Ishu ya Rashford kaishika Amorim

Muktasari:
- Rashford, ambaye ni zao la kutokea kwenye akademia ya Man United amejiunga na Aston Villa kwa mkopo kwenye dirisha la Januari baada ya kupigwa chini na kocha huyo Mreno.
MANCHESTER, ENGLAND: LISEMWALO ni Marcus Rashford hatakuwa na maisha yoyote kwenye kikosi cha Manchester United endapo kama Kocha Ruben Amorim ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.
Rashford, ambaye ni zao la kutokea kwenye akademia ya Man United amejiunga na Aston Villa kwa mkopo kwenye dirisha la Januari baada ya kupigwa chini na kocha huyo Mreno.
Tangu alipotua Villa Park, Rashford ameasisti mara nne katika mechi tisa za michuano yote huku akitengeneza kombinesheni matata kabisa na mchezaji mwenzake wa mkopo, Marco Asensio.
Kinachoelezwa ni Aston Villa inaweza kukamilisha dili la kumbeba jumla Rashford na hilo linaweza kuwa na faida kubwa kwa Mwingereza huyo baada ya kocha Amorim kumfuta katika hesabu zake.
Aston Villa inaweza kunasa saini ya mshambuliaji huyo kwa ada ya Pauni 60 milioni kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Mkataba wa Rashford, 27, huko Man United imebakiza miaka mitatu, lakini kwa mujibu wa gwiji wa timu hiyo, Bryan Robson haoni kama mchezaji huyo atatoboa mbele ya kocha Amorim.
"Marcus ana kipaji kikubwa na amekuwa akifanya vizuri Manchester United,” alisema.
“Hakupaswa kwenda Aston Villa. Alipaswa kucheza kwa nguvu zote na kwa ubora wote Man United. Lakini, ishu ya kurudi itakuwa ni uamuzi wa kocha na mchezaji. Lakini, kwa upande wangu, Rashford ana kipaji kikubwa."