TUONGEE KISHKAJI: Teknolojia ni laana na baraka kwa sanaa

Muktasari:
- Na hii ilikuwa lazima kwa sababu studio hazikuwepo babu, zilikuwa chache. Na sio studio tu, zamani ili ngoma itambe ilikuwa lazima ichezwe kwenye redio za majayanti na hizo redio zilikuwa na mambo mengi ikiwemo kuulizwa ngoma umerekodi wapi na jibu ilikuwa ni lazima iwe umerokedi kwa majayanti… vinginevyo hakuna atakayechukua CD yako kuicheza redioni.
ZAMANI ilikuwa ili msanii wa muziki aweze angalau kurekodi wimbo, ni lazima apambene kufika studio za ‘majayanti’ kama kina P Funk au Master Jay. Na akifika hapo inabidi awahakikishie kwamba kweli ana kipaji kisha majayanti wakimkubali ndio anaingizwa booth, anarekodi.
Na hii ilikuwa lazima kwa sababu studio hazikuwepo babu, zilikuwa chache. Na sio studio tu, zamani ili ngoma itambe ilikuwa lazima ichezwe kwenye redio za majayanti na hizo redio zilikuwa na mambo mengi ikiwemo kuulizwa ngoma umerekodi wapi na jibu ilikuwa ni lazima iwe umerokedi kwa majayanti… vinginevyo hakuna atakayechukua CD yako kuicheza redioni.
Lakini siku hizi studio kama zote - za kutosha. Kila mtaa una mshkaji ana kompyuta, spika fulani za kinyama, mic ya kurekodia na anajiita prodyuza. Iwe unaweza kuimba au huwezi hizo sio shida zake, ukimpoza hela ya luku anakuingiza booth unarekodi.
Na kuhusu ngoma utaichia wapi wala sio swali gumu hilo. Siku hizi kuachia ngoma redioni sio big deal kivile. Watu siku hizi ngoma wanaziachia mtandaoni tu - Audiomack, Youtube, Spotify, BoomPlay na sehemu kama hizo. Kisha ukifanya na chalenji ya Tiktok ngoma inaweza kutembea bila kutegemea.
Hata kwenye muvi na tamthilia ni vivyo hivyo. Zamani ilikuwa ni lazima kwanza uwe kwenye makundi ya michezo ya kuigiza kama Kaole, Mambo Hayo na kadhalika. Kisha makundi yanaandaa michezo na kwenda kuuza kuwapa haki za kuonyesha chaneli za TV katika runinga na kadhalika.
Baadaye kina Kanumba na Ray wakapata madili ya kutengeneza filamu. Ikawa ili utoboe inabidi uhakikishe unapata nafasi ya kuwa karibu na wasambazaji kama Steps ambao watakupa pesa ya kutengeneza filamu yako au watanunua haki za kuisambaza filamu. Ikaenda...ikaenda zikaja Maisha Magic na Azam. Nao mchezo ni uleule inabidi upambane sana kupata nafasi ya kazi yako kuonyeshwa kwenye chaneli hizo.
Lakini, siku hizi madogo hawasubiri kupewa kibali na Maisha Magic na Azam. Mtu anachukua kamera anatunga stori ya chap chap ambayo haina mambo mengi anachukua washkaji zake wanaopenda kuigiza, anaingia location, wanatengeneza tamthilia, anakwenda kuziweka zake Youtube. Na si haba kupitia Youtube wasanii wadogo wanapata pesa angalau hata za kununua Iphone za Makumbusho na maisha yanakwenda kuliko kuendelea kusubiri mpaka TV iseme kazi yako ni nzuri tutainunua.
Sasa licha ya kwamba teknolojia imebariki wasanii kwa namna kubwa kama ambavyo nimeeleza hapo juu, kwa upande mwingine imelaani sana. Hii ni kwa sababu sasa kila mtu ana uwezo wa kufanya sanaa zake bila kuulizwa kama ana uwezo wa kufanya kwa ubora. Matokeo yake, kumekuwa na mlundikano wa kazi ambazo kiwango chake ni kidogo sana kiasi kwamba sasa jukwaa hilo jipya huria lililotengenezwa na teknolojia linaanza kuonekana kama jalala la wasanii ambao hawana vipaji au uwezo wa kufanya sanaa kutupia kazi zao.
Na kama hali itaendelea hivyo, jukwaa hilo pia litajaa takataka za sanaa na matokeo yake mashabiki watalidharau na kulipa kisogo. Tusipoliwahi na kuhakikisha tunatafuta njia ya kuliboresha tutarudi tena kwenye kufanya sanaa kwa kutegemea ruhusa za majayanti.