Palmer aikana Man United
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England, alijiunga na Chelsea 2023 akitokea Manchester City kwa dau la pauni 42.5 milioni.
LONDON, ENGLAND: INAWEZEKANA hii ikawa habari njema kwa mashabiki wa Chelsea, kufuatia kiungo mshambuliaji wa matajiri hao wa London, Cole Palmer, kufichua kuwa hana mpango wowote wa kuondoka klabuni hapo huku akisema amekuwa akicheka anaposikia uvumi unaomuhusisha na Manchester United.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England, alijiunga na Chelsea 2023 akitokea Manchester City kwa dau la pauni 42.5 milioni.
Ingawa alitumia miaka 13 katika akademi ya Manchester City, Palmer ni shabiki wa kutupwa wa Manchester United tangu utotoni.
Baada ya kufunga mabao 43 katika mechi 97 katika misimu yake miwili ya kwanza Stamford Bridge, msimu huu amefunga mabao 10 pekee, hali iliyozua mjadala kuhusu kiwango chake kushuka.
Kumekuwa na madai kwamba kupungua kwa kiwango chake kunaweza kusababishwa na kukosa furaha London (homesickness), hali iliyochochea uvumi kwamba Manchester United wanaweza kujaribu kumsajili.
Hata hivyo, Palmer amekanusha yote hayo. “Watu wanazungumza tu,” alisema Palmer. “Nikiona hizo habari nachukua kama utani. Manchester ni nyumbani kwangu, familia yangu iko huko, lakini sijapamisi.”
“Labda nitahisi kumisi nyumbani kama sikwenda kwa miezi mitatu lakini hakuna kitu cha ajabu ninachokosa.”
Palmer aliongeza kuwa hana mpango wa kuondoka Chelsea na alisisitiza kuwa bado wana malengo mengi msimu huu. “Tuna mambo mengi ya kupigania, kama fainali ya FA na pia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya,” alisema.
Palmer pia alisema kwa pamoja na nahodha Reece James wamezungumza na uongozi wa klabu kuhusu usajili wa wachezaji wapya ili kuimarisha kikosi hicho ambacho jana, Jumamosi kilicheza dhidi ya Manchester United.