P Diddy anavyopitishwa kwenye ‘tanuru la moto’
Muktasari:
- Combs, mwenye umri wa miaka 55 na mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika historia ya muziki huo, anasubiri huku akiwa mahabusu baada ya kukutwa na makosa ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono dhidi ya wake zake wa zamani wawili na usafirishaji watu kuvuka mipaka ya majimbo kwa ajili ya ukahaba.
NEW YORK, MAREKANI: WAKATI mwanamuziki maarufu wa hip hop nchini Marekani, Sean ‘Diddy’ Combs akisubiri hukumu baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya usafirishaji binadamu kwa ajili ya ukahaba na kujihusisha na biashara hiyo, ile himaya yake ya biashara ambayo zamani ilisifika imeporomoka kwa kasi.
Combs, mwenye umri wa miaka 55 na mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika historia ya muziki huo, anasubiri huku akiwa mahabusu baada ya kukutwa na makosa ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono dhidi ya wake zake wa zamani wawili na usafirishaji watu kuvuka mipaka ya majimbo kwa ajili ya ukahaba.
Tayari Mahakama ya Shirikisho ya New York imempata na hatia katika makosa hayo, ambapo hukumu yake inatarajiwa kutolewa miezi michache ijayo.
BIASHARA ZAKE HOI
Biashara zake zimeporomoka kwa kasi, ikielezwa kwamba hata kabla ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka, biashara kubwa zilikuwa hoi.
Coms alijiuzulu na baadaye kuachana kabisa na umiliki wa kituo cha televisheni cha Revolt TV alichokianzisha 2013 ambacho kilikuwa kikirusha vipindi vinavyohusu utamaduni wa hip-hop, muziki wa R&B, haki za kijamii na makala.
Pia, inadaiwa amepoteza mkataba wa kipindi cha runinga ya Hulu na chapa yake maarufu ya mavazi, Sean John kutoweka kabisa katika maduka maarufu ya nguo ya Macy’s.
Mwaka 2016 Jiji la New York lilimnyang’anya fursa kubwa za biashara ya muziki kupitia Kampuni ya Peloton ambayo iliondoa muziki wake, huku Chuo Kikuu cha Howard kikiifuta shahada yake ya heshima, na shule yake ya msingi ya charter huko Harlem iliondoa uhusiano naye.
Mwaka jana pia alifikia makubaliano ya kisheria na kampuni ya Diageo kuachana na umiliki wa chapa zake za pombe zenye mafanikio — Ciroc na DeLeon. Hata hivyo, haki za muziki wake bado hazijaguswa. Hadi mwaka 2022, Combs alikuwa na utajiri wa Dola 900 bilioni, akiwa mmoja wa wasanii wenye mkwanja wa maana zaidi duniani.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali utajiri wake mwaka huu unakadiriwa kuwa takriban Dola 400 milioni ikiwa ni kushuka kwa kiasi kikubwa kutoka kilele cha mafanikio yake kifedha miaka michache iliyopita. Mwanzoni mwa kesi yake mwaka jana, thamani ya mali zake ilikuwa inakadiriwa kufikia takriban Dola 600 milioni, kwa mujibu wa Merca2.
Hata hivyo, hali yake ya kifedha ilikuwa tofauti miaka mitano iliyopita. Mwaka 2020 inadaiwa thamani ya mali ya awali ya utajiri wake mkubwa ulitokana na shughuli zilizokuwa na mafanikio katika muziki na fasheni za mavazi pamoja na ushirikiano wake na kampuni kubwa ya vinywaji ya Diageo, hususan katika kutangaza chapa ya pombe ya Ciroc.
MUZIKI WAKE JE?
Bad Boy Records, studio ya Combs iliyowahi kutikisa miaka ya 1990 kupitia wasanii kama Notorious B.I.G, Faith Evans, Mase na 112, iliendelea kuwa imara hadi kukamatwa kwake. Mwaka 2023, Combs alitoa albamu baada ya karibu miongo miwili, The Love Album: Off the Grid, na Janelle Monae pia alitoa albamu iliyosifiwa, The Age of Pleasure, kupitia Bad Boy. Albamu zote mbili ziliteuliwa kushiriki tuzo za Grammy.
Kabla ya kutoa The Love Album, Combs alitangaza kurudisha haki ya utunzi wa nyimbo kwa baadhi ya wasanii wa zamani wa Bad Boy, baada ya kukosolewa kwa miaka kuhusu mikataba yao.
Lakini, lililo dhahiri ni kuwa Bad Boy Records bado inafanya kazi, lakini imeyumba kutokana na sakata hilo la kisheria na hadi sasa hakuna tangazo la mradi mpya mkubwa. Wiki chache zilizopita, EP ya kushangaza ‘Never Stop’ kutoka kwa mwanawe, King Combs na Ye (zamani Kanye West) ilitolewa kupitia Goodfellas Entertainment.
MALI, UTAJIRI WAKE HATARINI?
Licha ya kwamba anasubiri huku, Combs ameshtakiwa na watu wengi wanaodai kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono. Tayari amelipa Dola 20 milioni kwa mpenzi wake wa zamani Cassie kama fidia ya nje ya mahakama. Mashtaka mengine bado yanaendelea na haijajulikana ni mangapi yatamuumiza au gharama ya kujitetea kwake itakuwa kiasi gani.
Waendesha mashtaka wa serikali pia wameiambia Mahakama kwamba iwapo Combs atapatikana na hatia, serikali itataka kuchukua mali au mali isiyohamishika iliyotumika kufanikisha uhalifu. Orodha kamili ya mali hizo haijatajwa hadi baada ya hukumu.
MUZIKI WAKE MITANDAONI
Licha ya mgogoro wa kisheria, muziki ya Combs bado unapatikana kwenye majukwaa makubwa ya mitandao kama Spotify, Apple Music na Amazon. Hakuna jukwaa lililotangaza litafanya mabadiliko yoyote iwapo atapatikana na hatia. Cha kushangaza, kati ya Aprili na Mei 2025, kusikilizwa kwa muziki wake Marekani kuliongezeka kwa takribani asilimia 20 — ongezeko kubwa zaidi mwaka huu. Hata hivyo, mwezi Juni usikilizwaji ulishuka kwa asilimia tano hadi 10.
DIDDY NA BIASHARA NYINGINE
Chapa ya mavazi ya Sean John iliyoanzishwa 1998, imekuwa kimya na haipo tena katika maduka makubwa kama Macy’s na hakuna dalili za kurudishwa sokoni. Mwaka 2023, Combs alizindua Empower Global, soko la mtandaoni lililolenga kuinua biashara za Wamarekani weusi na kuimarisha mzunguko wa fedha miongoni mwao. Mradi huo ulizinduliwa na chapa 70 na mpango wa kuongeza zaidi kila mwezi. Lakini, mwishoni mwa 2023, baadhi ya chapa za washirikika wake kibiashara walijiondoa wakielezea kutoridhishwa na mwenendo wa biashara na tuhuma zinazomkabilia.
Mbaya zaidi ni kwamba, mwaka huu pekee mwanamuziki huyo amekimbiwa na washirika chini ya 10 wa kibiashara, huku biashara zake ndogo na za kati zaidi ya 30 akilazimika kuzifunga kutokana na kadhia za kisheria anazopitia. Lakini, hata baada ya changamoto hizo binafsi, Combs anabaki kuwa miongoni mwa watu wenye utajiri mkubwa katika tasnia ya muziki wa hip-hop, ingawa hajawahi kufikia hadhi ya kuwa bilionea - tofauti na uvumi na tetesi zilizoenea miaka ya nyuma.