Maguire kusaini mkataba mpya Man United
Muktasari:
- Maguire ambaye alijiunga na Man United mwaka 2019 akitokea Leicester City kwa ada ya Pauni 85 milioni ameonekana kuwa katika kiwango kizuri tangu kocha Michael Carrick achukue mikoba ya kuifundisha Man United msimu huu hali iliyoibua matumaini ya kupewa dili jipya kwani awali alionekana kuwa huenda angeachwa baada ya msimu kumalizika.
MANCHESTER, ENGLAND: Beki wa Manchester United Harry Maguire amefunguka kuhusu hatma yake katika kikosi cha Manchester United akieleza kuwa katika wiki chache zijazo atakuwa amefikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya wakati ule wa sasa ukimalizika mwisho wa msimu huu.
Maguire ambaye alijiunga na Man United mwaka 2019 akitokea Leicester City kwa ada ya Pauni 85 milioni ameonekana kuwa katika kiwango kizuri tangu kocha Michael Carrick achukue mikoba ya kuifundisha Man United msimu huu hali iliyoibua matumaini ya kupewa dili jipya kwani awali alionekana kuwa huenda angeachwa baada ya msimu kumalizika.
Akizungumzia suala hilo Maguire amesema: “Naamini tutafikia makubaliano yatakayokuwa bora kwa klabu na kwangu pia. Makubaliano hayo mtayajua ndani ya wiki chache zijazo. Maamuzi yatafanyika hivi karibuni iwe nitabaki au nitaondoka. Ninaipenda klabu hii lakini makubaliano yoyote yatakayofanywa ni lazima yawe sahihi kwangu na pia sahihi kwa klabu. Sipendi kubaki kwa sababu ya hisia tu. Nataka kubaki kwa sababu nataka kuisaidia klabu kusonga mbele hivyo nahitaji makubaliano ya hivyo.”
Maguire mwenye umri wa miaka 33 pia amesema kuwa anaamini yeye ni miongoni mwa mabeki wa kati wenye kiwango cha juu kwa sasa na amemshukuru kocha Carrick kwa sababu tangu ajiunge na timu hiyo amemfanya kiwango chake kuwa kikubwa zaidi.
“Huwezi kucheza kwa miaka saba Manchester United chini ya presha kubwa tuliyonayo hasa katika nafasi ya beki wa kati ambapo kila bao unaloruhusu linachambuliwa sana bila ya kuwa mchezaji bora. Ni kweli wakati sikuwa nikipata nafasi Man United bado nilikuwa nachaguliwa timu ya taifa wakati Gareth Southgate akiwa kocha. Kumekuwa na vipindi vya panda shuka katika miaka miwili iliyopita kutokana na majeraha lakini sasa niko katika kiwango changu bora.”