Nabi arithi mikoba ya Fadlu Raja
Muktasari:
- Raja imethibitisha ujio wa kocha huyo raia wa Tunisia ambaye amesaini mkataba wa kuinoa hadi Juni 2027, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza muda wa ushirikiano huo.
KOCHA wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi, ametangazwa kuwa kocha mkuu wa Raja Casablanca ya Morocco, ikiwa ni siku chache baada ya klabu hiyo kuachana na Fadlu Davids.
Raja imethibitisha ujio wa kocha huyo raia wa Tunisia ambaye amesaini mkataba wa kuinoa hadi Juni 2027, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza muda wa ushirikiano huo.
Nabi anatua Raja Casablanca akiwa na rekodi ya kutwaa mataji sita akiwa Yanga yakiwemo mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili ya Kombe la Shirikisho (FA Cup) na mawili ya Ngao ya Jamii.
Pia aliifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2023.
Baada ya kuondoka Yanga, Nabi alikwenda Afrika Kusini kuifundisha Kaizer Chiefs ambako aliisaidia kutwaa Kombe la Nedbank na kumaliza kipindi kirefu bila taji.
Uamuzi wa Raja kumchukua Nabi umefuatia kuondoka kwa Fadlu ambaye ameshindwa kuirudisha timu hiyo katika makali yake.
Viongozi wa Raja wanaamini uzoefu wa Nabi katika soka la Afrika na uwezo wa kujenga timu shindani ndio utakaosaidia kurejesha makali ya klabu hiyo katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Kwa mashabiki wa Yanga, jina la Nabi bado lina kumbukumbu kubwa kutokana na mafanikio yake, huku wengi wakifuatilia kwa karibu hatua yake mpya ndani ya moja ya klabu kubwa zaidi Afrika Kaskazini.
Na sasa kocha huyo atakuwa na kibarua kizito huko Casablanca ambacho anakabiliwa kurudia mafanikio aliyoyapata Tanzania kuirejesha Raja kwenye kiwango chake.
Fadlu ameachana na miamba hiyo ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Morocco maarufu kama Batola Pro ikiwa na pointi 42 ipo nyuma ya vinara Fez kwa tofauti ya pointi mbili.