Dili iliyokufa - 8
ILIPOISHIA
Zainab akatabasamu.
“Nitafurahi sana”
“Nataka mke wangu upate afya nzuri uweze kumlea mtoto wetu aliye tumboni mwako”
“Usijisahau mume wangu. Ukumbuke kuwa umeacha mke wako akiwa na kitoto chako tumboni”
“Nitakukumbuka mke wangu. Mimi naenda Sauzi kwa ajili yenu”
“Sawa mume wangu”
“Ondoa wasiwasi. Niombee nifike salama na nipate kazi.
SASA ENDELEA...
“Nitakuwa nakutumia pesa za matumizi kila mwezi. Ukija kujifungua utamwambia mwanangu baba yako amekwenda ughaibuni kutafuta maisha, akirudi atakuletea gari na kukujengea nyumba…”
Zainab akacheka.
“Sawa mume wangu, nitamwambia na mwenyewe anasikia humo tumboni.”
Siku ya pili yake Wakwetu alimuachia Zainab kiasi kidogo cha pesa za matumizi. Akaenda Msumbiji ambako alidandia malori kutoka nchi moja hadi nyingine hadi akafika Zimbabwe.
Zimbabwe alikaa kwa siku tatu. Akafanikiwa kuvuka mpaka na kuingia Afrika Kusini akiwa na vijana wengine ambao walikuwa wanaenda kutafuta maisha katika nchi hiyo iliyoko katika pembe ya Afrika.
Vijana wa Kitanzania aliokutana nao katika jiji la Cape Town ndio waliomuhifadhi kwa siku kadhaa.
Alifanikiwa kupata kazi katika duka moja la Muhindi. Siku tatu baada ya kuajiriwa, majambazi walivamia duka hilo wakamuua mmiliki wake na kupora mamilioni ya pesa.
Mkosi ulikuwa bado unamuandama Wakwetu. Alikamatwa yeye na kushitakiwa kwa kosa la kushirikiana na majambazi, kumuua mmiliki wa duka na kupora mamilioni ya pesa.
Miongoni mwa watu walioitwa na upande wa mashitaka kutoa ushahidi dhidi ya Wakwetu alikuwa binti wa tajiri aliyeuawa ambaye alisema alikuwa katika duka hilo wakati majambazi sita walipoingia katika duka hilo.
Akasema majambazi hao walizungumza na Wakwetu na alimsikia Wakwetu akiwambia kuwa ni lazima kwanza wamuue mmiliki wa duka hilo ndipo wangeweza kupora pesa zilizokuwepo.
Msichana huyo aliendelea kuiambia mahakama kuwa baada ya hapo alisikia milio ya risasi na watu waliokuwa ndani ya duka hilo wakaamriwa walale chini.
“Baba yangu alikuwa akipiga simu polisi akapigwa risasi ya kichwa na kufa pale pale. Mimi nilijificha chini ya meza kusalimisha maisha yangu,” msichana huyo alisema.
Alipoulizwa na mwendesha mashitaka ni nani aliyempiga risasi baba yake, akajibu kuwa ni Wakwetu.
Ushahidi huo ambao ulikuwa wa kupangwa ndio uliomponza Wakwetu. Akapatikana na hatia.
Siku ya hukumu Wakwetu hakuamini masikio yake jaji alipomwambia:
“Umepatikana na hatia ya kushiriki katika kosa la ujambazi, kupora pesa katika duka uliloajiriwa na kumuua mwajiri wako kwa kumpiga risasi ya kichwa. Ninakuhukumu kunyongwa kwa kitanzi hadi mauti yakukute!”
Wakwetu pamoja na marafiki zake waliokuwepo mahakamani waliangua vilio. Wakwetu alilia kwa uchungu kwa kuona alikuwa anakwenda kunyongwa bila kosa.
Marafiki zake walilia kwa vile waligundua kuwa Wakwetu alionewa. Alikamatwa kwa kuonewa, alishitakiwa kwa kuonewa na alihukumiwa kwa kuonewa. Walikuwa wameifuatilia kesi yake kwa karibu miezi sita wakiamini kuwa mwisho wa siku Wakwetu angeachiwa huru, lakini haikuwa hivyo.
Wakwetu alihukumiwa kunyongwa!
Kwa sababu ya kutaharuki Wakwetu hakuweza hata kuagana na rafiki zake. Alitolewa nje ya mahakama haraka haraka na kupakiwa kwenye karandinga la magereza.
Wakati anapanda karandinga hilo alimuona rafiki yake wa karibu akimuaga kwa kumpungia mkono wa buriani.
Wakwetu naye aliinua mkono wake uliokuwa ukitetemeka.
“Mtanisalimia mke wangu na mwanangu. Mtamwambia yaliyonikuta…” akamwambia.
Kabla ya kumaliza sentensi yake alisukumwa na askari wa magereza akaingizwa ndani ya lori hilo.
Safari ya kuelekea katika gereza la Hill Fort ikaanza.
Wakwetu aliacha kulia akawa anawaza. Alimkumbuka sana mke wake na mwanawe atakayezaliwa. Alijiambia mwanawe atakuwa yatima asiye na baba na mkewe atakuwa mjane asiye na matumaini ya maisha.
Mawazo ya Wakwetu yalikwenda mbali zaidi. Aliunda picha iliyomuonesha mwanawe akiwa ombaomba katika mitaa ya jiji la Dar.
Akatikisa kichwa kusikitika.
Alifikishwa katika gereza hilo na kupelekwa katika sehemu ya wafungwa waliohukumiwa kunyongwa. Aliwakuta wafungwa wenzake kadhaa waliokuwa wanasubiri utekelezaji wa hukumu zao za vifo.
