Moises Caicedo kubaki Stamford Bridge hadi 2031
Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya The Telegraph, mkataba huo mpya utaongeza muda wa makubaliano yake ya sasa huku pia akitarajiwa kuongezewa mshahara.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Chelsea, Moises Caicedo anatarajiwa kuendelea kubaki katika kikosi hicho kwa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo yenye maskani yake jijini London.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Ecuador mwenye umri wa miaka 24, amekuwa mchezaji muhimu kwa Chelsea, tangu alipojiunga nao akitokea kutoka Brighton mwaka 2023 kwa ada ya Pauni 100 milioni na tangu wakati huo, amecheza mechi 140 katika mashindano yote na kufunga mabao nane.
Caicedo bado ana mkataba wa kuitumikia klabu hiyo kutoka Stamford Bridge hadi mwaka 2031, lakini Chelsea ina nia ya kumwongezea mkataba mpya wenye masilahi bora zaidi, jambo ambalo mchezaji huyo pia amelikubali.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Telegraph, mkataba huo mpya utaongeza muda wa makubaliano yake ya sasa huku pia akitarajiwa kuongezewa mshahara.
Akizungumza mwezi uliopita kuhusu mustakabali wake, amesema: “Nimejikita kwenye klabu yangu kwa sasa. Nina mkataba nayo na nataka kufanya vizuri. Nataka kuwa gwiji wa klabu, Mungu akipenda.”
Habari hizi zimemfurahisha sana kocha wa Chelsea, Liam Rosenior, ambaye amemtaja Caicedo kama mmoja wa viungo bora wa ulinzi duniani. Amesema: "Kwa mtazamo wangu, Moises ni mmoja wa viungo bora wa ulinzi, kama si bora zaidi duniani. Hii ni kutokana na akili yake, nguvu zake, ubora wake kiufundi na namna anavyouelewa mchezo.”
Taarifa hii pia ni faraja kwa klabu hiyo ikizingatiwa baadhi ya wachezaji wameanza kuonyesha kutilia shaka mustakabali wao.
Miongoni mwa mastaa hao ni Enzo Fernandez ambayee hivi karibuni amezungumzia uwezekano wa kujiunga na Real Madrid hali iliyosababisha asimamishwe.
Marc Cucurella naye akiikosoa uongozi wa klabu kuhusu sera yao ya usajili hali iliyoonyesha kwamba anaweza kufikiria kuondoka.