Kinachoendelea Arsenal dirisha la usajili

Muktasari:

  • Kocha Mikel Arteta anataka kuboresha kiwango cha timu yake kwa ajili ya msimu ujao, kuhakikisha anatengeneza timu ya kupambana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City ya Pep Guardiola.

LONDON, ENGLAND: ARSENAL bado haijafanya biashara ya maana kwenye dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi huko Ulaya, lakini kinachoonekana muda wowote, chama hilo la Emirates litatangaza usajili mpya.

Kocha Mikel Arteta anataka kuboresha kiwango cha timu yake kwa ajili ya msimu ujao, kuhakikisha anatengeneza timu ya kupambana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City ya Pep Guardiola.

Klabu hiyo dhamira kubwa bado ipo kwenye kunasa saini ya mshambuliaji wa kati, eneo ambalo limedaiwa kuwa na shida kubwa kwa misimu ya hivi karibuni na kutibua mipango yao kwenye mbio za ubingwa.

Kwenye hilo, kuna mastaa kibao wenye majina makubwa wamehusishwa na mpango wa kutua huko Emirates, wakiwamo mastraika wa kiwango cha juu kabisa kama Victor Osimhen na Viktor Gyokeres.

Kiungo mpya pia ni eneo linalopewa kipaumbele kwenye mpango wa usajili wa miamba hiyo ya Emirates, kutokana na mkali wa Ghana, Thomas Partey kuwa kwenye hali ya sintofahamu juu ya hatima yake kwenye kikosi hicho cha Washika Bunduki.

Kwenye mpango huo wa kiungo mpya, kikosi hicho cha kocha Arteta kinahusishwa na huduma za mastaa kadhaa, akiwamo kiungo wa Everton, Amadou Onana na wa Newcastle, Bruno Guimaraes.

Straika wa Napoli, Osimhen amekuwa akihusishwa sana na Arsenal kwa siku za hivi karibuni, huku bosi anayesimamia usajili kwenye kikosi hicho cha Emirates, Mbrazili Edu alisema mpango wao kwenye dirisha hili ni kuhakikisha wanaboresha safu yao ya ushambuliaji ili kuwa na makali ya kutisha.

Kocha mpya wa Napoli, Antonio Conte alithibitisha kwamba kuna dili linajadiliwa juu ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Nigeria kubadili timu kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwa kuwa Osimhen yupo kwenye mipango ya kuuzwa na huenda akatua Arsenal, miamba hiyo ya Serie A inayonolewa na Conte, hesabu zao kwa sasa zipo kwenye kunasa huduma ya straika wa Chelsea, Romelu Lukaku ili kwenda kuziba pengo huko.

Kwenye ishu ya beki wa kati, Arsenal iliwahi kuhusishwa na Jules Kounde, lakini mpango wao huo uliwekewa ngumu na Barcelona.

Arsenal inamtaka Kounde, 25, kwa sababu inaweza kumtumia kwenye beki ya kulia na beki ya kati, huduma ambayo bila ya shaka ni kitu ambacho kocha Arteta atapenda kuwa nacho kwenye kikosi chake.

Hata hivyo, Arsenal inalazimika kutazama machaguo mengine kutokana na Barcelona kuripotiwa kuwa haina mpango wa kumuuza Kounde. Kuna taarifa zinafichua kwamba, mambo ya kumuuza Kounde yanaweza kubadilika kulingana na Ronald Araujo, ambaye amekuwa akihusishwa na Manchester United, ikihitaji saini yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwenye kupata huduma za mastaa wapya huko Emirates, kocha Arteta anahitaji kupiga bei mastaa kibao akiwamo Smith Rowe, ambayo yenyewe imelenga kupata walau Pauni 25 milioni ili kuongeza kitu kwenye bajeti yao ya usajili. Mastraika wengine kwenye rada za Arsenal ni pamoja na Ivan Toney, Joshua Zirkzee, ambaye pia anatakiwa na Man United, Serhou Guirassy na Alexander Isak.