Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu Mkononi - 28

Muktasari:

  • Baada ya kuolewa na Sele saa tano usiku nilihesabu ndoa ya tatu. Nikajiambia nisingeweza kuishi na waume watatu kwa muda mrefu. Kitu cha msingi ni kutafuta sababu ili niachwe na waume wengine. Licha ya ujinga huo nilioufanya, sikuwa na wasiwasi hata kidogo.

SELE akasita kujibu.

“Mchumba wangu mbona umenyamaza?” Nikamuuliza.

“Naona unaniuliza maswali mengi, ninashindwa kukujibu.”

“Haya nimekubali. Sasa umenichagulia jina gani?”

“Nitakuoa kwa jina la Saumu.” Sele akanijibu haraka.

“Ndilo ulilolipenda au ndilo ulilochaguliwa na mganga?”

“Ah Mishi! Hilo ni jina linaloafikiana na wewe kinyota. Kama nitakuoa kwa jina hilo tutakaa sawa.”

“Kwa hiyo mimi nyota yangu ndio ilikuwa upepo, yako wewe ni vumbi. Uliona nitakupeperusha?”

Sele akacheka.

“Hayo ni mambo ya nyota tu, hakuna tatizo.”

“Binaadamu ninyi!”

“Tuna nini?”

“Mna makubwa!”

“Hilo jina nitalitumia wakati wa kukuoa tu. Lakini jina lako litabaki hilo hilo la Mishi.”

“Sawa. Unavyopenda wewe mume wangu mtarajiwa.”

“Usijali.”

Sele akakata simu.

Baada ya kuzungumza na Sele nikamwambia mtumishi wangu kuwa ninakwenda sokoni kununua vitu vidogo vidogo. Nikajitayarisha kisha nikatoka.

Sikwenda sokoni. Nilikwenda nyumbani kwangu Kimara kwa Musa. Nilikuwa nimemuachia nyumba mtumishi wetu Mage. Nilikuta nyumba ikiwa safi. Nilipofika Mage mwenyewe alikuwa akifua nguo zake.

“Shikamoo dada,” akaniamkia japokuwa umri wetu haukuwa umepishana sana.

“Marahaba. Habari za hapa?”

“Nzuri, unamuonaje shangazi?”

Nilipoondoka hapo nyumbani nilimwambia kuwa ninakwenda kwa shangazi yangu ni mgonjwa.

“Bado anaumwa,” nikamwambia.

Mage akaguna.

“Hana nafuu hata kidogo?’ Aliniuliza.

Nikajidai natikisa kichwa.

“Hana, ndio maana tangu juzi niko huko. Na hivi nimekuja mara moja tu kukujulia hali. Nitarudi huko huko.”

“Mie nipo. Sina tatizo.”

“Ukipata tatizo nipigie simu kunijulisha, nitakuja mara moja.”

“Sawa dada.”

“Na pia mume wangu akitokea unipigie simu uniambie.”

“Sawa.’

Nikatia mkono kwenye mkoba wangu na kutoa notI za shilingi elfu ishirini nikampa.

“Za nini?” Akaniuliza.

“Tumia,” nikamwambia.

“Asante dada.”

“Haya, mimi naondoka.”

“Utarudi lini tena?”

“Kesho kutwa,” nilijisemea tu.

Nikaondoka na kwenda sokoni. Nilinunua vitu nilivyohitaji na nisivyohitaji, ilimradi nikifika nyumbani kwa Mustafa nionekane nilikwenda sokoni.

Baada ya kujaza kapu nikaenda zangu Mbezi. Mustafa alikuwa hajarudi, nikashukuru.

Niliahirisha kuoana na Sele mara mbili kwa kisingizio cha shangazi anaumwa sana. Kumbe nilikuwa nikimsubiri Mustafa apate safari ya kwenda nje.

Musa naye alikuwa hajarudi kutoka Zambia. Sikujua alikuwa amepatwa na nini. Na mimi sikutaka kuuliza kwa sababu sikuwa na shida. Kama yeye hayupo, waume zangu wengine wapo.

