Neymar kwenye rada ya Ligi Kuu Marekani
Muktasari:
- Zaidi ya suala la anakoelekea kipindi hiki anachopitia Neymar kinafungua mlango wa maisha yake ya soka, kwani iwapo atafanikiwa kutua MLS na hasa timu kama Cincinnati hatakabiliwa na ufuatiliwaji na vyombo vya habari mara kwa mara bali changamoto ya kiushindani kikosini.
CINCINNATI, MAREKANI: WANASEMA kila mtu na bahati yake. Kuna kila dalili zinaonyesha supastaa wa Kibrazili, Neymar, anaweza kuwa anafikiria mabadiliko mapya katika maisha yake ya soka na safari hii akitarajiwa kutua Marekani akakipige kwenye Ligi Kuu (MLS).
Licha ya ukweli kwamba wengi wanaamini bado ana uwezo wa kucheza Kombe la Dunia 2026, kutokuwepo kwake hivi karibuni katika timu ya taifa ya Brazil kumeibua shaka na kwa muktadha huo tetesi za uwezekano wa kubadilisha ligi zimepata nguvu, huku MLS ikiingia kwenye mjadala.
Ikiwa kuna jambo moja ambalo Neymar amelidhihirisha katika hatua hii, ni hana mpango wa kupotea kwenye ramani kwa sababu licha ya ukosoaji bado anataka kubaki kuwa na ushawishi, na hatua ya kimkakati inaweza kuwa muhimu kufanikisha hilo.
Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha FC Cincinnati imeanza mawasiliano na wawakilishi wa mchezaji huyo ili kupata uwezekano wa kumsajili, na taarifa hizo zimewavutia wengi, hasa kwa sababu siyo timu ambayo wengi wangetarajia. Timu kama Inter Miami ambako Lionel Messi anacheza zilionekana kuwa chaguo bora zaidi kwa wengi.
Ingawa wazo la kumuona Neymar akicheza MLS linaendelea kupata mvuto kuna mambo muhimu yanayofanya uhamisho wa haraka kuwa mgumu, ikiwamo mkataba wake na Santos na kuna kipengele vha kifedha kinachofanya iwe vigumu kuondoka kwa muda mfupi.
Zaidi ya hilo, kuna mambo mengine ikiwamo sheria za mishahara, mipaka ya kikosi na taratibu za kiutawala ambazo zinaathiri moja kwa moja mazungumzo yoyote. Kwa nyota wa kiwango cha dunia kama Neymar mambo hayo yanaweza kuchelewesha au kurefusha mchakato.
Zaidi ya suala la anakoelekea kipindi hiki anachopitia Neymar kinafungua mlango wa maisha yake ya soka, kwani iwapo atafanikiwa kutua MLS na hasa timu kama Cincinnati hatakabiliwa na ufuatiliwaji na vyombo vya habari mara kwa mara bali changamoto ya kiushindani kikosini.