Abigail chams shoo 5 za nguvu zakumfananisha na Beyonce

Muktasari:
- Wapo wasanii wanaojua kuimba lakini linapokuja suala la kufanya shoo, wanachemka na hasa zile za moja kwa moja ‘live’ stejini na hapa kuna wakali wake.
KATIKA burudani, suala la kuimba ni lingine na kufanya shoo ni lingine.
Wapo wasanii wanaojua kuimba lakini linapokuja suala la kufanya shoo, wanachemka na hasa zile za moja kwa moja ‘live’ stejini na hapa kuna wakali wake.
Wapo wengi, lakini ukimtaja mwanamama Beyonce wa Marekani, hapa ndipo mahala pake, na ndiyo linapokuja suala la nani wengine wanaweza kama yeye.
Ukiwasikiliza mashabiki wa burudani Bongo, wanamtazama msanii Abigail Chams kama nyota inayokuja kwa kasi na hasa katika upande wa shoo. Wamebambika. Wameshikwa na shoo zake na baadhi wameshindwa kuficha hisia zao wakifunguka wazi ni ‘Beyonce ‘ wa muziki wa Bongo Fleva na Afrika.
Wamevutiwa na kiwango chake kikubwa cha ubunifu, sauti ya kuvutia, na uwepo wa jukwaani usio na kifani na ameitikisa Afrika Mashariki hasa kwa wimbo wake wa ‘Me Too’ alioutoa hivi karibuni akimshirikisha Harmonize ‘Konde Boy’.
Wimbo huo umetoka mwezi mmoja sasa na unafanya vizuri Tanzania na ukishika namna moja kwenye chati mbalimbali nchini Kenya na pamoja wamejiita ‘Grammy Gang’ wakidhamiria kuileta tuzo kubwa za muziki duniani kama Grammy kutokana na wimbo huo.

Mwanamuziki huyo fundi wa kupiga alama za muziki amefanya shoo mbalimbali lakini hizi tano zimewakosha mashabiki wengi na Mwanaspoti limekuandikia na kuweka maoni yao.
1. Glitch Sessions
Glitch Africa ni jukwaa lenye ushawishi mkubwa linaloandaa maonyesho ya muziki wa moja kwa moja (Live Performance) na Podcast maarufu zaidi barani Afrika na wasanii mbalimbali kutoka Afrika wanatumia jukwaa hilo kuonyesha uwezo wao wa kuimba live, nyota kama Asake, Davido, Fido, Ibraah, Joel Lwaga walipafomu kwa nyakati mbalimbali.
Mapema mwezi huu Abigail alipafomu kwenye jukwaa hilo akiimba nyimbo mbili, Muhibu na Nani ambayo alishirikiana na Marioo na hivi ndivyo mashabiki walivyotoa maoni katika mtandao wa YouTube.
mmoja aliandika; “Best performance Abigail umetisha sana kwenye live performance pokea maua yako mapema.”
Mwingine akaongeza; “Naiona Grammy ikija Bongo kupitia huyu Abigail ni mwanamuziki haswa.”
“Kibongo bongo huyu ndio anajua kuimba live”
namaliza wiki sasa namsikiliza huyu dogo, ana kitu ni New Generation ya Vanessa endelea kupambana,” aliandika shabiki mwingine.
Huyu ndio akamaliza kabisa kwa kumfananisha na Beyonce; “Huyu ni Beyonce wa Afrika, Grammy inakuja Tanzania.”
2.Tuzo za TMA
Mbali na kushiriki na kuwania kwenye Tuzo za Muziki (TMA), mwanamuziki huyo alikuwa miongoni mwa wasanii waliopafomu kwenye usiku wa Oktoba 19 mwaka 2024. Shoo hiyo iliwashika pia mashabiki hasa kutokana na alivyopafomu live na hivi ndivyo mashabiki walivyomzungumzia;
-”Msanii pekee anayejua namna ya kupafomu live,”
-”Hongera sana mdogo wetu. Unatuheshimisha sana sisi ndugu zako Watanzania.”
-”Napenda live kama hivyo, nyie ambao hamjamuelewa mmezoea masingeli tulieni.
-”Yani Abigail alifanya kitu cha tofauti sanaaa yaani hongera, namuona Beyonce wa Bongo.”

3.Dar es Salaam
Usiku wa April 28, 2024 nyota huyo alifanya shoo jijini Dar es Salaam iliyokuwa Live mbali na kuimba alionyesha umahiri wake wa kucheza na vyombo. Jambo hilo la kutumia vyombo liliwavutia wengi na hawa ni baadhi walioonyesha hisia zao.
-”Hongera sana Abigail Chams Best Performance..makubwa nasubiri kushuhudia katika sanaa yako ya muziki...nataka kuona zaidi ya ulichofanya.”
-”Hizi ndio shoo, sio wale wa kushotooo kuliaaa kushotoo kulia.”
-”Aisee huyu ni msanii ni vile Tanzania hatumpi sikio, kama Beyonce vile yaani.”
4. Siku ya watoto Duniani
Mwaka 2020 alipafomu kwenye kilele cha siku ya watoto duniani, LIVE at Expo 2020 Dubai na aliimba wimbo mmoja ‘Reimagine’ wenye ujumbe wa kuwapambania watoto na uliwavutia wengi na wengine wakaacha ujumbe kwenye mtandao wa YouTube wakisifia shoo hiyo.
-”Hongera unaliwakilisha taifa letu, wewe ndo Beyonce wa bongo.”
-”Abigail Chams ni msanii anayejua kupafomu live bila kutetereka na watu tunainjoi.”
-”Nani amegundua anafanana na Christina Shusho hongera sana Abigail naipenda nchi yangu.”

5. Half Time Shoo ya BAL
Ijumaa ya Mei 26, 2023 alitumbuiza kwenye fainali za Mpira wa Kikapu barani Afrika (BAL) katika Mji wa Kigali, Rwanda. Shoo hiyo iliwabamba mashabiki wa nchi mbalimbali kuonyesha anachofanya ni kipaji halisi na atazidi kukaa juu.
-”Endelea hivyo Abby, siku moja utakaa juu ya dunia ukiwaangalia wengine kutoka huko.”
-”Nenda, nenda, nenda endelea kung’aa Kenya tunakupenda na tunaamini utafanya zaidi ya Vanessa Mdee.”