Zaylissa: Niliolewa kwa sherehe, natoka kwa sherehe

Muktasari:
- Zaylissa amesema ataandaa sherehe hiyo atakayoipa jina la 'Usiku wa Talaka' kwani hadi anaipata talaka hiyo, haikuwa kazi rahisi na ametumia nguvu za ziada.
MOJA ya habari zinazotreni mitandaoni na vyombo vya habari ni iliyokuwa ndoa ya Haji Manara na Zaylissa ambayo imefikia mwisho na inaelezwa mwanadada huyo amepanga kushusha bonge la pati kusherehekea talaka yake.
Zaylissa amesema ataandaa sherehe hiyo atakayoipa jina la 'Usiku wa Talaka' kwani hadi anaipata talaka hiyo, haikuwa kazi rahisi na ametumia nguvu za ziada.
Akizungumza na Mwanaspoti, mwigizaji huyo wa Bongo Movie amekiri mpango huo ni kweli kwani aliolewa kwa sherehe na na atatoka kwa sherehe.
"Eeeh! sio shida nzangu kufanya sherehe, sasa kwa nini niolewe na sherehe na nitoke bila sherehe? Mimi mtoto wa Kitanga bwana, sherehe kwangu kama maji ya kunywa tu na isitoshe nimeitaka mwenyewe talaka alaah! We subiria muda ukifika nitakwambia nipo kwenye maandalizi na nitawaalika watu wengi wacheze, kunywa na kula kwa kadiri watavyojisikia, pia wakiwa wamevalia sare ya vijora pambe tu," amesema Zaylissa.
Zaylissa aliongeza, “Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kurejesha furaha yangu na kufungua ukurasa mpya wa maisha yangu, kwani siku chache zilizopita nilikuwa siko poa."
Amesema ndoa yake hiyo imemfunza mambo mengi na hata kama ikitokea ndoa nyingine, haitaweza kumteteresha kwani tayari ameshapita kwenye mafunzo.
“Sipendi kuzungumzia sana habari za ndoa hii kuvunjika, ila kifupi nilikuwa katika wakati mgumu na leo hii nimejifunza mengi katika maisha ya ndoa," amesema.
Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya aina hiyo ya wanawake wanaotoka kwenye mahusiano na hasa ndoa 'talaka' kufanya sherehe kufurahia talaka hiyo.
Pia wapo wengine walioondoka kwa waume zao kabla hawajapewa talaka ila wanapokwenda kuichukua tu, huwa wanafanya sherehe. wenyewe huziita sherehe maalumu za kusherehekea kuachwa na kupewa talaka.
Mbali na hiyo, wapo wanawake wanaoongezewa mke kwa waume zao huwa wanafanya sherehe ya kumpokea mke mwenza. Mambo haya sio mageni kwa sasa na yanatrendi sana mitandaoni.