Skauti kibao waenda kumtazama Ronaldo Jr

Muktasari:
- Kinda huyo mwenye umri wa miaka 14 alivaa jezi Namba 7 katika mechi hiyo, alishangiliwa wakati anaingia uwanjani kutokea benchini katika mechi ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya timu ya taifa ya Japan kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 15, Jumanne.
ZAGREB, CROATIA: SKAUTI wa klabu kibao za Ulaya ikiwamo Manchester United walikwenda kumtazama mtoto wa supastaa Cristiano Ronaldo, Cristiano Ronaldo Jr wakati alipocheza mechi yake ya kwanza ya timu ya taifa ya Ureno kwa vijana chini ya miaka 15 ili kuona kama ana ubora wa kunaswa haraka.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 14 alivaa jezi Namba 7 katika mechi hiyo, alishangiliwa wakati anaingia uwanjani kutokea benchini katika mechi ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya timu ya taifa ya Japan kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 15, Jumanne.
Akivaa jezi yenye namba sawa aliyokuwa akivaa baba yake kwa awamu zote mbili alizokuwa Old Trafford, Ronaldo Jr alionyesha kiwango bora kwenye kipindi cha pili katika mashindano ya Vlatko Markovic huko Croatia. Benchi la ufundi la Man United lilituma skauti wake kwenda kumtazama mchezaji huyo na huenda likamtazama tena kwenye mechi zijazo za Ureno dhidi ya Ugiriki au England.
Man United inafahamu uwezo wa mchezaji huyo baada ya kudumu kwenye akademia yao kwa miezi 14, wakati alipokuwa timu moja na mtoto wa Wayne Rooney, Kai.
Wapinzani wa Man United kwenye fainali ya Europa League itakayopigwa Bilbao, Tottenham nayo ilituma skauti wake kumtazama kinda huyo, pamoja na klabu 10 za Bundesliga nazo zilienda kuona uwezo wa Ronaldo Jr.
Gazeti la Ureno Sportske Novosti liliripoti kwamba Bayern Munich, Borussia Dortmund, RB Leipzig, Hoffenheim, Red Bull Salzburg, Inter Milan, Juventus na Atalanta zilituma skauti wake kwenda kutazama mechi hiyo, ambayo Ronaldo Jr alikuwa kivutio kutokana na uwezo wake alionyesha.
Fowadi wa Braga, Rafael Cabral alikuwa staa wa mchezo baada ya kufunga hat-trick.