Prime
Kocha Barker aachiwa wawili kuamua Simba
UONGOZI wa Simba kwa kuona mgumu wa kuamua kipa yupi abaki ndani ya kikosi cha Simba msimu ujao kati ya Kassali Djibril na Mousa Camara umeliacha jukumu hilo kwa benchi la ufundi chini ya kocha Steve Barker kuamua hatma ya makipa hao wawili.
Camara na Kassali mikataba yao inafikia tamati mwisho wa msimu, hivyo viongozi wa Simba watalazimika kuamua hatma ya kipa moja abaki ili kukidhi kanuni ya usajili inayotaka timu kusajili kipa mmoja tu wa kigeni.
Camara kabla ya kuumia aliingoza Simba kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita wakati Kassari amekuwa na mafanikio tangu alipotua Simba wakati wa dirisha dogo akiwa na rekodi ya cleansheet 12, akiwa chachu ya miamba hiyo kuisaka ndoto ya ubingwa msimu huu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori akizungumza na Mwanaspoti, alisema makipa hao wawili mikataba yao itafikia tamati mwisho wa msimu huu na uongozi haujafanya mazungumzo na yeyote kwa sasa akili ipo katika kumaliza mechi tano za mwisho wa msimu.
“Camara mkataba wake unafikia ukingoni mwisho wa msimu huu, sasa uamuzi haya tunaliachia benchi la ufundi litaamua kama litasema tumpe mkataba mpya Camara tutafanya hivyo, kama tutaendelea na Kassali (Djibril) tutawasikia au tutafanya vinginevyo tutajua maana kanuni zetu zinataka timu moja kuwa na kipa mmoja wa kigeni.” alisema Magori.
Magori akizungumzia hatma ya Camara alisema kipa huyo baada ya kuondolewa kwenye mfumo wa usajili bado Simba haijafanya uamuzi na benchi la ufundi la Simba limeachiwa kutoa uamuzi wa kipi kitafanyika.
“Camara ni kweli tulimuondoa kwenye usajili kwa sababu alikuwa hawezi kupona mpaka Aprili au Mei mwaka huu, tulikuwa katikati ya mashindano makubwa unatakiwa kucheza, lakini kibaya zaidi kipa wetu namba mbili Yakubu (Suleiman) naye akaumia.
“Hatuwezi kusajili makipa wawili wa kigeni kanuni zinatuzuia, ikabidi tumuambie (Camara) wewe tutakuondoa kwenye usajili, ili tusajili kipa wa kucheza kwa sababu hatuwezi kusubiri na kubaki na kipa mmoja Abel mpaka yeye apone na awe tayari kuanza kucheza hapo tena msimu utakuwa umekwisha.
Katika hatua nyingine Magori alisema hatma ya mshambuliaji Jonathan Sowah itajulikana mwisho wa msimu huu.
Magori ameeleza kwa mara ya kwanza juu ya sakata hilo akisema kila kosa ndani ya klabu hiyo lina hatua zake za kuchukuliwa katika kulitolea adhabu.
Magori alisema Sowah alikutwa na hatia na kupewa adhabu kwa mujibu wa sheria za klabu ambapo baada ya kukaidi kwenda timu ya vijana, uongozi wa klabu hiyo hauwezi kuingilia uamuzi ya kamati hiyo ambapo hatua hiyo itapelekwa kwenye kanuni za kinidhamu huku akisema uamuzi wake yatatolewa mwisho wa msimu.
“Suala la Sowah lilikuwa la kinidhamnu kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za maadili za klabu, kuna makosa akifanya mchezaji, kuna makosa yanaamuliwa moja kwa moja kwakuwa yana adhabu zake, kama vile umechelewa au umefanyaje, kuna faini yake, unaweza ukakatwa mishahara,” alisema Magori.
“Hiyo mara nyingi sekretarieti hasa mtendaji mkuu wa klabu akipata taarifa kutoka benchi la ufundi kwamba huyu amechelewa hivi moja kwa moja kuna onyo au atakatwa mshahara, sasa hili alilofanya Sowah lilikuwa ni kubwa, likapelekwa kwenye vyombo ambavyo kidogo ni vya uamuzi ambavyo vinajitegemea ambavyo wewe mwenyewe huwezi kujiamulia kwa hiyo tukaenda kamati ya nidhamu.
“Kikafanyika kikao na kamati ikatoa uamuzi wake na adhabu ikawekwa na mwisho wa siku uamuzi yakafanyika, kwa hiyo ni kwamba alikuwa aende huko(timu ya vijana) akagoma,ukigoma kwenda huko basi, tunaangalia kwenye kanuni za nidhamu kuna adhabu gani, basi tunafanya, kuhusu hatma yake, tutajua dirisha kubwa,” alimaliza Magori.