Tuchel avujisha kikosi cha England, Danny Welbeck yumo
Muktasari:
- Suala linalozua gumzo kubwa zaidi ni kujumuishwa kwa mshambuliaji mkongwe wa Brighton, Danny Welbeck ambaye mara ya mwisho aliichezea timu ya taifa ya England miaka minane iliyopita (ushindi wa 1-0 dhidi ya Switzerland huko King Power Stadium).
KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya England, Thomas Tuchel, anatarajiwa kuwasilisha orodha ya awali ya wachezaji 55 kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026. Hata hivyo, majina matatu ya wachezaji watakaokuwemo kwenye orodha hiyo yamevujishwa mapema.
Suala linalozua gumzo kubwa zaidi ni kujumuishwa kwa mshambuliaji mkongwe wa Brighton, Danny Welbeck ambaye mara ya mwisho aliichezea timu ya taifa ya England miaka minane iliyopita (ushindi wa 1-0 dhidi ya Switzerland huko King Power Stadium).
Kwa sasa mshambuliaji huyo ana miaka 35, lakini amekuwa na msimu bora zaidi, akifunga mabao 14 kwenye mashindano yote chini ya kocha Fabian Hurzeler.
Mabao ya mshambuliaji huyo yameiongezea Brighton kupata pointi 13 muhimu. Pia ndiye mchezaji wa England anayeongoza kwa mabao Ligi Kuu (mabao 13), akilingana na Morgan Gibbs-White wa Nottingham Forest.
Mbali na Welbeck, gazeti la The Telegraph limethibitisha kuwa mabeki wawili Luke Shaw (Manchester United) na Jarrad Branthwaite (Everton) nao wamo kwenye orodha hiyo.
Kwa sasa, mdahalo mkubwa nchini England ni nani atakayekuwa msaidizi wa Harry Kane katika safu ya ushambuliaji. Ingawa Dominic Calvert-Lewin na Dominic Solanke walijumuishwa kwenye kikosi cha Tuchel mwezi Machi, fomu ya sasa ya Welbeck na Ollie Watkins inampa Welbeck nafasi kubwa ya kufanya maajabu.
Brighton kwa sasa inapambana kuwania nafasi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ikiwa nyuma kwa pointi tatu dhidi ya Bournemouth inayoshika nafasi ya sita, huku zikiwa zimesalia mechi mbili pekee.
Nafasi ya sita inaweza kutoa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iwapo Aston Villa itamaliza ndani ya tano bora na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Europa League.
Mei 22, 2026, Thomas Tuchel anatarajiwa kutangaza kikosi chake cha mwisho cha wachezaji 26.