Kocha Chelsea afunguka njia wanayopita

Muktasari:
- Hadi kufikia mechi 16 za ligi, Chelsea ilikuwa imeshinda mechi tano mfululizo na walikuwa na tofauti ya pointi tatu tu dhidi ya Liverpool ya Arne Slot.
LONDON, ENGLAND: WAKATI ligi ipo kwenye nusu ya mzunguko wa kwanza, Chelsea ilikuwa ikionekana kuwa mpinzani halisi wa Liverpool katika mbio za ubingwa.
Hadi kufikia mechi 16 za ligi, Chelsea ilikuwa imeshinda mechi tano mfululizo na walikuwa na tofauti ya pointi tatu tu dhidi ya Liverpool ya Arne Slot.
Enzo Maresca kuhusu kuchukua taji msimu huu alisema; “Kwa sasa tupo mbele ya matarajio yetu kwa namna tunavyocheza na pointi tulizo nazo, ningependa kuwa na aina hiyo ya presha ya kuwania ubingwa lakini sio sasa.”
Tangu kauli hizo, kiwango cha Chelsea kilishuka na sasa wapo nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, nyuma ya Liverpool kwa pointi 22.
Maresca bado anaweza kuibadilisha Chelsea kuwa washindani wa kweli lakini kuna mambo yanapaswa kubadilika.
Kocha huyo amemkosa Nicolas Jackson kwa muda kutokana na majeraha na amekosa mtu wa kuziba nafasi yake ya kukimbia nyuma ya mabeki, kushirikiana na Cole Palmer na kutoa pasi za haraka.
Huenda wanahitaji mshambuliaji anayecheza sawa na Jackson ili kuziba pengo lake anapoumia.
Chelsea walikuwa juu mwanzoni mwa msimu kwa sababu ya mabeki wa pembeni waliogeuka viungo timu ilipokuwa inashambulia.
Marc Cucurella na Malo Gusto walifanya vizuri, huku Fernandez na Moises Caicedo wakiwika katikati.
Lakini sasa Chelsea wameshaeleweka, na mchezo wao umekuwa ukilenga sana katikati ya kiwanja na kuwa wa kutabirika. Hakuna ubunifu wa kutosha kutoka kwa wachezaji wa pembeni, na wanahitaji mchezaji wa mguu wa kushoto anayeweza kucheza upande wa kushoto na kuwapita mabeki moja kwa moja.
Hapa wanaweza kumsajili Jamie Gittens, 20, ambaye wamekuwa wakimwinda kwa muda mrefu lakini watatakiwa kutoa kiasi kikubwa cha pesa.
Sehemu nyingine ambayo inapaswa kubadilika kubadilika katika kikosi hicho ni kipa kwa sababu Robert Sanchez amekuwa na makosa mengi.
Maresca anataka kipa wake aweze kujiunga na safu ya ulinzi na kuwa kama mchezaji wa ziada anapokuwa na mpira jambo ambalo Sanchez hafanyi na muda mwingi sio mtulivu anapokuwa na mpira mguuni.