Refa aanguka uwanjani kisa joto Copa America

Muktasari:

  • Mwamuzi msaidizi, Humberto Panjoj alianguka uwanjani kwenye mechi baina ya Canada na Peru iliyofanyika juzi Jumanne.

OTTAWA, CANADA. WACHEZAJI wa Canada wamebainisha wasiwasi wao juu ya usalama wa wachezaji kwenye fainali za Copa America baada ya mwamuzi kuanguka uwanjani kutokana na joto kali.

Mwamuzi msaidizi, Humberto Panjoj alianguka uwanjani kwenye mechi baina ya Canada na Peru iliyofanyika juzi Jumanne.

Tukio hilo lilitokea kwenye kipindi cha kwanza ambapo wachezaji kadhaa walikimbia kwa mwamuzi kumpa msaada wa haraka.

Kipa Maxime Crepeau alikuwa wa kwanza kwenda kumsaidia Panjoj wakati kona ilipokuwa ikipigwa kwenye upande wa pili.

Uzuri ni kwamba refa huyo alikuwa amechoka, lakini anapumua. Kipa Crepeau alisema: "Nilifurahi kwa sababu alichoka, lakini alikuwa anapumua.

"Nimesikia kwamba anaendelea vizuri, tunashukuru Mungu. Lakini, tunahitaji kulijadili hili.

"Sijali watu wanasema nini, lakini afya za watu waliopo uwanjani ni kitu muhimu, tunahitaji kulitazama hilo kwa kina."

Panjoj ameripotiwa kuendelea vizuri baada ya tukio hilo la kuanguka uwanjani. Hali ya hewa ya joto la uwanjani Children's Mercy Park, Kansas liliripotiwa kuwa juu kiasi cha 38°C.

Na wachezaji na waamuzi hawakuwa na mapumziko ya kunywa maji kwenye kipindi cha kwanza.

Beki wa Canada, Alistair Johnston alisema: "Hizi ni zile aina ya mechi kwamba hali ya hewa inakuwa mbaya kuliko adui yako."

Na badala yake, mapendekezo ya wengi ni kubadili muda wa kuanza kwa mechi hizo. Canada ilishinda 1-0, shukrani kwa bao la Jonathan David.