Man United kufanya tena mabadiliko

Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya The Times, inaelezwa Brailsford atapunguza majukumu yake Man United na kurejea katika nafasi yake kama mkurugenzi wa michezo wa Ineos
MANCHESTER, ENGLAND: MKUU wa masuala ya mpira wa miguu wa Manchester United, Dave Brailsford anatarajiwa kujiondoa katika nafasi hiyo ikiwa ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayofanywa na tajiri wa timu hiyo Sir Jim Ratcliffe.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Times, inaelezwa Brailsford atapunguza majukumu yake Man United na kurejea katika nafasi yake kama mkurugenzi wa michezo wa Ineos.
Brailsford kwa sasa ni ndio msimamizi wa shughuli za mpira wa miguu ndani ya Old Trafford na amekuwa katika nafasi hiyo kwa mwaka mmoja akijaribu kuleta mabadiliko kwenye timu hiyo.
Hata hivyo, mambo hayajakuwa mazuri tangu achukue usukani ni majanga makubwa kwake baada ya United kumaliza katika nafasi ya 15, ambayo ni ya chini zaidi kuwahi kukionyesha kwenye EPL.
Man United pia haitashiriki mashindano ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika muongo mmoja msimu ujao baada ya kupoteza fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham kwa kichapo cha 1-0, huku ikimaliza katika nafasi ya 15 katika Ligi Kuu.
Licha ya hayo, Brailsford, mwenye miaka 61, amesifiwa na bilionea wa Uingereza, Ratcliffe kwa kufanyia marekebisho mfumo wa utendaji wa timu hiyo.
Alijihusisha pia kwa kiasi kikubwa katika mpango wa ukarabati wa Pauni 50 milioni wa kituo cha mazoezi cha Man United cha Carrington na kuweka malengo yaliyoainishwa kwenye Mission 21 ili kuhakikisha timu za wanaume na wanawake zinashinda mataji ya ligi.
Kujiondoa kwa Brailsford kunakuja wakati ambapo kampuni ya Ineos inapunguza kujihusisha kwake na michezo.
Katika miezi michache iliyopita pekee, kampuni hiyo ya petroli imesitisha mkataba wake wa udhamini na timu ya taifa ya rugby ya New Zealand.
Tangu Man United iwe chini ya umiliki wa Ineos imekuwa katika misuko suko mingi hususani kwa wafanyakazi wake ambapo kati yao 450 wamefukuzwa kazi kama sehemu ya kubana matumizi.