Palace yaichapa Man City, yabeba Kombe la FA

Muktasari:
- Bao la Eberechi Eze alilofunga kipindi cha kwanza lilitosha kuizima Man City na hivyo kuweka rekodi ya kumaliza msimu bila ya taji la kimashindano kwa mara ya pili tangu kocha Pep Guardiola achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo.
LONDON: CRYSTAL Palace imebeba taji la Kombe la FA baada ya kuichapa Manchester City bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Wembley.
Bao la Eberechi Eze alilofunga kipindi cha kwanza lilitosha kuizima Man City na hivyo kuweka rekodi ya kumaliza msimu bila ya taji la kimashindano kwa mara ya pili tangu kocha Pep Guardiola achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Hii pia inakuwa ni mara yapili katika maisha ya ukocha ya Guardiola kumaliza msimu bila kushinda taji lolote la kimashindano.
Palace imefanikiwa kushinda kombe hili kwa mara ya kwanza katika historia baada ya kufika fainali mara mbili.
Mara yamwisho kwa Palace kucheza fainali ya michuano hii ilikuwa msimu wa 2015-16 ambapo ilikutana na Manchester United na ikapoteza.
Mbali ya kushindwa kuambulia taji lolote msimu huu, Man City pia ipo kwenye hatari ya kutoshiriki hata michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao kutokana na nafasi yao kwenye ligi endapo itashindwa kushinda mechi zilizobaki kwenye Ligi Kuu England.
Hadi sasa matajiri hawa wa Jiji la Manchester wanashika nafasi ya sita wakiwa na pointi 65 tofauti ya alama moja na Aston Villa ambayo ipo kwenye nafasi ya tano ambayo timu itakayomaliza hapo inafuzu Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo, Man City ina faida yakuwa na mchezo mmoja mkononi ambao ikishinda itapanda nafasi ya tano kwa tofauti ya alama mbili.