PSG yaivamia Barcelona vita ya Julian Alvarez

Muktasari:

  • Taarifa za awali zilieleza kuwa Man City haina mpango wa kumuuza staa huyu lakini Barca na PSG hazijakata tamaa.

PARIS St-Germain imejumuika katika vita dhidi ya Barcelona katika harakati za kuiwania saini ya mshambuliaji wa Manchester City na Argentina, Julian Alvarez katika dirisha hili.

Taarifa za awali zilieleza kuwa Man City haina mpango wa kumuuza staa huyu lakini Barca na PSG hazijakata tamaa.

PSG inataka kumsajili fundi huyu ili kuboresha eneo la ushambuliaji ambalo limepoteza nguzo muhimu baada ya Kylian Mbappe kutimkia zake Real Madrid.

Alvarez mwenyewe ambaye ana umri wa miaka 24, hajaonyesha nia ya kutaka kuondoka na mara kadhaa alizohojiwa amekuwa akisema kwamba anahitaji kubaki Man City.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa watu wake wa karibu zinaeleza anataka kuondoka ili kujiunga na timu ambayo atakuwa na uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza tofauti na ilivyo sasa ambapo mara nyingi anatumika kama mbadala wa Erling Haaland.

Timu nyingi zimevutiwa na kiwango alichoonyesha msimu uliopita ambapo alicheza mechi 56 za michuano yote na kufunga mabao 20.

Mkataba wake unamalizika mwaka 2028 inaonekana pia kuwa ngumu kwa Man City kumruhusu aondoke kirahisi hivyo, na hata kama atauzwa inaweza kuwa kwa mkwanja mrefu. Staa huyo ameshinda mataji takriban yote makubwa ya soka.


MBALI ya timu za England, pale Italia AC Milan  pia inahitaji saini ya straika wa AS Roma, Tammy Abraham katika dirisha hili.

Tammy ambaye mkataba wake na Roma unamalizika mwaka 2026, ameripotiwa kuwekwa sokoni na timu hiyo.

Staa huyu raia wa England anahusishwa kuondoka Roma baada ya kutofanya vizuri msimu uliopita.


JUVENTUS inamfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Atalanta, Ademola Lookman, 26, ambaye pia Bayern Munich ilituma maskauti kwa ajili ya kumtazama msimu uliopita.

Staa huyu raia wa Nigeria mwenye umri wa miaka 26, mkataba wake unaisha 2026.

Msimu uliopita alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 17 na kutoa asisti 10. Aliitungua Leverkusen ‘hat-trick’ fainali ya Europa League.


BAYERN Munich ipo katika mazungumzo na Bayer Leverkusen kwa ajili ya kuipata huduma ya beki wa timu hiyo na Ujerumani, Jonathan Tah, 28, katika dirisha hili.

Tah ni miongoni mwa mastaa walioonyesha kiwango bora akiwa na Leverkusen kwa msimu uliopita ambapo aliisaidia timu hiyo kushinda taji la Bundesliga. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2025.


MABOSI wa Newcastle United wana matumaini makubwa kwamba straika wao kutoka Sweden, Alexander Isak, 24, atasaini mkataba mpya na kuendelea kusalia katika kikosi chao kwa msimu ujao licha ya timu nyingi kuonyesha nia ya kutaka kumsajili ikiwa pamoja na Arsenal. Isak ambaye alikuwa katika kiwango bora kwa msimu uliopita, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.

Paris Saint-Germain ni miongoni mwa timu zilizoonyesha nia ya kutaka kumsajili.


BARCELONA inataka kuachana na mpango kumsajili beki wa kulia wa Bayern Munich na Ujerumani, Joshua Kimmich, katika dirisha hili na sasa imehamishia nguvu kwa mastaa wengine ikiwa pamoja na Amadou Onana kutoka Everton na staa wa Real Sociedad na Hispania, Mikel Merino.

Barca ilikuwa inataka kumsajili Kimmich kwa sababu mbali ya kucheza kama beki wa kulia pia anacheza kama kiungo.


TOTTENHAM inakumbana na upinzani mkali kutoka kwa timu za Hispania na Ujerumani ambazo pia zinahitaji saini ya kiungo wa Leeds United na England, Archie Gray, 18, katika dirisha hili.

Kwa mujibu wa tovuti ya Talksport, Spurs ndio ilikuwa ya kwanza kuingia katika mazungumzo na mabosi wa Leeds ili kumnasa Gray ambaye mkataba wake unaisha mwaka 2028.


EVERTON imejumuika na timu nyingine katika harakati kuiwania saini ya winga wa Hull City, Jaden Philogene, 22.

Jaden amekuwa katika rada za timu nyingi barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita ambapo alicheza mechi 33 za michuano yote na kufunga mabao 12. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.