Neymar anaandaliwa akakipige Kombe La Dunia 2026
Muktasari:
- Kocha wa Santos, Cuca amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kumweka mchezaji huyo katika kiwango cha juu kwa ajili ya michezo ijayo.
SAO PAUL, BRAZIL: NYOTA wa Brazil, Neymar amefanyiwa matibabu maalum ya goti wakati wa mapumziko ya kimataifa ili kumweka katika hali bora kuelekea Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kocha wa Santos, Cuca amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kumweka mchezaji huyo katika kiwango cha juu kwa ajili ya michezo ijayo.
Neymar alikosa mchezo dhidi ya Flamengo pamoja na mechi ya Copa Sudamericana dhidi ya Deportivo Cuenca, lakini kocha wake alisisitiza ni sehemu ya maandalizi ya muda mrefu.
Tiba aliyofanyiwa ni ya PRP (Platelet-Rich Plasma), ambayo hutumia damu ya mchezaji mwenyewe kuharakisha uponaji wa misuli na viungo.
“Tunataka kumjenga ili aweze kucheza michezo 13 mfululizo bila matatizo,” amesema Cuca.
Hata hivyo, mbali na afya, Neymar anakabiliwa na changamoto za kinidhamu baada ya kumshambulia kwa maneno mwamuzi Savio Pereira Sampaio kutokana na uamuzi tata katika mechi moja.
Shirikisho la Soka Brazil linachunguza tukio hilo na adhabu yoyote inaweza kuathiri maandalizi yake ya kuelekea Kombe la Dunia.
Licha ya changamoto hizo, matarajio ni kumuona Neymar akiwa fiti na katika kiwango cha juu atakachoweza kulivutia benchi la timu ya taifa ya Brazil kuelekea mashindano hayo makubwa duniani.