Si rahisi kuendesha lebo ya muziki

Muktasari:
- Oktoka 10 mwaka huu (kesho kutwa) lebo ya mwimbaji wa Bongofleva, Harmonize, Konde Music Worldwide (Kond e Gang) inakwenda kutimiza miaka minne tangu kuanzishwa kwake Alhamisi ya Oktoba 10, 2019.
Oktoka 10 mwaka huu (kesho kutwa) lebo ya mwimbaji wa Bongofleva, Harmonize, Konde Music Worldwide (Kond e Gang) inakwenda kutimiza miaka minne tangu kuanzishwa kwake Alhamisi ya Oktoba 10, 2019.
Konde Music ilikuja baada ya Harmonize kuachana na WCB Wasafi, lebo yake Diamond Platnumz ambapo ndio ilimtoa kimuziki mwaka 2015, kupitia wimbo wake maarufu, ‘Aiyola’.
Ndani ya miaka minne Konde Music imeweza kusimamia wasanii saba ambao ni Harmonize, Ibraah, Country Boy, Anjella, Cheed, Killy na Young Skales kutoka Nigeria.
Utakumbuka Aprili 11, 2020 ndipo Konde Music walitangaza kumsaini msanii wa kwanza ambaye ni Ibraah, Mei 8 mwaka huo akaachia Extended Playlist (EP) yake, Steps ikiwa na nyimbo tano alizowashirikisha Joeboy, Skibii na Harmonize.
Akizungumzia kwa ufupi safari hiyo ya miaka minne nje ya lebo iliyomtoa kimuziki, Harmonize alisema: “Haikuwa kazi rahisi, kuna wakati wa kucheka, kulia, kuteleza, kuamka, kufikiri nje ya boksi na kuona mwanga pia. “Lakini muhimu mashabiki wamekuwa pamoja nasi bila kujali vipindi vyote hivyo, ama kwa kujua au kutokujua wametuunga mkono siku zote, binafsi ninawashukuru na kuwaheshimu sana, wao ni sehemu ya Konde Gang.
“Juhudi zao zimeifanya lebo ya Konde Music kuwa kubwa Afrika Mashariki.”
Kuhusu siku ya maadhimisho ambayo ni Oktoba 10, alisema: “Tunatarajia kufanya jambo kubwa katika siku hiyo ikiambatana na kuhitimu baadhi ya members (wanachama) wa Konde Music”, jambo linaloonyesha kuwa kuna wasanii wataachana nao.
Harmonize pia ameweka wazi azma ya lebo hiyo kusaini wasanii wapya hivi karibuni.
Mafanikio ya Konde Music
Sehemu ya kwanza ya mafanikio ya lebo hii ni albamu ya kwanza ya Harmonize tangu kuanza muziki, Afro East iliyotoka Machi 2020.
Albamu hiyo ina nyimbo 18 alizowashirikisha wasanii kama Mr Blue, Lady Jaydee, Morgan Heritage (Jamaica), Khaligraph Jones (Kenya), Phyno, Skales, Yemi Alade, Mr Eazi na Falz wote kutoka Nigeria.
Baada ya mwaka mmoja Harmonize akatoa albamu nyingine, High School ikiwa na nyimbo 20 na kuwashirikisha wasanii sita ambao ni Anjella, Ibraah na Sholo Mwamba, Sarkodie (Ghana), Naira Marley (Nigeria) na Busiswa (Afrika Kusini).
Septemba 2020 Country Boy aliachia EP yake, The Father yenye nyimbo saba, huku Seyi Shay, Snymaan, Skales na Harmonize wakishirikishwa, aliipa jina hilo kwa madai ametoa motisha kwa kizazi kipya katika muziki na mitindo. Hii ilikuwa ni EP ya pili chini ya Konde Music baada ya ile ya Ibraah, Steps.
Utakumbuka Ibraah alipewa tuzo na kipindi cha Empire cha E FM Radio kama msanii bora chipukizi kwa mwaka 2020, lakini msanii huyu hajawahi kushinda tuzo yoyote ya muziki ya ndani wale nje. Chini ya Konde Music Ibraah ametoa albamu moja, The King of New School yenye nyimbo 17, iliyotoka Julai 2022 na kuwashirikisha Maud Elka, Christian Bella, L.A.X, Waje, AV, Roberto na Bracket.
Waimbaji Cheed na Killy waliojiunga Konde Music Septemba 2020 wakitokea King’s Music ya Alikiba nao kila mmoja ametoa EP yake na kumshirikisha Harmonize. Cheed akaachia ‘Endless Love’ na Killy, ‘The Green Light’, kwa ujumla ndani ya miaka minne Konde Music wametoa albamu tatu na EP tatu.
Magari kwa wasanii
Konde Music wamekuwa na utaratibu wa kuwapatia magari wasanii wake, ambapo Julai 2021 Harmonize alimpatia gari Angella aina ya Crown, hiyo ni baada ya Ibraah, Country Boy na meneja wa Ibraah, Jose wa Mipango kupatiwa magari aina hiyo.
Changamoto
Januari 2022 Konde Music walitangaza kumalizika kwa mkataba kati yao na Country Boy baada ya mwaka mmoja wa kufanya kazi pamoja, walimalizana vizuri bila mzozo kama ambavyo imekuwa baadhi ya wasanii na lebo zao hivi karibuni. Hata hivyo, kwa mujibu wa Country Boy mkataba wake na Konde Music ulikuwa wa miaka mitano, lakini aliamua kuachana na lebo hiyo baada ya kuona waliyokubaliana hayatekelezwi. Miongoni mwa makubaliano ni pamoja na kupeleka muziki wake kimataifa kwa kumtafutia kolabo na wasanii wakubwa wa nje. Pia alipoteza nafasi ya kutumbuiza kwenye shoo nyingi kama za vyuo ambazo alikuwa anahitajika kutokana na Konde Music kuhitaji fedha nyingi, ambazo aliona haikuwa sawa kwa kiwango cha muziki wake. Licha ya kuachana vizuri, Country Boy alipoteza zaidi ya Sh12 milioni kwa mchakato wa kuhama kampuni ambayo ilikuwa inasambaza muziki wake chini ya Konde Music na kwenda kampuni mpya chini ya lebo yake, I Am Music. Changamoto nyingine ambayo imekuwa ikiwasumbua ni video zao kuondolewa YouTube kutokana malalamiko ya hakimiliki, video zao nyimbo kama ‘Ni Wewe’ wa Killy, ‘Uno’, ‘Sandakalawe’, ‘Amen’ za Harmonize na ‘Kioo’ wa Anjella zimekutana na hilo.
Ukame wa tuzo
Tangu kuanzishwa kwake, hakuna msanii wa Konde Music ambaye ameshinda tuzo ya yoyote ya kimataifa ingawa Harmonize amekuwa akitajwa kuwania tuzo kama Afrimma (Marekani) na Afrima (Nigeria).Katika tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021 zilizotolewa Aprili mwaka huu, Harmonize pekee ndiyo aliibuka kidedea.