Mke sababu ya Bruno kukataa bilioni 725 kwa mwaka

Muktasari:
- Timu hiyo ilikuwa imemuweka Fernandes kama kipaumbele katika usajili kabla ya Kombe la Dunia la Klabu ikitaka kumpa mkataba wa mshahara usio na kodi wa Pauni 700,000 (takriban Sh2.5 bilioni kwa wiki pamoja na bonasi kiasi ambacho ni zaidi ya mara tatu ya mshahara wake wa sasa.
MANCHESTER, ENGLAND: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes amevunja ukimya na kueleza kwa nini ameikataa ofa nono kutoka kwa miamba ya Saudi Arabia, Al-Hilal ambayo ingemfanya avute Pauni 200 milioni kwa mwaka (takriban Sh725 bilioni).
Timu hiyo ilikuwa imemuweka Fernandes kama kipaumbele katika usajili kabla ya Kombe la Dunia la Klabu ikitaka kumpa mkataba wa mshahara usio na kodi wa Pauni 700,000 (takriban Sh2.5 bilioni kwa wiki pamoja na bonasi kiasi ambacho ni zaidi ya mara tatu ya mshahara wake wa sasa.
Man United ingeweza kupokea Pauni 100 milioni kama ada ya uhamisho iwapo angekubali kuondoka. Kwa mujibu wa Mail Sport, wakala wa Fernandes, Miguel Pinho alikaa kwa siku tatu katika Hoteli ya Four Seasons mjini Riyadh wiki iliyopita akifanya mazungumzo ana kwa ana na maofisa wa Al-Hilal.
Hata hivyo, juzi Jumanne asubuhi habari ziliripoti kuwa Fernandes amefikia uamuzi wa kukataa ofa hiyo. Kwa nini alikataa? Fernandes ameeleza kuwa: “Rais wa Al Hilal alinipigia simu mwezi mmoja uliopita kuniuliza kuhusu hilo. Kulikuwa na kipindi cha kusubiri ili nitafakari kuhusu mustakabali wangu. Kama nilivyosema siku zote ningekuwa tayari kwenda iwapo Manchester United wangeona inafaa.
“Nilizungumza na kocha Ruben Amorim ambaye katika kipindi chote hicho aliniomba sana nisiende. Klabu ilisema haitakuwa tayari kuniuza isipokuwa labda kama ningeamua kuondoka.”
Fernandes pia alisema moja ya sababu kubwa ya kubaki ni kutaka kuendelea kucheza katika kiwango cha juu akiwa Ulaya.
“Ilikuwa ofa yenye malengo makubwa. Rais wao ni mtu mzuri sana. Hatukuzungumzia kiwango cha fedha mwanzoni, lakini wakala wangu alifanya hivyo.
“Baadaye nilizungumza na mke wangu na familia. Aliniuliza malengo yangu binafsi ni yapi katika kazi yangu. Yeye huwa ananiunga mkono sana. Ingekuwa rahisi kwetu kuhamia, hasa kwa kuwa nina urafiki mkubwa na Joao Cancelo aliyepo Saudi Arabia. Lakini bado nataka kuendelea kucheza katika mashindano makubwa na naamini bado naweza.” Amorim ameendelea kusisitiza kuwa Fernandes ni sehemu muhimu ya mipango yake ya kujenga upya kikosi na kwamba, fedha za kusawazisha bajeti zitatokana na mauzo ya wachezaji wengine kama Antony, Marcus Rashford, Jadon Sancho na Alejandro Garnacho.
Kumekuwapo na sintofahamu miongoni mwa mashabiki kuhusu mustakabali wa Fernandes hasa kutokana na posti zake za hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii na kuonekana kwake pamoja na nyota wa Al-Hilal. Hivi karibuni pia alihudhuria sherehe ya kuzaliwa ya Joao Cancelo, jambo lililozidisha uvumi wa kuondoka kwake. Pamoja na hayo yote, Fernandes amesisistiza kuwa anabaki Ulaya na kushindana katika kiwango cha juu ndicho kitu muhimu zaidi kwake kwa sasa.