Vita ya Waarabu ipo hapa fainali CAFCC
Muktasari:
- Fainali hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kutokana na ubora wa timu zote mbili, itaanza kupigwa Mei 9, 2026 kwa USM Alger kuwa wenyeji wa mechi hiyo, huku ile ya marudiano itakayoamua bingwa ikipigwa Misri, Mei 16, 2026.
MACHO na masikio ya wadau wa soka kwa sasa, yanaelekezwa katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, itakayohusisha timu zote za Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika, kwa maana ya Waarabu wa USM Alger ya Algeria dhidi ya Zamalek SC ya Misri.
Fainali hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kutokana na ubora wa timu zote mbili, itaanza kupigwa Mei 9, 2026 kwa USM Alger kuwa wenyeji wa mechi hiyo, huku ile ya marudiano itakayoamua bingwa ikipigwa Misri, Mei 16, 2026.
USM Alger ilifuzu fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Olympique Safi ya Morocco, ikinufaika na faida ya bao la ugenini, katika mechi iliyochelewa kuanza kwa dakika 80, kutokana na kutawaliwa na vurugu.
Katika mechi hiyo, ilianza pia kwa wachezaji kupoteza muda kwa kujifanya wameumia na wakati mwingine wakipinga uamuzi wa mwamuzi, huku chupa na fataki zikirushwa uwanjani na kusababisha moshi mkubwa kuzuka na hali ya sintofahamu.
Ahmed Khaldi aliifungia USM Alger bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, ingawa, Safi ilisawazisha dakika ya 75, kupitia kwa Msenegali Moussa Kone, likiwa ni la sita kwake katika michuano hiyo.
Timu hizo, zilikuwa zote kundi moja la A msimu huu na USM Alger ilimaliza kinara na pointi 14, baada ya kushinda mechi nne na kutoka sare mbili kati ya sita iliyocheza, huku Olympic Safi, ikimaliza nafasi ya pili na pointi zake 13.
Katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi, Olympic Safi, ilichapwa bao 1-0, kwao Morocco, Novemba 28, 2025, huku ile ya marudiano iliyopigwa Algeria, Februari 14, 2026, zikatoka suluhu (0-0), hivyo, kukutana tena hatua hiyo ya nusu fainali.
Kwenye Hatua ya robo fainali, USM Alger iliitoa AS Maniema Union ya DR Congo kwa faida ya bao la ugenini, baada ya sare ya jumla ya mabao 2-2, kama ilivyotokea pia kwa Olympic Safi, iliyoiduwaza Wydad Casablanca ya Morocco kwa jumla ya 3-3.
Kwa upande wa Zamalek, iliongoza kundi D na pointi 11, ikiungana na Al Masry ya Misri iliyomaliza ya pili na pointi 10, iliyoishia robo fainali kwa kutolewa na CR Belouizdad ya Algeria kwa bao la ugenini, baada ya sare ya jumla ya bao 1-1.
Katika hatua ya robo fainali, Zamalek iliitoa AS Otoho ya Congo Brazzaville kwa kuifunga jumla ya mabao 3-2, kisha nusu fainali ikaenda kukutana na CR Belouizdad ya Algeria na kuitoa kwa jumla ya bao 1-0, hivyo, kutinga fainali hiyo kibabe.
FAINALI SIO YA KINYONGE
Katika fainali ya msimu huu, timu hizo zote zinakutana zikiwa sio wanyonge, kwani zimeshawahi kutwaa taji hilo na USM Alger imechukua mara moja, ambayo ilikuwa msimu wa 2022–2023, ambao utaendelea kukumbukwa na mashabiki wa Tanzania.
Msimu huo, utaendelea kukumbukwa na wadau wa soka Tanzania, kwani ilishuhudiwa USM Alger, ikitwaa taji hilo kwa faida ya bao la ugenini, baada ya kuifunga Yanga, iliyokuwa kwenye kiwango bora chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.
Kwa msimu huo, Yanga ilichapwa nyumbani mechi ya kwanza mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Mei 28, 2023, kisha kushinda Algeria kwa bao 1-0, Juni 3, 2023 na kukosa taji hilo kubwa Afrika kwa faida ya bao la ugenini.
Ubingwa huo kwa USM Alger, uliiongezea makali kikosi hicho, kwani ilienda kutwaa pia CAF Super Cup mwaka 2023, baada ya kuishangaza Al Ahly ya Misri kwa kuichapa bao 1-0, likiwa ni taji la kwanza pia kwa timu hiyo katika mashindano hayo.
Kwa upande wa Zamalek, inasaka taji hilo la Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya tatu, baada ya kutwaa mara mbili hadi sasa, ikianzia msimu wa 2018–2019, ilipoichapa RS Berkane ya Morocco kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya jumla ya bao 1-1.
Taji lingine la Kombe la Shirikisho Afrika ambalo Zamalek ililichukua ambalo ni la pili kwake, ni la msimu wa 2023–2024, ilipoichapa tena RS Berkane ya Morocco kwa faida ya bao la ugenini, baada ya miamba hiyo kutoka sare ya jumla ya mabao 2-2.
Zamalek ni klabu ya pili kwa mafanikio makubwa katika mashindano ya CAF baada ya majirani zao wa Cairo, Al Ahly, ikiwa imeshinda 13, yakiwemo, mawili ya Kombe la Shirikisho, ikikabiliwa na kibarua cha kupambana na kikosi cha USM Alger.