Mbosso aiombea Tanzania tuzo za hifadhi Afrika

Muktasari:
- Tanapa imeingiza Hifadhi 10 katika vipengele nane tofauti ambapo zitachuana na hifadhi nyingine kutoka Afrika katika kuwania tuzo hizo, ambapo upigaji kura utafikia tamati Mei 4 mwaka huu.
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limeingiza Hifadhi 10 kuwania tuzo za hifadhi bora Afrika, huku msanii Mbwana Yusuph 'Mbosso' akiomba wananchi kupigia kura kwa wingi ili Tanzania kuibuka kinara.
Tanapa imeingiza Hifadhi 10 katika vipengele nane tofauti ambapo zitachuana na hifadhi nyingine kutoka Afrika katika kuwania tuzo hizo, ambapo upigaji kura utafikia tamati Mei 4 mwaka huu.
Hifadhi hizo zilizoteuliwa ni Kitulo katika kipengele cha hifadhi bora kwa fungate, Serengeti, Kilimanjaro, Nyerere, Katavi, Ruaha, Arusha, Mahale, Tarangire na Udzungwa huku kila upande ukiwa na kipengele chake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupigia kura hifadhi zote, Mbosso alisema Kitulo ni moja ya hifadhi bora zenye vitu vya tofauti ikiwamo ndege wanaotoka nchi za nje na wanyama ambao si wakali.
"Nilifanyia wimbo wangu hapa wa 'Tamu' nilifurahia mandhari ya hifadhi hii, tumepata fursa ya kupata Hifadhi 10 kwenye tuzo Afrika, naomba Watanzania wapige kura Tanzania ipate heshima yake.
"Hii ni sifa kwetu kuona tunapata fursa kubwa kama hizi, wasanii, watu mbalimbali kwa kila mmoja kwenye nafasi yake tushiriki kupiga kura kwa wingi tumuunge mkono Rais Samia," alisema Mbosso.
Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa uhifadhi na mkuu wa kitengo cha maendeleo ya biashara Tanapa, Jully Lyimo, alisema hiyo ni historia ya kwanza kuingiza hifadhi 10 katika kuwania tuzo Afrika.
Alisema sababu kubwa ni utendaji kazi bora wa serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii na juhudi za Rais Samia kwenye kampeni ya kutangaza vivutio nchini ikiwamo 'Royal Tour'.
"Mbali na hizo hifadhi, tuna kipengele cha Tanzania kuwa eneo muhimu la utalii, tunaposhinda nchi inapata fursa kiuchumi na ajira kupitia utalii, naomba tushiriki zaidi kupiga kura," alisema Jully.
Jully aliongeza kuwa awali walikuwa wakiingiza hifadhi mbili pekee, za Serengeti na Mlima Kilimanjaro ambazo kwa pamoja zilishinda mara sita mfululizo tangu 2019 hadi 2024.
Naye Mkuu wa Hifadhi ya Kitulo Kamishna msaidizi, Harry Gazi alisema hifadhi hiyo ni ya kipekee kwa utalii ikiwa na mandhari nzuri yenye vivutio bora na huduma nzuri kwa mtalii.
"Eneo hili ni maalumu kwa fungate, wale wapenzi walionuniana wakifika huku wanarudiana haraka, tunayo maua ambayo ni adimu Afrika, hatuna wanyama wakali, tupigieni kura tushinde kipengele chetu," alisema Gazi.