Hamisa Mobetto afurahia ujauzito wake

Muktasari:
- Hayo yameibuka baada ya mwanadada huyo ambaye hivi karibuni aliolewa na mchezaji wa Yanga Aziz KI, kutupia picha mtandaoni ambayo iliwafanya wajuzi wa mambo kuikagua vilivyo na kuhitimisha kuwa ni mjamzito.
MWANAMITINDO Hamisa Mobetto ameibua gumzo kufuatia muonekano wake wa sasa unaomuonyesha akiwa na dalili zote za kuwa mjamzito.
Hayo yameibuka baada ya mwanadada huyo ambaye hivi karibuni aliolewa na mchezaji wa Yanga Aziz KI, kutupia picha mtandaoni ambayo iliwafanya wajuzi wa mambo kuikagua vilivyo na kuhitimisha kuwa ni mjamzito.
“Kitumbo bado hakijatoka kivile lakini ana kila dalili kwamba amenasa mimba. Ukitaka kujua kwamba kweli ana ujauzito angalia mashavu yake, pua na hata sehemu ya kifuani, unaona kabisa ana kitu tumboni,” alisema Ashura muuza nguo Magomeni baada ya kuiona picha hiyo
“Hivi ndio inatakiwa mwanamke anabeba mimba mapema baada ya ndoa, asisubirie kukaa miaka tele japo kupata mimba ni jambo la majaliwa ya Mungu,” alikomenti mdau mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Zizaclassic kwenye mtandao wa Instagram.
Mwingine akaandika: “Waoo kipenzi cha watu wengi zaa mama… zaa umzalie Azizi Ki, pesa ya kukuhudumia anayo.”.
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu madai hayo ya ujauzito, Hamisa alisema, hili ni jambo la kheri na kupata ujauzito mapema kwenye ndoa changa ni jambo la furaha sana hivyo kama anayo watu wasubirie wataiona maana mimba huwa haijifichi.
“Jamani ujauzito ni kitu cha furaha sana kwetu, na hizo taarifa zimenifurahisha sana, hivyo kama ninayo si mtaiona jamani, kupata mtoto mwingine kwangu furaha itaongezeka maana mimi na mume wangu tumekutana tunapenda watoto na bahati nzuri hata pesa ya kuwalea tunayo,” alisema Hamisa.