Usajili wa Anderson watikisa England
Muktasari:
- Manchester City ilithibitisha imefikia makubaliano na Nottingham Forest kumsajili Anderson, huku taratibu za mwisho za uhamisho zikitarajiwa kukamilika baada ya kumaliza majukumu yake kwenye Kombe la Dunia.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO Elliot Anderson atakuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya Uingereza baada ya kukamilika kwa uhamisho wake wa pauni 116 milioni kutoka Nottingham Forest 116 kwenda Manchester City.
Manchester City ilithibitisha imefikia makubaliano na Nottingham Forest kumsajili Anderson, huku taratibu za mwisho za uhamisho zikitarajiwa kukamilika baada ya kumaliza majukumu yake kwenye Kombe la Dunia.
Mwaka 1979, Nottingham Forest iliweka rekodi ya uhamisho wa gharama kubwa zaidi nchini Uingereza kwa kumnunua Trevor Francis kutoka Birmingham City, na kumfanya kuwa mchezaji wa kwanza nchini humo kununuliwa kwa ada ya pauni1 milioni.
Safari hii, Nottingham Forest ndiyo itakayopokea ada ya rekodi, huku Anderson akivunja rekodi ya pauni milioni 105 ambayo Arsenal ililipa kumsajili Declan Rice miaka mitatu iliyopita.
Tangu ajiunge na Nottingham Forest akitokea Newcastle United miaka miwili iliyopita kwa ada ya pauni milioni 35, Anderson amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho. Aidha, ameanza katika kila mechi ya England chini ya kocha Thomas Tuchel kwenye Kombe la Dunia.
Kubeba hadhi ya kuwa mchezaji wa gharama kubwa zaidi katika historia huja na presha pamoja na matarajio makubwa.
Hivyo basi, je, Anderson anastahili kweli ada hiyo kubwa ya uhamisho?
Uhamisho huo unamfanya Anderson kushika nafasi ya tatu katika orodha ya usajili ghali zaidi Ligi Kuu England akiwa nyuma ya Alexander Isak na Florian Wirtz walio mbele yake kwa kiwango cha ada iliyolipwa.
Hata hivyo, utafiti mpya uliofanywa na mtaalamu wa masuala ya fedha usajili, Kieran Maguire kwa kushirikiana na Profesa Jason Laws unaonyesha kuwa Anderson angekuwa katika nafasi ya 31 ikiwa ada za usajili wa zamani zingerekebishwa kulingana na uwezo wa matumizi wa klabu kwa sasa.
Tofauti na tafiti nyingi zinazotumia mfumuko wa bei wa kawaida, mfumo huu mpya unazingatia ongezeko kubwa la mapato ya Ligi Kuu England katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Kwa mujibu wa wataalamu hao, mapato ya ligi yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 3,500, jambo ambalo limebadili kabisa uwezo wa vilabu kutumia fedha kwenye usajili wa wachezaji.
Kwa kutumia kipimo hicho, usajili wa Alan Shearer kutoka Blackburn Rovers kwenda Newcastle United mwaka 1996 kwa pauni15 milioni ndio unaochukuliwa kuwa ghali zaidi katika historia ya Ligi Kuu England.
Ingawa kiasi hicho kinaonekana kidogo kwa viwango vya sasa, thamani yake kwa mazingira ya leo inakadiriwa kufikia pauni237 milioni.
Nafasi ya pili inashikiliwa na usajili wa Juan Sebastian Veron, aliyenunuliwa na Manchester United mwaka 2001 kwa pauni 28 milioni, ambao leo ungekuwa na thamani ya pauni 199 milioni. Rio Ferdinand anafuata baada ya kuhamia Manchester United mwaka 2003 kwa pauni33 milioni, usajili ambao sasa ungekuwa na thamani ya pauni 179 milioni.
Usajili wa Stan Collymore kutoka Nottingham Forest kwenda Liverpool mwaka 1995 unashika nafasi ya nne kwa thamani ya sasa ya pauni179 milioni, huku Fernando Torres akifuata baada ya uhamisho wake kutoka Liverpool kwenda Chelsea, ambao ungekuwa na thamani ya pauni177 milioni kwa viwango vya leo.
Majina mengine yanayopatikana ndani ya 10 bora ni Dennis Bergkamp, Andy Cole, Andriy Shevchenko, Dwight Yorke na Paul Pogba, hali inayomaanisha kuwa nusu ya wachezaji katika 10 bora walikuwa usajili wa Manchester United.
Rio Ferdinand pia anaonekana kwa mara ya pili ndani ya 15 bora kupitia usajili wake wa kwanza kutoka West Ham United kwenda Leeds United mwaka 2001. Ada ya pauni 18milioni aliyogharimu wakati huo sasa ingekuwa na thamani ya pauni 140milioni. Kwa jumla, usajili wake mara mbili ungekuwa na thamani ya pauni339 milioni kwa mujibu wa Laws-Maguire Index.
Miongoni mwa wachezaji wa sasa wa Premier League walio ndani ya 20 bora kwa kipimo hicho ni Alexander Isak, Jack Grealish, Moises Caicedo na Enzo Fernandez.
Kwa ujumla, utafiti huo unaonyesha kuwa ingawa ada za usajili zimekuwa zikiongezeka kila mwaka, ukilinganisha na uwezo wa kifedha wa klabu katika nyakati husika, baadhi ya usajili wa zamani ulikuwa mzito zaidi kifedha kuliko usajili wa kisasa. Hivyo, licha ya Anderson kuwa mmoja wa wachezaji waliogharimu fedha nyingi zaidi kwa thamani halisi ya ada, katika kipimo kinachozingatia nguvu ya matumizi ya klabu anashuka hadi nafasi ya 31.