Joto latishia nyota Canada

Muktasari:


  • Joto linaripotiwa ni kali sana nchini humo na kwa jana katika Uwanja wa Children’s Mercy Park, Canada ikicheza dhidi ya Peru kulikuwa na nyuzi joto 38.

KANSAS CITY, MAREKANIL: WACHEZAJI wa Canada wameonyesha wasiwasi juu ya  usalama wa afya zao kutokana na hali ya joto kali iliyopo huko Marekani inakofanyika michuano ya Copa America.

Joto linaripotiwa ni kali sana nchini humo na kwa jana katika Uwanja wa Children’s Mercy Park, Canada ikicheza dhidi ya Peru kulikuwa na nyuzi joto 38.

Hali hiyo ya joto kali ilisababisha mwamuzi msaidizi wa mchezo huo, Humberto Panjoj kudondoka uwanjani baada ya kuzidiwa hali iliyozua taharuki na kuwaogopesha mastaa ambao wameshauri mechi zichezwe usiku au baada ya jua kuzama.

Mmoja kati ya wachezaji wa Canada waliozungumzia suala hilo ni beki, Alistair Johnston ambaye alisema:” Haya ni mazingira ambayo huwezi hata kumwombea adui yako akutane nayo, nafikiri wabadilishe muda, haiwezi kuwa saa 11, walau wapeleke mbele iwe saa mbili au tatu usiku, kwa sababu hali ya sasa sio salama hata kwa mashabiki.”

Mwamuzi Panjoj ambaye alidondoka dakika za mwisho za kipindi cha alisaidiwa na wachezaji ikiwemo kipa wa  Canada, Maxime Crepeau na baadae akatolewa kupatiwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya The Sun kwa sasa anaendelea vizuri.