Kitu ambacho kilimpa moyo ni kuwa aliwakuta wenzake hao wakiwa wachangamfu kama vile walikuwa na matumaini kuwa wataachiwa.
Wakwetu alikutana na wafungwa wenye uzoefu wa kisheria. Wafungwa hao walimuuliza Wakwetu alihukumiwa kunyongwa kwa kosa gani.
Wakwetu aliwaeleza tukio lililotokea ambalo lilisababisha akamatwe, ashitakiwe na hatimaye ahukumiwe kunyongwa.
Hapo ndipo aliposhauriwa kukata rufani.
“Ukikata rufani utatoka!” mfungwa mmoja alimwambia na kuongeza, “Sisi tutakufundisha jinsi ya kukata rufani. Kuna mambo kumi ya kisheria ambayo hayakuzingatiwa na jaji aliyekuhukumu.”
Kutokana na msaada wa wafungwa wenzake Wakwetu alifanikiwa kukata rufani akiwa mfungwa anayesubiri hukumu ya kunyongwa.
Rufani yake ilichukua miezi mitatu kusikilizwa. Jaji wa mahakama ya rufani ambaye alikuwa Mzungu aligundua kuwa jaji aliyemhukumu Wakwetu alitumia ushahidi usiokubalika kisheria kumtia Wakwetu katika hatia. Aliikubali rufani ya Wakwetu, akaibatilisha hukumu ya kunyongwa na kumuachia huru.
Wakwetu alipotoka mahakamani alilakiwa kwa furaha na marafiki zake wa Kitanzania. Siku chache baadaye alianza tena kuhangaika kutafuta kazi. Baada ya miezi miwili alifanikiwa kupata kibarua cha msaidizi wa fundi umeme katika Bandari ya Cape Town. Aliajiriwa kama msaidizi wa fundi umeme kwa vile alikuwa amesomea ufundi umeme alipokuwa Tanzania.
Akiwa fundi umeme msaidizi, Wakwetu alikuwa akilipwa vizuri na kuna siku ambazo alichukuliwa kwenye meli kurekebisha hitilafu za umeme.
Siku chache tu baada ya kuajiriwa aliitwa katika meli moja ya Kigiriki ambayo ilikuwa na tatizo la umeme.
Wakwetu akagundua kuwa kulikuwa na hitilafu katika mfumo wa kusambaza umeme ndani ya meli. Baada ya kulishughulikia tatizo hilo, kapteni wa meli hiyo alimshauri Wakwetu waimuajiri kazi ndani ya meli hiyo ili ashughulikie matatizo ya umeme yanapotokea.
Wakwetu akakubali. Huo ukawa mwanzo wa Wakwetu kufanya kazi ndani ya meli. Alizunguka na meli dunia nzima: Ulaya, Asia, Marekani na Afrika. Hakuwa na mawasiliano tena na mke wake wala ndugu zake yeyote.
Wakwetu alifanya kazi ndani ya meli kwa miaka kadhaa. Alikuwa akibadili meli huko huko Ulaya. Alipoondoka Afrika alikuwa na umri wa miaka ishirini na minane. Alipoamua kuacha kazi kwenye meli alikuwa na miaka hamsini.
Aliporudi Tanzania alikuwa mtu mzima. Mvi zilikuwa zimeshaanza kupamba kichwani mwake.
Alipotua Dar es Salaam alikwenda kwao. Alikuta wazazi wake wote wawili wameshakufa. Ndugu yake wa kike alikuwa ameshaolewa huko Mwanza, naye alikuwa mtu mzima.
Wakwetu alirudi tena Tanga na kuanza kumtafuta aliyekuwa mke wake. Alilikuta eneo la Magomeni alilokuwa akiishi likiwa limebadilika. Lilikuwa na nyumba nyingi za kisasa zilizobadili mandhari ya eneo hilo.
Mahali alipokuwa anaishi palikuwa na nyumba nyingine ya ghorofa. Hakupata hata mtu wa kumuuliza chochote. Akaenda katika mtaa aliokuwa akiishi bibi yake Zainab, yaani bibi wa aliyekuwa mke wake. Zainab alikuwa yatima aliyelelewa na bibi yake.
Bibi yake Zainab ambaye pia alikuwa akiitwa Zainab alikuwa akiishi katika banda la uani. Wakwetu alilikuta banda hilo likiwa limebomoka na kiwanja kilikuwa kimeota vichaka.
Katika nyumba ya jirani na kiwanja hicho Wakwetu alimkuta mzee aliyekuwa ameketi barazani kwenye kiti cha uvivu. Akaenda kumsalimia.
“Shikamoo mzee.”
“Marahaba. Hujambo?”
“Sijambo. Unajisikiaje hali yako mzee wangu?”
“Hali yangu ni nzuri. Karibu.”
“Asante. Mzee wangu naomba kukuuliza.”
“Uliza.”
“Kulikuwa na bibi mmoja aliyekuwa na kiwanja hiki kilichoko jirani yako. Sijui kama unamfahamu?”
“Nani? Bibi Zainab?”
“Ndiye yeye hasa!”
“Yule bibi alishakufa miaka mingi sana.”
“Alikuwa na mjukuu wake msichana mmoja aliyekuwa akiitwa jina hilo hilo. Sijui kama naye unamfahamu?”
“Yule aliwahi kuolewa na kijana mmoja akamkimbia akaenda Afrika Kusini. Hakurudi tena. Alimuacha mwenzake na ujauzito…”