Kumenoga Euro 2024! Kwa rekodi hizi kitanuka mtoano

Muktasari:

  • Mchezo ambao macho na masikio ya mashabiki wengi watatamani kuushuhudia ni ule wa Ufaransa na Ubelgiji utakaopigwa Julai 1, kwenye dimba la Merkur Spiel-Arena, Dusseldorf.

MUNICH, UJERUMANI: MICHUANO ya Euro sasa imenoga na kuanzia wikiendi hii, hatua ya 16 bora inatarajiwa kuanza kupigwa huku baadhi ya mechi ambazo zitakutanisha vigogo zikionekana kusubiriwa kwa hamu.

Mchezo ambao macho na masikio ya mashabiki wengi watatamani kuushuhudia ni ule wa Ufaransa na Ubelgiji utakaopigwa Julai 1, kwenye dimba la Merkur Spiel-Arena, Dusseldorf.

Mara ya mwisho kwa mataifa haya kukutana katika michuano ya Euro ni mwaka 1984 na Ufaransa ilishinda mabao 5-0.

Lakini katika matokeo ya jumla kwa mechi za michuano yote walizokutana, Ubelgiji ndio inaongoza kwa kupata  matokeo mazuri zaidi ikishinda mara 30, kupoteza 26 na sare 19.

Mara ya mwisho kwa Ubelgiji kupata ushindi mbele ya Ufaransa ni mwaka 2015, katika mchezo wa kirafiki na ilishinda mabao 4-3.

Utamu wa mechi hii ni, timu zote zina mastaa ambao wanatamba Ulaya ambao wanasubiriwa kuonwa kama wataweza kuokoa mataifa yao na kuyavusha kwenda robo fainali.

Mbali ya mchezo wa mafahari hao, bingwa mtetezi Italia itashuka dimbani kesho kuvaana na Uswiss ambayo imekuwa na historia nzuri dhidi yao.

Mara ya mwisho Uswiss kushinda dhidi ya Italia ilikuwa Mei 01, 1993, katika Fainali za Kombe la Dunia na ilishinda 1-0, tangu hapo imefungwa mara tano na kutoa sare sita katika mechi 11 za mwisho.

Katika mechi tano za mwisho za michuano hii dhidi ya Uswiss, Italia imeshinda tatu na kutoa sare mbili.

Wana fainali wa michuano iliyopita, watoto wa mfalme Charles III, England ilimaliza ikiwa kinara kwenye kundi lao kwa pointi nne na katika hatua hii itakutana na Slovakia Jumapili ya wikiendi hii.

Tangu England ianze kukutana na Slovakia mwaka 2002,  historia inaonyesha haijawahi kupoteza, katika mechi sita imeshinda tano na sare moja.

Mara ya mwisho kukutana katika Euro ni mwaka 2016 na mchezo ukamalizika kwa sare.

Wenyeji na mabingwa wa kihistoria wa michuano hii, Ujerumani, wao wataumana na Denmark ambao walimaliza nafasi ya pili katika kundi lao nyuma ya England.

Mataifa haya yatakuwa kwa mara ya 29 katika historia ya michuano yote huku Ujerumani ikionekana kuwa na rekodi nzuri zaidi.

Katika mechi 28 walizokutana hapo awali, Ujerumani imeshinda 15, sare tano na Denmark ikashinda nane.

Tangu mwaka 2010, Denmark haijawahi kupata ushindi wowote mbele ya Ujerumani na katika kipindi hicho hadi sasa zimecheza mechi nne, Ujerumani ikashinda moja mwaka 2012 katika michuano ya Euro, kisha zilizobakia zikamalizika kwa sare.

Cristiano Ronaldo na Ureno yake iliyomaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi F, itakutana na Slovenia iliyoingia hatua hii kwa kumaliza nafasi ya tatu kundi C.

Hakuna historia kubwa baina ya timu hizi kwani zimekutana mara moja tu, Machi 24, mwaka huu na Slovenia ikapata ushindi wa mabao 2-0.

Miongoni mwa timu za kwanza kufuzu hatua hii ya mtoano Hispania, ambao pia ni mabingwa wakihistoria wa michuano ikibeba mataji matatu sawa na Ujerumani, itakutana na Georgia, Jumapili ya wikiendi hii.

Historia inaonyesha, katika mechi saba ni mchezo mmoja tu ndio Hispania ilipoteza mbele ya Georgia na zilizobakia zote imeshinda.

Mchezo huo iliopoteza ni wa kirafiki mwaka 2016.

Allianz Arena, Romania itakuwa na shughuli pevu dhidi ya miamba Uholanzi na katika mechi 13 za michuano yote zilipokutana Romania imeshinda moja tu, mwaka 2007 katika michuano ya Euro.

Wazee wa kazi, Uturuki wao wataumana na Austria ikiwa ni moja ya mechi ambazo zinasubiriwa kwa hamu kwani Austria imemaliza hatua ya makundi ikiwa kinara mbele ya Ufaransa wakati Uturuki ikimaliza nafasi yapili nyuma ya Ureno lakini pointi walikuwa sawa, wote sita.

Katika hatua ya robo fainali, mshindi wa mchezo kati ya Hispania na Gergia atakutana na mshindi kati ya Ujerumani na Denmark, Julai 05, kwenye uwanja wa MHPArena, Stuttgart, wakati Ureno na Slovenia timu itakayopita itakutana na mbabe kati ya Ufaransa na Ubelgiji, Julai 05, kwenye Uwanja wa Volksparkstadion, Hamburg

Ikiwa England ama Slovakia mmoja wao atapita basi ataenda kuvaana na mshindi kati ya Uswiss na Italia, vilevile mshindi wa mchezo kati ya Romania na Uholanzi atakutana na mshindi wa mechi ya Austria na Uturuki, zote zitapigwa Julai 06.

Mechi hizi za hatua ya 16 bora zinatarajiwa kupigwa kuanzia kesho, Juni 29, 30 na Julai 01 na 02.