Seseme wa Sikinde OG afariki dunia, kuzikwa leo

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, msemaji wa Bendi ya Sikinde OG, Mwalimu Libingai amesema mwili wa marehemu Seseme utatolewa katika Hospitali ya Amana saa nne asubuhi na kupelekwa kwenye Msikiti wa Mwinyimkuu Magomeni kwa ajili ya kuandaliwa kwa mazishi.
Mpiga gitaa mkongwe nchini, Omar Seseme aliyefariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi ya moyo anazikwa leo katika makaburi ya Mzimuni, Mwinyimkuu Magomeni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, msemaji wa Bendi ya Sikinde OG, Mwalimu Libingai amesema mwili wa marehemu Seseme utatolewa katika Hospitali ya Amana saa nne asubuhi na kupelekwa kwenye Msikiti wa Mwinyimkuu Magomeni kwa ajili ya kuandaliwa kwa mazishi.
"Maziko ya Omar Seseme ni leo saa 10 jioni, ambapo mwili wake utaswaliwa kwenye Msikiti wa Mwinyimkuu Magomeni. Baada ya hapo atazikwa katika Makaburi ya Mzimuni, Mwinyimkuu Magomeni," amesema Libingai.

Libingai akizungumza na Mwanaspoti alivyopata taarifa ya Seseme kufariki dunia, amesema uongozi wa Sikinde OG ulizipata jana saa 10 jioni baada ya kuvunjwa mlango wa nyumba aliyokuwa akiishi mwanamuziki huyo saa 8 mchana na majirani zake.
"Tulipata taarifa saa 8 mchana na vijana anaoishi nao jirani walisema Babu (Seseme) toka asubuhi hajafungua mlango wake wa chumba ndipo tulipowaambia wavunje. Baada ya kuvunjwa Seseme akakutwa amefariki," amesema Libingai
"Lakini hadi jana jioni Seseme aliwasiliana na uongozi wa Sikinde OG akaomba ahamishwe sehemu aliyokuwà anaishi na kutaka apelekwe maeneo ya Amana karibu na kliniki anapofanyia matibabu."
Libingai amesema walishindwa kutoa taarifa mapema za msiba kwa sababu kuna mambo walikuwa wanashughulikia ikiwemo kuwatafuta ndugu zake bila mafanikio, hadi walipoupeleka mwili wa marehemu katika Hospital ya Amana kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Amesema Seseme alianza kuugua tangu mwaka 2022 na alikuwa akiwaambia kwamba mwili wake ulikuwa unachoka, na hata alipokuwa stejini alikuwa akifanya kazi akiwa amekaa kwenye kiti.
Libingai amesema ilipofika Januari 2024 uongozi wa Sikinde OG ulimpeleka Hospital ya Amana kwa ajili ya vipimo na aligundulika kuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo.
"Seseme baada ya uongozi wa Sikinde kumpeleka hospitali tukamfungulia kliniki akawa anahudhuria kila baada ya wiki, na tulimkatia bima na hata nyumba aliyofariki (dunia) ni ya Sikinde OG," amesema.

Enzi za uhai wake Seseme alikuwa anaitumikia Sikinde OG aliyojiunga nayo mwaka 2022 akitokea Super Kamanyola ya Mwanza. Pia aliwahi kuzitumikia bendi kadhaa akiwemo TamTam, TOT na nyinginezo.