Emery anasa kifaa cha Chelsea

Muktasari:

  • Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Unai Emery kimekubali kulipa Pauni 37.5 milioni kwa ajili ya kunasa huduma ya beki huyo wa kushoto na kuripotiwa kwamba imemsainisha mkataba wa miaka sita.

BIRMINGHAM, ENGLAND: NDO hivyo. Aston Villa imekamilisha usajili wa Ian Maatsen kutoka Chelsea.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Unai Emery kimekubali kulipa Pauni 37.5 milioni kwa ajili ya kunasa huduma ya beki huyo wa kushoto na kuripotiwa kwamba imemsainisha mkataba wa miaka sita.

Maatsen, 22, alijiunga kwenye akademia ya Chelsea akitokea PSV mwaka 2018. Alicheza mechi yake ya kwanza Septemba 2019, lakini alitolewa kwa mkopo kwenda Charlton, Coventry na Burnley.

Maatsen - ambaye anajiandaa na mechi yake ya Uholanzi katika mchezo wao wa hatua ya 16 bora kwenye fainali za Euro 2024 dhidi ya Romania keshokutwa Jumanne, aliichezea Chelsea ya kocha Mauricio Pochettino mechi 15 msimu uliopita.

Hata hivyo, Mdachi huyo aliruhusiwa kwenda Borussia Dortmund kwenye nusu ya pili ya msimu wa 2023-24.

Na kwenye kikosi hicho cha miamba ya Bundesliga, alianzishwa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Dortmund ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Real Madrid uwanjani Wembley. Maatsen alicheza mechi kadhaa za Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Dortmund na alifunga bao kwenye robo fainali dhidi ya Atletico Madrid.

Kiwango chake bora huko Dortmund kimemfanya apate namba kwenye timu ya msimu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku kocha Edin Terzic alimsifu Maatsen kuwa ni beki wa kushoto bora kabisa kwenye Bundesliga.

Dortmund ilitamani kubaki na huduma ya mchezaji huyo, lakini kikosi hicho kinachonolewa na kocha Nuri Sahin kwa sasa, kiliona kulipa Pauni 37 milioni ni pesa nyingi sana na hivyo kuwaruhusu Aston Villa kwenda kunasa saini yake, ikijiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.