Neymar achagua timu mbili fainali Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Kombe la Dunia litaanza Juni 11, mwaka huu katika nchi za Canada, Mexico na Marekani likishirikisha nchi 48 kutoka mabara yote dunia, ambapo Neymar anataka nchi yake ya nyumbani, Brazil na Argentina zicheze fainali ya Kombe la Dunia, mwaka huu ili wakutane na kikosi cha Lionel Messi.
BRASILIA, BRAZIL: MSHAMBULIAJI wa Santos na Brazil, Neymar Jr amechagua nchi mbili ambazo angependa kucheza nazo katika fainali ya Kombe la Dunia 2026, ingawa hadi sasa hana uhakika wa kuchaguliwa kwenye kikosi kitakachoshiriki michuano hiyo.
Kombe la Dunia litaanza Juni 11, mwaka huu katika nchi za Canada, Mexico na Marekani likishirikisha nchi 48 kutoka mabara yote dunia, ambapo Neymar anataka nchi yake ya nyumbani, Brazil na Argentina zicheze fainali ya Kombe la Dunia, mwaka huu ili wakutane na kikosi cha Lionel Messi.
“Fainali ya Brazil dhidi ya Argentina itakuwa ya ajabu. Bila shaka, nafikiria Kombe la Dunia kama kila mchezaji, ningependa kuwa huko. Natumaini itatokea,” Neymar amesema kama alivyomnukuliwa na Fabrizio Romano.
Neymar anatarajia kujumuishwa katika kikosi cha mwisho cha Brazil na kocha Carlo Ancelotti, ambapo amesisitiza kuwa mshambuliaji huyo wa Santos yupo katika njia sahihi za maandalizi kuelekea fainali hizo ikizingatiwa kwamba hana majeraha yoyote yanayotishia mustakabali wake.
Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid aliweka wazi kuwa utimamu wa mwili wa Neymar ndio utakaokuwa kigezo sambamba na majeraha ambayo awali yalimuandama kwa muda mrefu.
“Ana muda mfupi kuonyesha bado ana ubora wa kucheza Kombe la Dunia lijalo. Naamini anaweza kurejea katika asilimia 100. Nimesema hapo awali, na nitakuwa wazi ni wachezaji walio tayari kimwili tu watakaoitwa," alisisitiza kocha huyo.
“Baada ya jeraha lake la goti, Neymar amerejea vizuri; anafunga mabao. Anahitaji kuendelea katika mwelekeo huu na kuboresha utimamu wake wa mwili. Yuko katika njia sahihi.”
Neymar ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Brazil, akiwa na mabao 79 na asisti 59 katika mechi 128 za kimataifa za wakubwa.