ya taifa ya Brazil kupata kichapo cha mabao 2-1 nyumbani kutoka kwa Ufaransa, supastaa wa nchi hiyo, Neymar Jr ameibuka tena katika mjadala ambao unaweka shinikizo kwa kocha Carlo Ancelloti kumuita kikosini.
Katika kipigo hicho ambacho Brazil ilitanguliwa kwa mabao 2-0 na Ufaransa yaliyofungwa na Kylian Mbappe na Hugo Ekitike kabla ya kufunga bao la kufutia machozi kupitia kwa Gleison Bremer, ilishuhudiwa mashabiki wakiliimba jina la Neymar kuonyesha kwamba kikosi hicho kinamhitaji mchezaji huyo.
Wakati mashabiki wakiliimba jina la Neymar, nyota huyo amepata sapoti nyingine ya kushangaza kutoka kwa gwiji wa Brazil, baada ya kuachwa kikosini na Ancelotti.
Mjadala unaoendelea kuhusu uwepo wa Neymar katika timu ya taifa ya Brazil unapata sura mpya kila uchao na safari hii ni nahodha wa zamani na Dunga, ambaye pia aliwahi kuifundisha nchi hiyo ambaye amegusia suala hilo akimtaka kuendele kujifua na kujiandaa kwa Kombe la Dunia.
Dunga, bingwa wa Kombe la Dunia ameweka wazi kwamba uwepo wa Neymar katika Kombe la Dunia 2026 unategemea yeye mwenyewe kupambania kuingia kikosini, lakini haoni nafasi ya kumuweka kando mchezaji huyo kwa sasa.
Nahodha huyo alisema Neymar atakwenda tu kwenye fainali hizo zinazotarajiwa kuanza Juni 11 hadi Julai 19, mwaka huu huko Marekani, Mexico na Canada iwapo ataendelea kuonyesha ubora katika kikosi cha timu yake ya Santos.
Kauli ya nahodha huyo wa zamani wa Brazil inakuja katikati ya mjadala mkubwa kuhusu kutokuwepo kwa Neymar katika kikosi kipya cha Brazil kilichoitwa na Ancelotti, licha ya kwamba yupo katika kiwango bora akiwa na Santos.
“Kama mchezaji, upande wa kiufundi hakuna mjadala. Atakayeamua kama ataenda Kombe la Dunia ni yeye mwenyewe. Ili uende Kombe la Dunia unapaswa kuwa angalau na asilimia 80 tayari, si lazima iwe 100. Lakini asilimia 80 kwa mchezaji wa kiwango chake. Kwa sababu kiufundi yeye ni burudani yenyewe,” alisema Dunga alipokuwa akizungumza katika podikasti ya “Um Assado para...”.
Kwa upande mwingine, gwiji huyo wa soka wa Brazil anaona haiwezekani kwa nyota huyo wa zamani wa Barcelona kwenda Kombe la Dunia akiwa mtu wa ziada au akiba kikosini, akisisitiza ushindani uliopo ni mkubwa katika maeneo hayo. Dunga alisema: “Naona watu wanasema, ‘mchukue Neymar kwa Kombe la Dunia hata kama atakuwa mchezaji wa akiba.’ Kama kuwa mchezaji wa akiba hawezi kutokana na ushindano uliopo, hilo hatukubali. Ikiwa Ancelotti atamuita (Neymar), atalazimika kucheza. Hakuna namna atakaa benchi.”
Hatima ya Neymar kuelekea Kombe la Dunia kama ataingia kwenye kikosi cha mwisho cha Brazil au la inaonekana kuwa moja ya simulizi kubwa kuelekea mashindano. Ikiwa ataachwa, Ancelotti atakuwa katikati ya mjadala mkubwa na atalazimika kueleza sababu za kumuacha mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya Brazil hasa kama ataendelea kuwa katika kiwango bora.