Rayvanny: Kufulia? Mtasubiri sana!

Muktasari:
- Rayvanny ameliambia Mwanaspoti, hajawahi kuwa tajiri na hivyo kwa sasa ndio ameanza kuitafuta hela yake kwa kuanza kufanya kazi mwenyewe, na kwamba yeye sio msanii wa kuanika maisha yake.
NYOTA wa muziki wa Bongo Fleva, Rayvanny amefunguka ishu ya watu kudai kuwa amefilisika, akidai wanaotamani hilo litokee, watasubiri sana kwani hajawahi kuwa tajiri hata mara moja.
Rayvanny ameliambia Mwanaspoti, hajawahi kuwa tajiri na hivyo kwa sasa ndio ameanza kuitafuta hela yake kwa kuanza kufanya kazi mwenyewe, na kwamba yeye sio msanii wa kuanika maisha yake.
“Mimi ni mmoja ya wale wasanii ambao sidhani kama wanaweka sana wazi mambo ya uchumi au maisha binafsi, ndio maana ni vigumu mtu kujua kama niko sawa kiuchumi au nimefulia, kwa sababu nina usiri wa maisha siku zote, hivyo naamini pia pesa inatafutwa nikiitafuta inakuja na inatumiwa na ukishaitumia inatoweka, huwezi kutafuta pesa ukaiweka ndani unaiangalia tu kama runinga,” alisema Rayvanny na kuongeza;
“Sasa hiyo ishu ya kuambiwa nimefulia, ni lini nilitangaza kuwa tajiri au nina pesa nyingi? Kwanza ishu ya kufilisika sioni kama tatizo kubwa sana kwani hata kampuni kubwa huwa zinayumba.”
Akijibu madai ya kutosikika baada ya kutoka lebo WCB, alisema yuko mbioni kuandaa vitu vipya.
Kwa sasa siko sana kwenye mitandao kama zamani, sababu kuna mipango naiweka sawa ya kutoa kazi nzuri kwa mashabiki wangu, nataka wapate ladha ya kitu kizuri nikiwa najisimamia mwenyewe na sio kuwa kwenye lebo ya mtu,” alisema Rayvanny.