Prime
Julius: Nimelala sana njaa na ustaa wangu
MSEMO wa usihukumu kitabu kwa kava lake ni halisi na unaendana na watu maarufu, utofauti wa maisha yao yanayoonekana katika kamera yanayowavutia mashabiki wao, lakini nyuma yake kuna mengi yamejificha ya kuumiza na kufurahisha.
Nyuma ya Kamera awamu hii imepata nafasi ya kuzungumza na msanii wa filamu za mapigano, Julias Charles 'Giant' anayefichua umaarufu haumanishi kumiliki pesa, kuna wakati mwingine wanashindwa kusaidika na jamii isiyoamini wanakwama.
Anajitolea mfano wa maisha yake, kuna nyakati anakosa pesa hata ya kununulia chakula, huku majirani na watu wanaomfahamu wakiwa hawaamini kama hilo linaweza likatokea kwake.
"Ni mara nyingi na siyo siku moja, nakuwa sina pesa ya kununulia chakula nakaa ndani ama nalala hadi asubuhi, kisha naanza kusaka michongo ya kuingiza kipato, mwanamume huwezi kutoka na kwenda kuomba chakula kwa majirani hasa wakiwa hawakuamini kama unaweza ukakosa," anasema na kuongeza;
"Binafsi sipendi maisha ya maigizo mitandaoni, maana jamii ama watu wanaokuzunguka ukiwaomba pesa huwezi kusaidika wanakuwa wanajua ni utani."
Anasema changamoto nyingine ni kushindwa kufanya biashara ndogo ndogo kama za genge na kulazimika kuweka mtu wa kuzisimamia: "Unajua ili upate faida ni vizuri mwenye biashara kusimama mwenyewe, sasa ukikaa gengeni jinsi jamii inavyokuchukulia unajikuta unashindwa, ukiwa na kibanda cha chipsi ama genge inabidi umpe mtu akuuzie."
Anasema alijaribu kufanya biashara hizo, akajikuta anakumbana na changamoto, huku wengine wanaacha kununua na kusimama kumwangalia: "Ujue na urefu nilionao, mtu anaweza akaja katika biashara zako anasimama tu na kuanza kukuangalia tu."
"Wasiyoyajua watu wengi, kuna vipindi watu maarufu tunapitia changamoto kubwa, kukaa siku nzima bila kula chochote kuanzia asubuhi hadi kuamkia asubuhi nyingine kwangu ni jambo la kawaida, siwezi kutoka nje kwenda kuomba ni mwanamume najikaza," anasema na kuongeza;
Jambo lingine anasema inakuwa ngumu kupata upendo wa kweli kwa watu wanaojulikana, kwani wengi wao wanafuata mvuto wa kazi zao na siyo maisha halisi:
"Mfano ninavyosema inatokea siku unakosa pesa ya kununulia chakula, halafu kaja mwanamke na picha ya kazi yako, unajua nini kitatokea kama siyo kwenda kukutangaza kila mahali."
Anasema zamani akiwa na umri wa miaka 16, kutokana na urefu wake wanawake walikuwa wanamcheka na kumbeza kama hawawezi kuwa kwenye mahusiano na mtu wa aina yake:
"Kauli ile ilinifanya nijiulize maswali mengi sana, moyo wangu uliniuma kupita kiasi, nikajiapiza sitakaa nioe katika maisha yangu, ndiyo maana nimechelewa sana kuingia katika mahusiano.
Anaongeza "Nimeanza mahusiano nikiwa na miaka 27 na mwanamke wa kwanza aliyenitoa uvulana wangu tulikuwa marafiki sana na alikuwa na watoto."
"Baada ya hapo nikapata safari ya kwenda Marekani ambako nilikaa zaidi ya miezi sita, akashindwa kunivumilia akapata mtu mwingine, mimi pia nikapata mzungu ila baada ya kurejea Tanzania umbali ukatufanya tuachane, kwa sasa ninaendelea na maisha mengine na DM zangu zimejaa watu maarufu na wasio maarufu wanaonitongoza."