Kwa nini bao la kusawazisha la Croatia lilikataliwa na VAR?
Muktasari:
- Josko Gvardiol alionekana kuwa shujaa wa Croatia alipofunga bao dakika ya 103 (dakika ya 13 ya muda wa nyongeza), akionekana kuifanya mechi kuwa sare ya mabao 2-2 na kupeleka mchezo katika muda wa ziada.
ATLANTA, MAREKANI: CROATIA walijikuta wakiondoka Kombe la Dunia wakiwa na majonzi makubwa baada ya teknolojia ya VAR na mfumo unaofanana na “Snicko” kuwanyima bao la kusawazisha katika dakika za mwisho za mchezo dhidi ya Ureno, jana. Ureno ilikuwa imetangulia kwa mabao 2-1.
Josko Gvardiol alionekana kuwa shujaa wa Croatia alipofunga bao dakika ya 103 (dakika ya 13 ya muda wa nyongeza), akionekana kuifanya mechi kuwa sare ya mabao 2-2 na kupeleka mchezo katika muda wa ziada.
Hata hivyo, mwamuzi wa VAR, Jarred Gillett, aliingilia kati na kuanza kupitia tukio hilo ili kubaini kama kulikuwa na kuotea. Kilichokuwa kinachunguzwa ni kama mshambuliaji wa Croatia, Igor Matanovic, aliugusa mpira kwa kichwa wakati wa maandalizi ya bao hilo.
Iwapo Matanovic angekuwa ameugusa mpira, basi angehesabika kuwa alihusika kwenye mchezo akiwa katika nafasi ya kuotea, na hivyo bao lingekataliwa. Kama asingekuwa ameugusa, basi bao la Gvardiol lingekubaliwa.
Katika marudio ya video haikuwa rahisi kuona kama Matanovic aligusa mpira au la. Hata hivyo, mwamuzi Espen Eskas alionyeshwa taarifa kutoka kwenye teknolojia inayofanana na “Snickometer”, ambayo ilionyesha mabadiliko ya mawimbi (spike) yaliyothibitisha kuwa mpira uliguswa. Kutokana na ushahidi huo wa kiteknolojia, mwamuzi alikataa bao hilo.
SNICKO NI NINI?
Teknolojia ya Snicko hutumika kubaini kama mpira umeguswa au la, ambapo mashabiki wa mchezo wa kriketi wanaifahamu vizuri ambayo hutumia mawimbi ya sauti kuonyesha kama mpira umegusa gongo (bat) kabla ya mwamuzi kutoa uamuzi.
Katika soka, mfumo kama huo umetumika tangu Kombe la Dunia 2022, mashindano ya Ulaya (Euro 2024), na sasa unaendelea kutumika katika Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), mpira rasmi wa mashindano wa Adidas Trionda una kifaa maalumu (chip) ndani yake kinachoweza kugundua kila mguso wa mpira kwa usahihi mkubwa.
Taarifa hizo hutumwa papo hapo kwa waamuzi wa VAR, na hivyo kuwasaidia kufanya uamuzi sahihi zaidi.
Kwa kuwa mfumo huo ulithibitisha kuwa Matanovic aliugusa mpira kabla haujamfikia Gvardiol, na Matanovic alikuwa ameotea, sheria ililazimisha bao hilo kukataliwa.
Kocha wa Croatia, Zlatko Dalic hakuficha masikitiko yake baada ya mchezo aliposema: “Sitazungumzia sana tukio hilo, lakini naweza kusema kuwa kiwango cha uamuzi wa waamuzi kilikuwa kibaya sana. Hatukupata faulo nyingi ambazo tulistahili, wala mipira ya adhabu. Hata hivyo, hiyo siyo sababu ya kushindwa.
“Kila mtu ameona jinsi hisia za mchezo zilivyopotea. Uamuzi huu unaua furaha ya soka. VAR imeua hisia, imeua kila kitu ndani ya mchezo. Tumekwenda mbali sana katika matumizi ya VAR.”
Hata hivyo, Kocha wa Ureno, Roberto Martínez, hakukubaliana na malalamiko hayo akisema: “Ni jambo la kusikitisha kwamba timu moja ilipaswa kuondoka. Lakini huu haukuwa uamuzi wa bahati wala wa upendeleo. Ulikuwa uamuzi sahihi.”
“Mpira wa mashindano una kifaa maalumu ndani yake, na sensa ilionyesha wazi kuwa mpira uliguswa.” Baada ya ushindi huo, Ureno wamefuzu hatua ya 16 Bora, ambapo wanakutana na majirani zao wa Rasi ya Iberia, Hispania.
LUKA MODRIC NDO BASI TENA
Uamuzi huo ulihitimisha safari ya mmoja wa magwiji wakubwa wa soka duniani, Luka Modric anayekipiga AC Milan kwa sasa.
Kwa Modric na Croatia, ulikuwa mwisho wenye heshima baada ya mapambano makubwa. Kipindi cha kwanza kilikuwa cha kawaida, lakini kipindi cha pili kiligeuka kuwa moja ya michezo ya kusisimua zaidi katika mashindano hayo.
Toronto ikaaga Kombe la Dunia kwa mchezo uliojaa drama, huku Croatia wakiondoka wakiamini walistahili zaidi.
Lakini baada ya filimbi ya mwisho, Ronaldo alionyesha upande mwingine wa utu ambapo alikuwa akilia huku akiinua juu jezi yenye namba 21 iliyokuwa ikivaliwa na mchezaji mwenzake, Diogo Jota, aliyefariki dunia kwa ajali mwaka jana.
Baada ya ushindi huo, wachezaji na benchi lote la Ureno walipiga picha wakiwa wameizunguka jezi ya Jota, wakionyesha kuwa safari yao sasa ina maana kubwa zaidi ya soka pekee. Hata hivyo, kwa Modric safari imefikia mwisho.