Onana kuzua vita kali Ulaya

Muktasari:

  • Jambo hilo linafanya vita ya kunasa saini ya kiungo huyo kuwa kali zaidi.

BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA imeripotiwa ipo tayari kutunishiana misuli na Manchester United na Arsenal kwenye mchakamchaka wa kunasa huduma ya kiungo ambaye pia Bayern Munich inamtaka ikiamini anafaa kwenda kuchukua buti za Joshua Kimmich huko Allianz Arena.

Jambo hilo linafanya vita ya kunasa saini ya kiungo huyo kuwa kali zaidi.

Unajua ni nani? Kiungo mwenyewe ni Amadou Onana wa Everton na timu ya taifa ya Ubelgiji, ambaye kwa sasa yupo kwenye fainali za Euro 2024 huko Ujerumani akijiandaa kuitumikia timu yake kwenye mchezo wa mtoano wa hatua ya 16 bora dhidi ya Ufaransa, kesho Jumatatu.

Awali, Barcelona ilikuwa ikihusishwa sana na Kimmich baada ya kuripotiwa kwamba Bayern ipo tayari kuachana na kiungo huyo, ambaye amecheza mechi 390 kwenye kikosi chao na kushinda mataji 20 huku akiingia mwaka wa mwisho kwenye mkataba wake.

Lakini, ripoti ya mwezi uliopita ilibainisha Kimmich amekataa ofa ya Barcelona na tangu hapo hakuna kilichoendelea.

Na sasa, kocha wa zamani wa Kimmich huko Bayern, Hansi Flick, ambaye amechukua mikoba ya kuinoa Barcelona, anafahamu wazi miamba hiyo ya Nou Camp ipo sokoni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kutafuta kiungo mpya.

Hivyo sasa imehamia kwa Onana wa Everton, huku viungo wengine waliopo kwenye rada yao ni Mikel Merino wa Real Sociedad. Lakini, kwenye ishu ya huduma ya Onana, jambo hilo litawaingiza kwenye vita kali na klabu za Arsenal, Man United na Bayern. Zote zinamtaka Mbelgiji huyo.

Bayern chini ya kocha Vincent Kompany, ambaye ni Mbelgiji anahitaji saini ya Onana baada ya kuona kuna ugumu kwenye mpango wao wa kumsajili Joao Palhinha. Arsenal yenyewe pia inamtaka Onana kwa sababu bado haina uhakika juu ya hatima ya staa wa Ghana, Thomas Partey.

Onana bado ana mkataba wa miaka mitatu kwenye kikosi cha Everton, lakini tatizo la uchumi linaweza kuilazimisha klabu hiyo ya Goodison Park kufanya biashara ya kumpiga bei kiungo huyo kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.