Pep: Tukifuzu UEFA tunashukuru

Muktasari:
- Man City imekuwa na msimu mbaya baada ya kubeba taji la Ligi Kuu England kwa misimu minne mfululizo na jana Jumamosi ilishuka uwanjani Etihad kukipiga na Brighton - ikiwa kwenye nafasi ya tatu, huku wapinzani wao hao wakiwa pointi moja nyuma.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola amesisitiza kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu yatakuwa mafanikio makubwa sana Manchester City.
Man City imekuwa na msimu mbaya baada ya kubeba taji la Ligi Kuu England kwa misimu minne mfululizo na jana Jumamosi ilishuka uwanjani Etihad kukipiga na Brighton - ikiwa kwenye nafasi ya tatu, huku wapinzani wao hao wakiwa pointi moja nyuma.
Guardiola alisema: “Brighton ni moja ya klabu bora ndani na nje ya uwanja. Nafasi waliyopo kwenye ligi kwa sasa ni kwa sababu wanafanya mambo yao vizuri na wastahili kuwepo hapo walipo.
“Na Bournemouth, na Aston Villa, na Newcastle, na pengine Fulham nao watakuwapo hapo kwenye vita ya kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya – ni timu nzuri. Haishangazi, nadhani wanastahili. Ni wazuri sana, wapo kwenye viwango vizuri kwa muda mrefu na wana silaha hatari wanapocheza.”
Man City ilipoteza nafasi ya kupanda kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya wikiendi iliyopita kuchapwa na Nottingham Forest, washindani wengine kwenye tiketi ya kuwania kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Guardiola alisema: “Yatupaswa tupambane kufikia viwango vya juu kufuzu michuano ya Ulaya msimu ujao. Tunapaswa kuwa kwenye viwango vizuri kwa kadri inavyowezekana. Mechi nyingi ni ngumu, hivyo yatupasa kufanya vizuri ili kutumiza lengo.”
Msimu mbaya wa Man City haukuishia tu Ligi Kuu England, bali hadi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na ilitupwa nje kuwania kutinga hatua ya 16 bora na Real Madrid.