Hamisa Mobetto, Rich Mavoko watoweka pamoja

MIAKA mitano iliyopita Hamisa Mobetto aliamua rasmi kuingia kwenye Bongofleva baada ya kufanya vizuri upande wa mitindo na urembo tangu mwaka 2010 aliposhinda taji lake la kwanza la Miss XXL, After School Bash.

Kwa kipindi kirefu Hamisa alikuwepo katika familia ya muziki akitokea kwenye video za wasanii, mfano alifanya kazi na Quick Rocka, My Baby (2013) na Diamond Platnumz, Salome (2016). 

Ukiachana na mitindo na urembo, Hamisa ni video vixen na mwigizaji aliyejaribu bahati yake kwenye Bongofleva kama ilivyo kwa kina Gigy Money, Amber Lulu, Lyyn, Nai, Caren Simba, Snura, Shilole, Rose Ndauka n.k. 

Hata hivyo, kabla ya uamuzi wake tayari sauti yake ilikuwepo masikioni mwa wengi bila kujulikana, ni pale alipoingiza sauti cha chini (back vocal) katika wimbo wa Diamond Platnumz, Nikifa Kesho (2013) na WCB Wasafi, Jibebe (2018).

Na kufika Agosti 2018 ndipo Hamisa akaachia wimbo wake wa kwanza ‘Madam Hero’ uliotengenezwa na Prodyuza C 9, huku Januari 2019 akifanya shoo yake ya kwanza pamoja na mastaa wengine kama Lady Jaydee, Aslay, Christian Bella na Ruby.

Licha ya ukosolewaji mkubwa Hamisa aliendelea na muziki hadi alipotoa EP yake, Yours Truly (2022) ikiwa na nyimbo sita na hadi sasa ameshirikiana na wasanii kama Diamond, Christian Bella, Seneta Kilaka, Whozu, Otile Brown, Korede Bello na Singah.

Ila ghafla Hamisa ameondoka kwenye muziki, mwaka wote wa 2023 hakutoa wimbo wowote, tangu alipoachia EP yake Mei 2022, hajatoa kazi nyingine zaidi ya kuachia video ya wimbo ‘Murua’  Hapo Desemba 2022 kutoka katika EP yake, Yours Truly.

Hamisa anakaa kimya kimuziki wakati alikuwa ndio anaanza kupata mafanikio, mfano mwaka 2020 alifikisha ‘streams’  1.4 milioni Boomplay Music na kupata wasikilizaji 221,000 waliotumia muda saa 67.4 kusikiliza muziki wake.

Lakini sasa ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu bila kutoa kazi mpya, kwa msanii ambaye bado alikuwa anajitafuta katika tasnia, ni wazi kuna sehemu anapoteza kufuatia ukimya wake huo.

Upande wa pili Rich Mavoko naye ametimiza mwaka mmoja bila kutoa wimbo wowote, wimbo wake wa mwisho kuachia uitwao ‘Stamina’ ulitoka Novemba 27, 2022, kwa kifupi mwaka 2023 naye hakutoa kazi yeyote.

Hata hivyo, huu umekuwa kama utaratibu kwa Rich Mavoko sasa tangu alipojiondoa WCB Wasafi, kipindi anajiandaa kuachia Minitape (2020) na albamu yake, Fundi (2022), pia alikaa kimya kimuziki na mtandaoni kwa muda mrefu.

Pengine Rich Mavoko amechukua mapumziko ya kimuziki kwani mwishoni mwa mwaka 2022 ndipo alipoachia albamu yake ‘Fundi’ yenye nyimbo 16 huku akiwashirikisha wasanii kama Fid Q, Phina, Masauti, H_art The Band n.k.

Kumbuka siku zote Mavoko anapokaa kimya kimuziki basi hutoweka na kwenye mitandao ya kijamii tofauti na wasanii wengine, mathalani alipoachia wimbo wake wa mwisho (Stamina) hakuchapisha chochote Instagram kwa zaidi ya miezi sita.

Rich Mavoko na Hamisa hawatakuwa wasanii wa kwanza Bongo kuchukua mapumziko ya kimuziki, Alikiba aliwahi kukaa kimya kwa miaka miwili hadi aliporejea kwa kishindo na wimbo wake, Mwana (2014) ambao ndio ulikuwa wa  kwanza chini ya RockStar Africa.

Wimbo huo ulikuwa na mafanikio makubwa katika muziki na matunda ya kukaa kwake kimya yakaonekana, mfano video yake iliyotoka Desemba 19, 2014 ndio video yake iliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote ikiwa na ‘views’ zaidi 33 milioni.

Ila tangu Mavoko aondoke WCB Wasafi takribani miaka mitano iliyopita akiwa ni msanii wa kwanza kufanya hivyo katika historia ya lebo hiyo, nguvu yake katika muziki hajawa kama ile aliyokuwa nayo mwanzo.

Harmonize na Rayvanny ambao walifuata nyayo zake, Rich Mavoko alijiunga WCB Wasafi akiwa tayari ni msanii mkubwa aliyetamba na nyimbo kali kama Silali, Marry Me, Follow Me, Pacha Wangu, One Time n.k.

Na hata ndani ya WCB Wasafi alitoa nyimbo maarufu kama Ibaki Stori, Kokoro ft. Diamond Platnumz, Rudi ft. Patoranking n.k, huku akishirikishwa na Harmonize katika wimbo wake, Show Me. Ila sasa muziki wake unaenda tofauti na kabla na baada ya kusaniwa WCB Wasafi. Rich Mavoko alijiunga WCB Wasafi yake Diamond Platnumz, mwaka 2016 na kuondoka mwaka 2018 kwa mvutano mkubwa hadi kufikishana Baraza la Sanaa Taifa (Basata) ili kupata usuluhishi. 

Na kwa mujibu wa Rich Mavoko, yeye hakulipa fedha WCB Wasafi kama walivyofanya Harmonize na Rayvanny lakini video zote za nyimbo ambazo alitoa chini ya lebo hiyo kama Ibaki Stori, Kokoro, Rudi n.k, zimeondolewa katika mtandao wa YouTube.