Prime
Sura tano tofauti za Hamisa Mobetto

Muktasari:
- Kutokana na nguvu yake ushawishi, tunakuleta sura tano tofauti za Hamisa ambazo kwa ujumla ndizo zinakamilisha chapa yake ambayo ndio inampa maisha kwa sehemu kubwa na kufanya tuendelee kumfuatilia na kumshabikia.
Jina la Hamisa Mobetto si maarufu Tanzania pekee bali Afrika Mashariki yote kutokana na kazi zake na mtindo wake wa maisha ambao unatolewa macho na vijana wengi na hata kuteka mazungumzo mtandaoni kila mara.
Kutokana na nguvu yake ushawishi, tunakuleta sura tano tofauti za Hamisa ambazo kwa ujumla ndizo zinakamilisha chapa yake ambayo ndio inampa maisha kwa sehemu kubwa na kufanya tuendelee kumfuatilia na kumshabikia.

1. Urembo na Mitindo
Akiwa mwanafunzi wa sekondari ya Tandika, Dar es Salaam ndipo Hamisa alishinda taji la Miss XXL After School Bash 2010, huku akimtaja Lisa Jensen, Miss Tanzania namba tatu 2006 kama role model wake maana alikuwa muigizaji na mwanamitindo.
Baada ya hapo Hamisa aliyezaliwa Desemba 10, 1994 huko Mwanza, alishiriki mashindano mbalimbali ya urembo akiibuka mshindi wa pili Miss Dar Indian Ocean 2011, nusu fainali ya Miss Tanzania 2011 na 10 bora ya Miss University Africa 2012.
Hatua hiyo ndio ilifungua milango mingi kwa Hamisa hata akipata fursa ya kuigiza filamu na kutokea katika video za wasanii kama Barnaba, Quick Rocka, Diamond Platnumz na Alikiba, mshindi wa MTV EMAs 2016. Na katika katika urembo na mitindo Hamisa amefanya vizuri zaidi na kushinda tuzo za ndani na kimataifa kama Abryanz Style Fashion (Uganda), Starqt Awards (Afrika Kusini), Scream Awards (Nigeria), Young C.E.O Round Table (Tanzania), EAEA (Kenya) n.k.

2. Muziki na Filamu
Hamisa aliamua kujaribu bahati yake katika muziki akianza na wimbo wake, Madam Hero (2018), kisha EP, Yours Truly (2022) yenye nyimbo sita lakini baada ya hapo aliamua kukaa kimya upande huo sasa ikiwa ni zaidi ya miaka miwili.
Moja ya nyimbo zake zilizokubalika na wengi ni Ex Wangu Remix (2021) akimshirikisha Seneta Kilaka, huu video yake imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 11.5, namba ambazo wanamuziki wengi maarufu hawajawahi kuzifikia.

Pia ametokea katika video za wasanii kama Barnaba, Magubegube (2012), Diamond, Mawazo (2012), Quick Rocka, My Baby (2013), Diamond, Salome (2016) na Alikiba, Dodo (2020), huku filamu yake ya mwisho kucheza ikiwa ni Zero Player (2017).
Ikumbukwe Hamisa ni video vixen na muigizaji mwingine aliyejaribu bahati yake kwenye Bongofleva kama ilivyo kwa kina Gigy Money, Amber Lulu, Lyyn, Nai, Caren Simba, Snura, Shilole na Rose Ndauka ambaye ametoa EP, Majibu Rahisi (2024).

3. Soka na Ushabiki
Kwa miaka Hamisa amejipambanua kama shabiki mkubwa soka, awali alikuwa shabiki Simba SC, katika fainali ya Simba Super Cup 2021, shindano dogo la kirafiki liloshirikisha na timu nyingine kama Al Hilal na TP Mazembe, ndiye aliyeleta kombe uwanjani.
Hata hivyo, Agosti 4, 2024 katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, Hamisa alihamia Yanga SC kama shabiki akimfuata mume wake, Aziz Ki ambaye alimkaribisha kwa kumvalisha jezi ya mabingwa hao mara 30 wa Ligi Kuu Bara.
Na kwa sasa Hamisa anatambulika kama shabiki wa Yanga na kubwa zaidi kama shabiki wa Aziz Ki huku akijitolea kumuunga mkono katika kazi yake hiyo, mathalani Januari 2025 alimzawadia viatu pea tatu alivyovinunua Afrika Kusini katika duka la Puma.
Utakumbuka katika hafla ya tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyofanyika Agosti 2024 ndipo waliweka wazi kuwa wao ni wapenzi na kuahidi kwenda pamoja Dubai kutalii baada ya Aziz Ki kushinda tuzo ya Mchezaji Bora Ligi (MVP) 2023/24.

4. Mapenzi na Ndoa
Kwa sasa Hamisa ameolewa na mchezaji wa Yanga SC, Aziz Ki ambaye tetesi za uhusiano wao zilianza Mei 2024 baada ya kuonekana wakitoka wote Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) pamoja na wachezaji wengine wa timu hiyo.
Hata hivyo, ndoa hii ni mwendelezo wa Hamisa kuzidi kugonga vichwa vya habari upande wa mahusiano yake na hasa kutokana na uzito wa watu ambao amekuwa akihusishwa nao mara kwa mara kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Mwaka 2014 alikuwa na Mkurugenzi Mtendaji wa E FM Radio na TV E, Majizzo na kujaliwa mtoto wa kike, Fantasy (2015), kisha kuanzia 2016 akawa na Diamond Platnumz, Mkurugenzi wa WCB Wasafi na Wasafi Media na kupata mtoto wa kiume, Dylan (2017).
Baada ya hapo, mwaka 20211 Hamisa alihusishwa na rapa wa Marekani, Rick Ross aliyetoka kimuziki na wimbo wake, Hustlin (2006), kisha 2023 akazama penzini na mfanyabiashara kutokea Togo, Kevin Sowax aliyemzawadia gari jipya aina ya Range Rover.

5. Mitandao ya Kijamii
Hadi sasa Hamisa ndiye staa wa kike Tanzania mwenye wafuasi (followers) wengi Instagram akiwa nao zaidi milioni 12.1 tangu ajiunge na mtandao huo wa kijamii hapo Desemba 2012 na ukurasa wake kuidhinishwa (verified) October 2018.
Mastaa Bongo wanaomfutia Hamisa ni Wema Sepetu, Miss Tanzania 2006 mwenye wafuasi milioni 11.8, kisha Shilole, mjasiriamali na mwanamuziki aliyetoka na kibao chake, Nakomaa na Jiji (2013), huyu ana wafuasi milioni 10.9.
Instagram ndio sehemu inayompatia Hamisa fedha nyingi zaidi pengine kuliko kazi zake zote, ni kupitia dili za ubalozi anazosaini kila mara na matangazo ya kampuni na taasisi mbalimbali anazofanya nazo kazi.
Na kwa Afrika Mashariki, Hamisa anashika nafasi ya pili kwa kuwa na wafuasi wengi Instagram baada ya Zari The Boss Lady kutokea Uganda mwenye milioni 12.4, huku duniani kwa ujumla, msanii wa Marekani Selena Gomez anaongoza akiwa na wafuasi milioni 421.