Siku ile ambayo Mustafa aliniaga kuwa anakwenda India, nikatoka kwenda kwa Sele. Ilikuwa ni siku ya Jumatatu na Sele alikuwa amepanga tuoane usiku wa siku ya Ijumaa.

Muda aliokuwa amepanga tufunge ndoa ni saa tano usiku. Ilikuwa ndoa ya ajabu lakini nilihisi aliyempangia siku na saa ya kuoana kwetu ni mganga wake. Nilikuwa nimeshagundua kuwa Sele alikuwa mshirikina sana. Yeye kila kitu alikuwa akitegemea waganga.

Mimi nikakubali kila alivyoniambia lakini niliahirisha kuoana kwetu kwa vile sikuwa na nafasi.

Sasa baada ya Mustafa kuondoka ndipo nilimfuata Sele nyumbani kwake.

“Jiandae tufunge ndoa Ijumaa hii,” nikamwambia.

“Kwani shangazi hajambo kidogo?” Akaniuliza.

“Hana hujambo yoyote lakini nimeona tuoane tu kwa sababu siku zinakwenda. Nitamsubiri shangazi hadi lini?”

“Tunaweza kuoana halafu pia unaweza kwenda kumuuguza shangazi yako ukiwa mke wangu.”

“Na itakuwa hivyo.”

“Sasa wewe umeshajiandaa?”

“Mimi nipo tayari hata kama ungetaka kunioa sasa hivi.”

Baada ya kupanga mipango ya ndoa yetu, Sele alizitumia zile siku chache zilizobaki kabla ya ijumaa kwa maandalizi. Nilihamia nyumbani kwake asubuhi ya siku ya alhamisi.

Asubuhi ya siku ya Ijumaa nikapelekwa saluni kupambwa kwa ajili ya ndoa yetu ya saa tano usiku.

Ule muda ulinikera sana na ulikuwa umekera watu wengi walioalikwa. Kila mtu aligundua kuwa muda huo ulipangwa na watu wa falaki (waganga). Mimi niliona lilikuwa jambo la kipumbavu sana kuamini kila anachosema mganga ambaye ni binaadamu kama binaadamu wengine, si Mungu wala si malaika.

Nilikuwa najiuliza kama mganga anakudanganya ili uone amekufanyia kazi umpe pesa, utajuaje? Na mimi niliamini bila shaka yoyote kwamba mganga wa Sele alikuwa muongo mkubwa na ule muda aliutoa tu kwa sababu alipewa pesa. Lakini hata kama tungeoana mchana ingekuwa sawa tu.

Licha ya kukerwa na upuuzi huo, nilijiambia. “Wajinga ndio waliwao.” Mwache aliwe, ni pesa zake mwenyewe.

Baada ya kuolewa na Sele saa tano usiku nilihesabu ndoa ya tatu. Nikajiambia nisingeweza kuishi na waume watatu kwa muda mrefu. Kitu cha msingi ni kutafuta sababu ili niachwe na waume wengine.

Licha ya ujinga huo nilioufanya, sikuwa na wasiwasi hata kidogo. Moyo wangu ulikuwa umeshazoea kufanya udanganyifu, hivyo sikuwa na woga.

Nilikuwa nikijiambia hata kama Mustafa na Musa wangegundua kuwa nilifanya udanganyifu wa kuolewa mara tatu, hatua ambayo wangechukua ni kuniacha tu na yule mtoto aliyezaliwa angechukuliwa na baba yake halisi, mambo yakaisha.

Mara tu baada ya kuolewa na Sele nilimuomba afanye vitu viwili, kwanza awekee mlinzi wa ile nyumba na pili anitafutie dada wa kazi. Sele alikubali kufanya yote. Aliajiri mlinzi na kunitafutia dada wa kazi.

Jambo ambalo lilinifurahisha ni kuwa Sele hakutaka dada yake yeyote akae pale nyumbani hata kama atasafiri. Nikawa nipo peke yangu na mtumishi wangu.

