Martha Mwaipaja, Angel Magoti kazi ipo

Muktasari:
- Baadhi ya wasanii waliopenya katika tuzo hizo zitakazofanyika Mei 23 ni pamoja na Martha Mwaipaja na Angel Magoti ambao watachuana na wenzao wengine watatu katika kipengele cha Mwimbaji Bora wa Kike wa miondoko hiyo ya Injili.
JUMLA ya kazi 529 za wasanii wa muziki wa Injili zimepokewa na Waandaaji wa Tuzo za Muziki wa Injili nchini (TGMA), ili kuanza mchakato wa kupata wakali watakaotunukiwa heshima siku ya hafla ya ugawaji wa tuzo hizo utakaofanyika mwezi ujao, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wasanii waliopenya katika tuzo hizo zitakazofanyika Mei 23 ni pamoja na Martha Mwaipaja na Angel Magoti ambao watachuana na wenzao wengine watatu katika kipengele cha Mwimbaji Bora wa Kike wa miondoko hiyo ya Injili.
Msemaji wa TGMA, Harris Kapiga aliyasema hayo juzi kwenye ofisi za Baraza la Sanaa nchini (Basata), akieleza hatua iliyofikia katika uandaaji wa tuzo hizo tangu walipozitambulisha Februari 7, mwaka huu.
Kapiga alisema tuzo hizo zitakazofanyika kwa mara ya kwanza zitatolewa Mei 23 na wamefurahi kuona mwamko wa wasanii katika kutuma kazi zao na imewatia moyo ikizingatiwa tuzo hizo ni mpya kabisa.
“Tumepokea kazi takribani 529 za wasanii mbalimbali wa muziki wa Injili kupitia mfumo maalumu na ukafanyika mchujo kwa kupiga kura kupata watu watano katika kila kipengele kwa vipengele 20 vilivyoainishwa,” alisema Kapiga.
Baadhi ya vipengele alivyovibainisha ni pamoja na wimbo bora wa kuabudu wa injili, wimbo bora wa sifa, wimbo bora wa injili wa mwaka pamoja na wimbo bora wa injili wa kimataifa, pia Mwimbaji bora wa kiume, muimbaji bora wa kike, muimbaji bora chipukizi pamoja na muimbaji bora wa nyimbo za injili wa jumla.
“Kuna kipengele cha Albamu bora, mtayarishaji bora, kolabo bora, mtunzi na muandaaji bora wa muziki wa injili wa mwaka,” alisema Kapiga na kubainisha baadhi ya waliofanikiwa kupenya katika vipengele hivyo kwa upande wa mwimbaji bora wa kike wa nyimbo za injili ni pamoja na Angel Magoti, Rehema Simfukwe, Stella Mhombo, Martha Mwaipaja na Miriam Mauki.
Kwa upande wa muimbaji wa waimbaji bora wa kiume aliwataja John Kavishe, Japhet Zabron, Joel Lwaga, Paul Clement na Obby Apha ndio wamefanikiwa kupenya kuwania tuzo hiyo, huku kwa mtunzi bora walioteuliwa ni Bernard Mukasa, Herman Mchome, Jeaphet Zabron, John Lisu na Obby Alpha.
Aliongeza kutakuwa pia na tuzo maalum kwa ajili ya mtu aliyechangia ukuaji wa mziki wa injili ambaye mshindi atapatikana kwa kuteuliwa na kamati ya majaji.
“Baada ya mchakato wa mchujo hatua inayofuata ni wasanii watapewa namba zao kwa ajili ya kupigiwa kura ili kupatikana mshindi, kura zitachukua asilimia 40 na 60 zilizobaki zitachukuliwa na majaji ili kuamua mshindi katika kila kipengele,” alisema Kapiga.
Alisema kuwa mchakato wa tuzo hizo umefikia asilimia 80 hadi sasa na siku ya kilele cha tuzo hizo na kuongeza lengo la kuzitoa ni kuwatia moyo wasanii wa muziki wa injili na kwamba mwaka huu kazi zote zilizopokelewa ni zile zilifanywa mwaka 2024 tu.