Mpo? Bukayo Saka anawawahi Madrid

Muktasari:
- Jambo hilo litaongeza mzuka mkubwa kwenye kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta na kuibua matumaini ya kufanya vizuri michuano ya Ulaya na huenda kwenye mechi hiyo ataingia kutokea benchi.
LONDON, ENGLAND: WINGA supastaa, Bukayo Saka anakimbizana na muda kuwahi kipute cha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na itakutanisha timu yake ya Arsenal dhidi ya Real Madrid uwanjani Emirates, Aprili 8.
Jambo hilo litaongeza mzuka mkubwa kwenye kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta na kuibua matumaini ya kufanya vizuri michuano ya Ulaya na huenda kwenye mechi hiyo ataingia kutokea benchi.

Arsenal matumaini yao ni Saka ataweza kucheza mechi hiyo itakayofanyika siku 10 zijazo na huenda akawekwa benchi kwenye mechi ya Fulham itakayopitwa, Aprili 1. Baada ya hapo, Arsenal itakipiga na Everton, Jumamosi ya Aprili 5, kabla ya kukabiliana na Los Blancos kwenye mchezo wa kwanza wa hatua hiyo ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Saka alipata maumivu ya misuli ya paja kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace, Desemba 21 mwaka jana na kufanyiwa upasuaji, ambao umemfanya awe nje ya uwanja kwa kipindi kinachozidi miezi mitatu.

Baada ya miezi mitatu ya kuwa nje ya uwanja, alirejea kufanya mazoezi na wenzake na sasa kuna matumaini makubwa akaanza kutumika baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Kinachoombwa na mabosi wa Arsenal kwa sasa ni Saka asipate majanga mengine ili kuhakikisha wanaikabili Real Madrid ikiwa na wachezaji wake mahiri.

Saka, 23, ni miongoni mwa wachezaji walioipa pigo kubwa Arsenal kutokana na kupata majeruhi yaliyowaweka nje ya uwanja kwa muda mrefu, huku wakali wengine kwenye kikosi hicho cha kocha Arteta waliopata majeruhi na kukaa nje muda mrefu ni Gabriel Jesus, Martin Odegaard, Kai Havertz na Gabriel Martinelli.
Odegaard amesharudi uwanjani huku Martinelli alirejea kwenye mechi dhidi ya Manchester United wiki iliyopita na Saka yupo njiani, huku Jesus na Havertz wameripotiwa wakiwa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu.