Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya DR Congo yamuibua Vicent Company

Muktasari:

  • Wiki hii, kocha wa Bayern Munich, Mbelgiji Vincent Kompany, ambaye baba yake alizaliwa Bukavu nchini DR Congo, aliulizwa kuhusu mzozo huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Vita vinavyoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) vimekuwa mjadala mkubwa ulimwenguni ukigusa nyanja ya michezo Ulaya na Marekani.

Wiki hii, kocha wa Bayern Munich, Mbelgiji Vincent Kompany, ambaye baba yake alizaliwa Bukavu nchini DR Congo, aliulizwa kuhusu mzozo huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

"Mimi ni Mbelgiji kwa asilimia 100 na asilimia 100 Mkongo. Baba yangu alizaliwa mashariki mwa Kongo. Bibi yangu anatoka Bukavu, eneo la Kivu mashariki mwa Kongo. Matumaini yangu ni kwamba watu waweze kurejea nyumbani kwao ili waweze kuishi maisha ya amani.

"Moyo wangu ni wa Kongo kwa asilimia 100 na mawazo yangu na salamu zangu za heri zinakwenda kwa familia zinazoteseka huko kwa sasa," amesema Kompany.

Mbali na Kompany, wachezaji wengi vijana wenye asili ya Kongo wanaocheza barani Ulaya wameanza kuzungumzia vita hiyo na ukosefu wa usalama uliodumu kwa miongo kadhaa mashariki mwa Kongo.

Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya DR Congo, Youssouf Mulumbu, fowadi wa Real Betis, Cédric Bakambu, na Simon Banza wa Trabzonspor, wamekashifu kile wanachoeleza kuwa ni ukimya wa dunia kuhusu mzozo ambao umegharimu maisha ya mamilioni ya watu.

Kwa Kompany, suala hilo ni la kibinafsi. Akiwa kocha wa Bayern Munich, pia anahusishwa na ushirikiano unaoendelea wa klabu hiyo na Rwanda.

Mapema Februari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Thérèse Kayikwamba aliziandikia Bayern Munich, Arsenal, na Paris Saint-Germain (PSG), akizitaka kusitisha mikataba yao ya udhamini na "Tembelea Rwanda," akitaja wasiwasi kwamba mpango huo unaweza kuhusishwa na unyonyaji haramu wa madini kutoka maeneo yenye migogoro nchini DR Congo.

Barua hiyo ilisema kwamba: "Hatia ya Rwanda katika mzozo imekuwa isiyopingika baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa kufichua kuwepo kwa wanajeshi 4,000 wa Rwanda wanaofanya kazi nchini DRC." Waziri wa Mambo ya Nje amelaani zaidi janga la kibinadamu linaloendelea, na kusisitiza kwamba:

"Maelfu ya watu kwa sasa wamenasa katika Jiji la Goma huku kukiwa na upungufu wa upatikanaji wa chakula, maji na usalama. Maisha ya wasio na hatia yamepotea; ubakaji, mauaji na wizi vinatawala. Mfadhili wako anahusika moja kwa moja na masaibu haya. Ikiwa si kwa dhamiri yako, basi vilabu vinapaswa kufanya hivyo (kumaliza makubaliano yao ya ufadhili) kwa waathiriwa wa uvamizi wa Rwanda."

Rwanda imekanusha mara kadhaa kuhusika moja kwa moja katika mzozo huo na kutupilia mbali madai kwamba inaunga mkono kundi la waasi la M23.

"Visit Rwanda" imekuwa mfadhili wa Arsenal tangu 2018, kwa mkataba wa thamani ya zaidi ya Euro milioni 12 kwa mwaka. PSG ilitia saini makubaliano kama hayo mwaka 2019, yakiendelea hadi 2025 na kuleta euro milioni 15 kila mwaka. Bayern Munich ilijiunga mwaka 2023 kwa ushirikiano wa miaka mitano wa maendeleo ya soka na utangazaji wa utalii. Ombi sawa na hilo lilitolewa kwa Kamishna wa NBA, Adam Silver, akitaka kuangaliwa upya kwa uhusiano wa ligi hiyo na Rwanda.


Kufikia sasa, hakuna klabu yoyote iliyojibu hadharani ombi la DRC. Bayern Munich imetuma wafanyakazi wawili nchini Rwanda kufuatilia hali ilivyo na iko katika mawasiliano na Ofisi ya Mambo ya Nje ya Ujerumani.

Wakati huo huo, ghasia katika Kivu Kaskazini na Kusini zimeongezeka. Waasi wa M23 wamepanua udhibiti wao, huku mapigano makali mjini Goma yakisababisha vifo vya watu 8,500 kufikia mwisho wa Januari, kulingana na serikali ya Kongo.

Huku mzozo huo ukiendelea kuongezeka, athari zake sasa zinafikia kiwango cha kimataifa, si tu katika siasa na diplomasia, bali pia katika ulimwengu wa michezo.