Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Al Masry: Simba inabeba ubingwa

KOCHA Pict

Muktasari:

  • Boujelbene alifunguka kwamba Simba inaweza kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa ubingwa wa Afrika msimu huu kutokana na ubora wa kikosi hicho uwanjani ambacho ndio kitu muhimu na kwamba licha ya wao kuwafunga mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza lakini Wekundu walikuwa bora zaidi yao.

SIMBA kila mmoja yuko kwenye kilele cha furaha baada ya timu yao kufuzu kwa mara ya kwanza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini Kocha wa Al Masry, Anis Boujelbene ametamka kitu kizito.

Amesema kwamba kwa kiwango ambacho Simba imekionyesha kwenye mechi mbili alizokutana nayo kisha akiangalia mastaa wa timu hiyo ya Msimbazi na hata ratiba yao, suala la ubingwa wa Afrika washindwe wenyewe.

Boujelbene alifunguka kwamba Simba inaweza kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa ubingwa wa Afrika msimu huu kutokana na ubora wa kikosi hicho uwanjani ambacho ndio kitu muhimu na kwamba licha ya wao kuwafunga mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza lakini Wekundu walikuwa bora zaidi yao.

Kocha huyo aliongeza kuwa kitu kikubwa ambacho Simba inakifanya ni kwamba hata kama itapoteza ugenini lakini ina uhakika mkubwa wa kushinda nyumbani.

“Tumekubali tumepoteza tulijitahidi sana, unaona hali ya uwanja ilitupa shida, lakini wenzetu walionekana kuimudu, nawapongeza Simba kwa kufuzu,” alisema.

“Hakuna mwenye uhakika zinapokuja penalti, wenzetu walibahatika kuwa imara kuliko sisi, wanaweza kuchukua ubingwa ndio (Simba) ukiangalia tulipokutana nao kule nyumbani tuliona bao moja halitoshi, tukatafuta la pili lakini nalo halikutosha kuwapa ugumu.

“Hiki kilichotokea kinamaanisha kwamba Simba ili uwape shida labda uwafunge kuanzia mabao matatu au zaidi, wanapokuwa nyumbani wana nguvu kubwa ya kutengeneza matokeo wanayoyataka.”


MUKWALA, MPANZU

Akizungumzia mastaa ambao wamewapa shida, Boujelbene alisema baada ya mchezo wa kwanza walijipanga kuhakikisha wanamdhibiti winga Elie Mpanzu ambaye aliwapa wakati mgumu lakini hawakufanikiwa zaidi ya kuwaumiza kwa kufunga bao la kwanza huku akishtushwa na sapraizi ya mshambuliaji Steven Mukwala aliyefunga bao la pili wakiwa wamejiandaa kumkabili Leonel Ateba.

“Kule nyumbani yule kiungo wa pembeni jezi namba 34 (Mpanzu) alijituma sana tukasema tunatakiwa kumchunga hapa ugenini lakini hatukufanikiwa, ana nishati sana na nguvu za miguu.

“Wana mshambuliaji mzuri pia, unajua tulitegemea kumkabili Ateba (Leonel), mimi binafsi namfahamu lakini tulishangaa kumuona yule aliyefunga bao la pili (Mukwala) hata kwenye mechi nyingi tulizozifuatilia hatukumuona sana lakini bado na yeye akafanya vizuri.

“Nadhani wana timu nzuri ambayo inaweza kutenegeneza matokeo ndani ya dakika 90 lakini pia hata ukifika nao kwenye penalti wanaweza kufanya vizuri,” alisema.

Kocha huyo akaongeza kuwa Simba itakwenda kukutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini iliyoing’oa Zamalek ya Misri kwa bao 1-0 ambapo akasema bado sio mpinzani mgumu sana kwa Wekundu hao.

“Nilidhani wangekutana na Zamalek, hata sisi wakati tunaiona ratiba tulidhani tuna nafasi kubwa ya kukutana na Zamalek lakini nao wametolewa, kama wakipanga hesabu zao sawasawa Simba inaweza kufika fainali,” alisema.


RATIBA YA FAINALI INAWABEBA

Kocha huyo alisema hata ratiba ya fainali kama Simba ikifanikiwa kufika huko atakayekutana naye anatakiwa kujipanga kwa kuwa watamalizia nyumbani kwa Wekundu hao.

“Hakuna timu imeifunga Simba hapa kwao, sijui hawa watakaokutana nao nusu fainali lakini ili upate nafasi kubwa ya kuwaondoa lazima ujue utafanyaje vizuri hapa Tanzania na ukiangalia ratiba ya fainali kama wakifuzu, wataanzia ugenini na kumalizia hapa kwao, hii ni changamoto nyingine,” alihitimisha.

Simba msimu huu kwenye mechi tano za Kombe la Shirikisho chini ya kocha Fadlu Davids ikiwa nyumbani, imeshinda zote ikiwemo moja ya hatua ya mtoano dhidi ya Al Ahli Tripoli iliposhinda 3-1. Tatu za hatua ya makundi ikizifunga Bravos, CS Constantine na CS Sfaxien kisha moja ya hatua ya robo fainali dhidi ya Al Masry. Katika mechi hizo tano, imefunga mabao kumi na kuruhusu mawili tu.