Ukweli wafichuka maisha ya Diddy gerezani
Muktasari:
- Hivi sasa Diddy anatumikia kifungo cha miaka minne na miezi miwili katika Gereza la Fort Dix kutokana na makosa ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba alichohukumiwa Oktoba 3, mwaka huu.
DIDDY hawezi kuacha kuwakumbatia wafungwa wenzake na kupiga picha nao, angalau ndivyo picha na video mpya zinavyoonekana, isipokuwa ukweli ni picha hizo ni za akili bandia (AI).
Hivi sasa Diddy anatumikia kifungo cha miaka minne na miezi miwili katika Gereza la Fort Dix kutokana na makosa ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba alichohukumiwa Oktoba 3, mwaka huu.
Tangu alipofungwa mitandao mbalimbali imekuwa ikisambaza picha zinazomuonyesha nyota huyo wa muziki wa r&b akishiriki matukio tofauti akiwa gerezani, ikiwa ni siku chache tangu taswira halisi ya jinsi alivyo gerezani ilipotoka.
Baadhi ya picha zilizosambaa hivi sasa zinaonyesha 'selfie' ya mfungwa mmoja akiwa mbele akipiga picha, huku Diddy akitabasamu na kumkumbatia mfungwa mwingine, lakini kimsingi haina ukweli wowote.
Ingawa mtandao wa TMZ ulipata picha halisi kadhaa za Diddy akiwa gerezani huko Fort Dix, hii ya saa siyo mojawapo na wala zile nyingine ambazo huenda watu wengi wanaziona kwenye mitandao ya kijamii. Huu ni ujanja wa mtu kutumia teknolojia ya akili bandia kufanya yake.
Vilevile kuna video ya AI inayodai kumuonyesha Diddy akiwa amevaa nguo za mazoezi gerezani akiwa na wafungwa wengine wawili uwanjani.
Kwa mujibu wa TMZ, hiyo pia ni taswira isiyo halisi kwani haingekuwa na maana kwa wafungwa kupiga 'selfie' jambo ambalo lingemrahisishia mkuu wa gereza kugundua ni nani anayepiga picha na Diddy.
Mtandao huo wa burudani na maisha ya mastaa umeeleza kwamba kwa kuwa dunia imeona picha halisi za kweli za Diddy akiwa na ndevu za kijivu kutokana na video na picha halisi za mwezi uliopita baadhi ya watu wameanza kuingiza taswira hizo kwenye AI na kutengeneza picha wazitakazo na kuzisambaza.
TMZ inadai picha hizo feki zinataka kuionyesha dunia kwamba Diddy wa gerezani yuko karibu kuwashinda mastaa waliowahi kufungwa kama Mr Rogers, Tupac na MLK Jr.
Akizungumza na TMZ, msemaji wa Diddy, Juda Engelmayer alizungumzia juu ya picha zinazosambaa ovyo za staa huyo akisema.
“Picha hizi siyo za kweli. Ni picha zilizotengenezwa na AI. Sean (Diddy) siku zote amekuwa akitenda mambo yake kwa unyenyekevu na heshima, lakini inatia wasiwasi kuona kwa kiwango gani picha bandia au zinazotengenezwa na AI zinasukumwa kwenye mazungumzo wakati yeye yuko mikononi mwa vyombo vya dola.
Aliongeza kuwa, "Hakuna chochote katika picha hizi zilizochezewa kinachoakisi uhalisia.”
Engelmayer anasema hata tukio linaloonyeshwa kupitia picha hizo likionyesha Diddy akipigwa kibao na mfungwa mwenzake gerezani halina ukweli wowote na ni tukio linalosambazwa ili kumchafua nyota huyo wa muziki.
Pia kuna picha inayomuonyesha Diddy akigawa chakula kwa wafungwa wenzake gerezani ambayo nayo siyo halisi.
ATHARI HASI ZA AI
Teknolojia ya AI kwa sasa inaweza kutengeneza picha au video zinazomfanya mtu aonekane akifanya kitu ambacho hakijawahi kutokea na watu wengi wanapotoshwa kirahisi.
Hata hivyo, kwa mtu yeyote kubaini uhalisia wa picha au video inamlazimu kujipa muda wa kufanya utafiti kupitia teknolojia hiyo kwani inaweza kumpa jibu, ingawa siyo rahisi kulifanya hilo kwa haraka.
Licha ya manufaa makubwa katika matumizi akili bandia, watumiaji wanaaswa kuwa makini, kwani athari hasi zinaweza kusababisha mambo mbalimbali katika jamii na kuibua changamoto za kisheria.
DIDDY MWENYEWE
Diddy (Sean Combs) ni mfanyabiashara, mwanamuziki maarufu na mwigizaji nchini Marekani wa kizazi cha kina Tupac Shakur, Dk Dre, Ice Cube na Christopher Wallace (BIG).
Nyota huyo alivuna utajiri mkubwa kutokana na kazi ya muziki na uigizaji katika miaka ya 1990 hadi 2000 na alijiingiza katika biashara za chapa mbalimbali zikiwamo za mavazi na mitindo na katika miaka ya karibuni amekuwa akikabiliwa na kesi na tuhuma mbalimbali.