Timu ya Mbappe yashuka, mashabiki wawaka

Muktasari:
- Jumatano wiki hii, Mbappe na timu yake ya Real Madrid waliondolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na Arsenal baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-1.
PARIS, UFARANSA: MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Kylian Mbappe ameendelea kuandamwa na jinamizi baada ya mashabiki wa timu ya Caen anayoimiliki iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Pili Ufaransa (Ligue 2) kushuka daraja na kuibua hasira.
Jumatano wiki hii, Mbappe na timu yake ya Real Madrid waliondolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na Arsenal baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-1.
Lakini, kwa mashabiki wa Caen wamemgeukia nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa wakimtuhumu kuisahau timu hiyo ambayo anaimiliki hasa baada ya kutimkia zake Hispania mwimu huu alikojiunga na Real Madrid. Caen imeshuka na sasa itashiriki Ligi Daraja la Tatu (National 1).
Katika kilele cha wiki ya huzuni kwa Mbappe, Caen walipoteza kwa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Martigues, juzi Ijumaa na kupoteza matumaini ya kubaki Ligue 2 wakiwa na michezo mitatu iliyosalia.
Hiyo ni mara ya kwanza tangu 1984 kwa Caen kushuka chini ya madaraja mawili ya juu ya soka la kulipwa nchini humo.
Mbappe ambaye kampuni ya familia yake Interconnected Ventures ilinunua asilimia 80 ya klabu hiyo Septemba 2024, sasa anakabiliwa na hasira ya mashabiki wanaomlalamikia kutokana na hali mbaya inayopitia timu hiyo. Mashabiki wa Caen walionyesha mabango mazito yenye ujumbe usemao: Uongozi, wachezaji wote mna hatia, tokeni wote; (Caen) Malherbe ni sisi, uchafu ni nyinyi.”
Hasira hizo zimekuwa zikijengeka tangu msimu uliopita, ambapo dirisha la usajili lilifanyika kwa namna haikuwafurahisha mashabiki, jambo ambalo hata wachezaji walilikosoa.
Nahodha wa timu hiyo, Romain Thomas aliwahi kusema: “Ni mara ya kwanza nimepitia hali hii kabla ya msimu (kumalizika). Kumekuwa na hali ya hewa nzito kila siku. Kila mchezaji hana uhakika wa mustakabali wake.” Baada ya matokeo kuendelea kuwa mabaya, mashabiki walimshambulia Mbappe kwa mabango yaliyosomeka: Mbappe, Caen siyo toi lako, huku mangine yakiandikwa ‘Kabla ya kuangazia kimataifa, heshimu waliopo nyumbani.’
Kilio hicho kiliongezeka Februari, mwaka huu wakati Mbappe alipofika kwenye kambi ya mazoezi baada ya kufunga hat-trick dhidi ya Man City, lakini alikumbana na mabango yaliyomkejeli mfano ni lile lililoandikwa: Hammoud jiuzulu. Mko wapi?; Fayza (mama yake na wakala wa Mbappe), Caen wako kwenye shimo refu.
Hali hiyo imechochewa zaidi na matamshi ya wachezaji kama mshambuliaji Alexandre Mendy, aliyesema baada ya kichapo kutoka Paris FC: “Tunaambulia kile tulichopanda. Tangu mwanzo, msimu huu haukuwa mzuri na wala hakuna nguvu mpya kikosini”.
Kwa sasa, Mbappe anakabiliwa na ukosoaji mkubwa - si tu kama mchezaji wa kiwango cha juu, bali pia kama mwekezaji ambaye kwa mara ya kwanza ameonekana kushindwa nje ya uwanja. Na kwa mashabiki wa Caen, msimu huu umeacha doa ambalo hata jina kubwa la Mbappe haliwezi kufuta haraka.