Kisa Ebola, kambi ya DR Congo yafutwa
Muktasari:
- Maandalizi hayo sasa yatafanyika Ubelgiji kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo, ambao unaaminika kusababisha vifo vya zaidi ya watu 130.
TIMU ya Taifa ya DR Congo imefuta kambi yake ya maandalizi ya Kombe la Dunia iliyokuwa ifanyike mjini Kinshasa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi hiyo.
Maandalizi hayo sasa yatafanyika Ubelgiji kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo, ambao unaaminika kusababisha vifo vya zaidi ya watu 130.
Wakati kambi hiyo ikifutwa, Serikali ya Marekani imesitisha utoaji wa viza kwa raia wa DR Congo kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo.
Hatua hii imezua taharuki kubwa na hofu juu ya mipango ya safari kwa mashabiki wa timu ya taifa ya nchi hiyo ambao walikuwa wakijiandaa kwenda Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026 na DR Congo ipo kundi K na Ureno, Colombia na Uzbekistan.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limesema linafuatilia kwa karibu sana hali hiyo ili kuona jinsi ya kunusuru ratiba na usalama wa kila mmoja. Hili linakuja kama pigo lingine kwa DR Congo baada ya taarifa za majeraha ya beki wao tegemeo, Rocky Bushiri Kisonga ambaye ameondoshwa kikosini.
WHO ambalo ni Shirika la Afya Duniani, limetangaza mlipuko huo wa Ebola kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa, lakini limesema bado haujafikia kiwango cha janga la dunia.
Msemaji wa timu ya taifa ya DR Congo, Jerry Kalemo amesema michezo ya kirafiki ya maandalizi Ulaya itaendelea kama ilivyopangwa, huku kikosi hicho kikijiandaa kushiriki Kombe la Dunia 2026 kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974.
Juni 3 mwaka huu, DR Congo inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Denmark huko Ubelgiji na Juni 9 dhidi ya Chile nchini Hispania kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia 2026, Juni 11.
Mchezo wao wa kwanza kwenye mashindano hayo utachezwa Juni 17 mjini Houston, Marekani, dhidi ya Ureno.
Kwa mujibu wa msemaji wa timu hiyo aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters, kufutwa kwa kambi hiyo kulitokana na masharti ya usafiri yaliyowekwa na Marekani, ambao ni mmoja wa waandaaji wa Kombe la Dunia pamoja na Mexico na Canada.
Mamlaka ya afya ya Marekani imepiga marufuku kuingia nchini humo kwa watu wasiokuwa raia wa Marekani ambao wamewahi kuwa DR Congo, Uganda au Sudan Kusini ndani ya siku 21 zilizopita, kama hatua ya kudhibiti kusambaa kwa Ebola.
Wachezaji wote wa DR Congo pamoja na kocha wao raia wa Ufaransa, Sébastien Desabre, wanaishi nje ya DR Congo, hivyo hawataathiriwa na masharti hayo baada ya kambi ya Kinshasa kufutwa.
Baadhi ya wafanyakazi wa timu waliokuwa DR Congo waliondoka nchini humo Jumatano ili kuepuka kuathiriwa na muda wa siku 21 uliowekwa na Marekani, Kalemo aliliambia shirika la Associated Press.