Baada ya wiki moja Sele akaenda zake Mirerani. Siku iliyofuata nikaondoka kwenda nyumbani kwangu Kimara. Musa alikuwa hajarudi. Mage alikuwa akiendelea kutunza nyumba. Nilimpa tena shilingi elfu shirini nikamwambia aendelee kubaki hapo nyumbani. Uongo wangu ulikuwa ule ule kuwa namuuguza shangazi.

Nikamsisitizia kuwa Musa akitokea anipigie simu kunifahamisha.

“Sawa dada nitakufahamisha.”

“Halafu sikiliza, usimwambie kuwa nimekwenda kwa shangazi siku zote hizi. Yule ana tabu kidogo. Mwambie nimekwenda sokoni mara moja kisha unipigie simu. Umenielewa?”

“Nimekuelewa dada.”

Baada ya kuzungumza na Mage nikamuaga na kuondoka. Nikaenda Mbezi.

Mwanangu alikuwa ametoka kwenda kununua ice-cream, tukakutana kwenye geti.

“Shikamoo mama,” akaniamkia.

“Marahaba mwanangu, hujambo?” Nikamuuliza tukiwa tumesimama kando ya geti.

“Sijambo, unatoka wapi?”

“Natoka safari mwanangu, unaishi vizuri na dada?”

“Dada ananipenda, kila siku ananipa hela ninunue ice-cream.”

“Usipende sana kula vitu vya baridi mwanangu.”

“Nala leo tu, kesho sili tena.”

“Haya twende ndani.”

Tukaingia ndani.

Mtumishi wangu aliponiona akanifuata kunipokea mkoba wangu.

“Shikamoo dada,” akaniamkia. Nilikuwa sipendi aniamkie. Si ajabu yeye alikuwa amenizidi umri. Alikuwa akiniamkia tu kwa heshima.

Hakujua kama ile heshima nilikuwa siitaki.

Sikumuitikia. Nikamuuliza.

“Mambo vipi?”

“Tupo. Shangazi anaendeleaje?”

“Bado anaumwa.”

Nikakaa kwenye baraza ya uani.

“Ngoja nikae hapa kwanza, nimechoka!”

Mtumishi naye akakaa karibu yangu.

“Umetuacha kwa muda mrefu.” Mtumishi akaniambia.

“Kwani kuna tatizo lolote?”

“Hakuna tatizo.”

“Rama hakusumbui?”

“Hanisumbui kabisa. Kila siku ananiuliza mama atakuja lini?”

“Leo nitamchukua mwanangu niende naye.”

Nikanyanyuka na kuingia ndani. Nilikuwa nimechoka kweli lakini nilijikaza.

Niliingia chumbani kwangu nikakagua vitu kisha nikatoka na kwenda kukaa sebuleni.

“Lakini dada safari hii umetakata! Unatumia losheni gani?” Mtumishi akaniuliza.

“Nimetakata, nimekuwaje?”

“Umependeza.”

“Mbona niko kawaida tu.”

“Umesema utamchukua Rama?” Mtumishi akabadili mada.

“Nitamchukua nikakae naye huko aondoe hamu yake. Mwenyewe ana hamu na mama yake.”

“Utanichukua mama eh?” Rama akaniuliza.

“Nitakuchukua mwanangu twende kwa bibi yako,” nikamwambia.

“Bibi yangu yuko wapi?”

“Yuko Ilala.”

Hapo hapo simu yangu ikaita, nikaichukua na kutazama namba iliyokuwa inapiga. Ilikuwa namba ya Amina.

Nikaipokea.

“Hello…Amina za kunisusa?”

“Sijakususa shoga mwenzako niko Arusha. Nilipoteza simu yangu nikawa sina namba yako. Nilikuwa najaribu tu namba.”

“Umekwenda lini Arusha?”

“Mbona niko muda mrefu.”

“Sasa uko na nani?”

“Si niko na Shabir.”

“Mmeshaoana?”

“Ndio tuko kwenye mipango.”

“Kwani Shabir hana mke?”

“Anae, yuko Dar.”

“Kwa hiyo utakuwa mke mwenza?”

“Nimekubali niwe mke mwenza kwa vile Shabir mwenyewe nimeshamchota. Mapenzi yote yako kwangu.”

Inaendelea...