Kajala, Paula na rekodi zao Bongo fleva

Muktasari:
- Licha ya kuwa mwigizaji aliyetamba na filamu kama Kijiji Cha Tambua Haki (2012) akiwa na Steven Kanumba, Kajala ana historia yake katika muziki wa Bongofleva na wasanii wake kwa miaka 20 sasa. Fahamu zaidi.
ALIZALIWA na kukulia Oysterbay, Dar es Salaam ambapo wazazi wake wote walikuwa anafanya kazi Polisi. Kabla ya kubatizwa alipewa jina la Kajala na baada ya kubatizwa akaitwa Winfrida, hivyo majina yake matatu ni Winfrida Kajala Masanja.
Licha ya kuwa mwigizaji aliyetamba na filamu kama Kijiji Cha Tambua Haki (2012) akiwa na Steven Kanumba, Kajala ana historia yake katika muziki wa Bongofleva na wasanii wake kwa miaka 20 sasa. Fahamu zaidi.
1. Kajala alipokuwa sekondari alikuwa mwanafunzi mtundu na miongoni mwa waliokuwa marafiki zake ambao ni mastaa katika muziki ni pamoja na Dogo Hamidu ambaye kwa sasa anajulikana kama Nyandu Tozzy. Ni Dogo Hamidu ambaye aliingizwa katika kundi la Hotpot Family na Soggy Doggy, rapa mwenye albamu tano kisha baadaye akajiunga na kundi la Dar Skendo lake Dudu Baya.

2. Kajala alisoma Sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam na alikuwa akicheza sana mpira wa kikapu wakati huo. Miongoni mwa mastaa aliosoma nao shuleni hapo ni rapa Witness a.k.a Kibonge Mwepesi. Witness ni miongoni mwa wanawake waliofanya vizuri katika muziki wa Hip Hop na alikuwa mshindi wa Coca-Cola Popstar 2004 wakiunda kundi la Wakilisha na wezake wawili ambao ni Langa na Shaa. Pia alishinda tuzo ya Channel O 2008.
3. Ndani ya Club Bilicanas ndipo alikutana na mzazi mwenzake P-Funk Majani. Kwa mujibu wa Kajala siku hiyo Majani alimwambia wakapate chakula cha usiku (dinner), kisha akajikuta nyumbani kwake na kuanza kuishi pamoja.

4. Kajala na Majani waliishi palepale ilipokuwa Bongo Records na wasanii wa mwanzo bibie kuwaona studio hapo wakati huo alikuwa ni Ferooz na Juma Nature ambaye ni msanii wa kwanza kusainiwa Bongo Records.
5. Akiwa na umri wa miaka 19, Kajala akajaliwa mtoto wake wa kwanza na wa pekee, Paula ambaye ametokea katika video tatu za msanii wa Bongofleva na mzazi mwenzake, Marioo ambazo ni Lonely (2023), Tomorrow (2023) na Sing (2023).
Ikumbukwe tangu Marioo ametoka kimuziki na wimbo wake ‘Dar Kugumu’ (2018), Paula, binti wa Kajala na Majani ndiye mrembo pekee ambaye ametokea mara nyingi katika video za Marioo, mwanzilishi wa lebo ya Badnation.
6. Inaelezwa wimbo wa Madee ‘Yote Maisha’ uliotengenezwa na Majani ambaye pia sauti yake inasikika katika kiitikio chake pamoja na mwanzoni (intro), ulikuwa kwa ajili ya Kajala ambaye aliishi pamoja na Majani kwa takriban miaka minane.
7. Siku ya kwanza Madee anampeleka MB Dogg kwa Majani ili kurekodi, Kajala ndiye aliyewafungulia geti la kuingia Bongo Records, studio iliyokuja kumtoa kimuziki na kufanya vizuri na albamu yake ya kwanza, Si Uliniambia (2005) yenye nyimbo 10.
8. Na kazi kubwa aliyofanya Majani ilimfanya MB Dogg kushinda tuzo mbili za mwanzo kutoka Tanzania Music Awards (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2005 na Albamu Bora ya Mwaka (Si Uliniambia) 2006.

9. Kipindi Country Wizzy anatafuta kutoka kimuziki na hana fedha, Kajala ndiye alimlipia gharama za kurekodi studio baada ya kumsikia akichana na kuvutiwa na uwezo wake.
Rapa huyo ambaye amewahi kusainiwa na lebo za L.F.L.G (Live First Live Good) na Konde Music Worldwide, wimbo aliolipiwa na Kajala unaitwa ‘You the One’ na ulirekodiwa mwaka 2010 kwa Lamar wa Fishcrab.
10. Hadi sasa Kajala ndiye mwanamke ambaye Harmonize kamwimbia sana katika nyimbo zake. Kipindi penzi lao limepamba moto alimuimbia nyimbo kama Deka (2022) na Nitaubeba (2022). Na alipomuumiza na kuachana akamtolea nyimbo kama Mtaje (2021), Vibaya (2021) na You (2022).