Hadithi
HADITHI: Kwa Mtutu wa Bunduki - 5

Muktasari:
- Alipoingia katikati ya kundi hilo akaliona gari la Idara ya upelelezi alilokuwa akiendesha Temba, tairi zake za mbele zimeingia katika mfereji. Msembeko alichungulia ndani ya gari hilo na alimuona Inspekta Temba amelalia sukani ya gari.
“UNA maana kwamba huyo mfungwa mko naye hadi sasa?”
“Tuko naye.”
“Kuna watu wameitambua picha yake wakidai kuwa amehusika katika tukio moja la uhalifu lililotokea hapa Dar.”
“Temba alinieleza lakini nilimthibitishia kwamba huyo mfungwa tuko naye na tulimuita ili amuone mwenyewe.”
“Hiyo ina maana kwamba huyo mfungwa siye aliyehusika.”
“Ndiyo maana yake.”
“Sasa tatizo jingine lililotokea ni kwamba Inspekta hajaleta taarifa ofisini na akipigiwa simu, simu inaita tu.”
“Aliniambia anakwenda Sinza.”
“Nitamfuatilia huko huko.”
Alipotoka Segerea Msembeko alikwenda Sinza lakini alipofika hatua chache kabla ya kuifikia klabu ya Tamasha aliona watu wengi wamekusanyika kando ya mfereji uliokuwa kando ya barabara.
Msembeko alisimamisha gari upande wa pili wa barabara na kushuka akaenda kutazama nini kimetokea.
Alipoingia katikati ya kundi hilo akaliona gari la Idara ya upelelezi alilokuwa akiendesha Temba, tairi zake za mbele zimeingia katika mfereji.
Msembeko alichungulia ndani ya gari hilo na alimuona Inspekta Temba amelalia sukani ya gari.
“Inspekta!” Msembeko alimuita.
Temba alikuwa kimya. Msembeko akawageukia watu. Waliokuwa hapo.
“Jamani nini kimetokea?” Akawauliza.
“Hili gari liliingia katika mfereji wakati linapitwa na gari jingine lililotokea kwa nyuma.” Msamaria mwema mmoja alimwambia Msembeko.
“Hebu nieleze vizuri. Hili gari lipitwe na gari jingine halafu liingie kwenye mfereji?”
“Hivyo ndivyo ilivyotokea.”
“Wewe uliona hilo tukio?”
“Ndiyo, nililiona.”
“Hilo gari lilikuwa la aina gani?”
“Ilikuwa ni Toyota Land Cruiser.”
“Ya rangi gani?”
“Nyeupe.”
“Baada ya hili gari kuingia kwenye mfereji, hilo gari lilisimama?”
“Hapana, halikusimama.”
Gari la polisi wa usalama barabarani likafika. Polisi wanne walishuka na kuelekea mahali lilipotokea tukio. Walisalimiana na Msembeko kisha wakauliza watu jinsi ajali ilivyotokea.
“Mmechelewa kiasi cha kutosha. Kwanza mngemtoa mtu aliyemo ndani ya gari.” Msembeko aliwaambia.
Likaanza zoezi hilo. Temba alipotolewa kwenye gari na gari hilo kusukumwa na kutolewa kwenye mfereji, Temba alionekana kama amezirai.
Baada ya Msembeko kumchunguza aligundua alikuwa akitokwa na damu juu ya sikio lake la mkono wa kushoto. Baada ya kumchunguza zaidi aligundua alikuwa na tundu juu ya sikio hilo iliyokuwa inavuja damu.
“Hii ni ajali kweli au kulitokea nini?” Polisi mmoja akauliza.
“Maelezo niliyoyapata ni kuwa hili gari lilipitwa na gari jingine kabla ya kuingia kwenye mfereji.” Msembeko alimwaambia.
“Kivipi?”
“Utawauliza mashuhuda.”
“Nani ameona wakati ajali hii inatokea?” Polisi huyo akauliza watu.
Yule mtu aliyetoa maelezo kwa Inspekta Temba akawaeleza polisi hao jinsi gari hilo lilivyoingia kwenye mfereji.
“Hebu kwanza muwahisheni huyu mtu hospitalini halafu mtarudi tena kuhoji watu.” Msembeko aliwaambia polisi hao kabla ya kusogea kando akatoa simu yake na kumpigia simu mkurugenzi wa upelelezi.
“Mkuu kuna tukio limetokea,” alimwambia mkurugenzi huyo baada ya kupokea simu.
“Tukio gani?”
Msembeko akamueleza mkurugenzi huyo kuhusu ajali hiyo iliyomkuta Inspekta Temba.
Dakika chache baadaye eneo hilo likajaa makachero na polisi mbalimbali waliokuja kuchunguza kuhusu tukio hilo.
**********
Msembeko alikaa kwenye benchi nje ya chumba cha upasuaji katika hospitali ya Muhimbili kwa saa nzima kabla ya mmoja wa madaktari kutoka katika chumba hicho na kumwambia Msembeko.
“Hii si ajali ya gari kama mlivyodhani. Majeruhi alishafariki na hakuwa amezirai. Tumechunguza na tumegundua kuwa alipigwa risasi juu ya sikio lake la kushoto na kusababisha kifo chake. Ni risasi ndogo ya bastola na ni hii hapa.” Daktari huyo alimwambia Msembeko na kumuonyesha risasi hiyo aliyokuwa ameishikilia kwenye mkasi.
Msembeko aliitupia macho na kumwambia.
“Kweli ni risasi ya bastola. Nafikiri walimpiga wakati wanampita kwa gari lao.”
“Bila shaka ilikuwa ni hivyo.”
“Sasa imefahamika kwamba Inspekta Temba ameuawa.”
“Kama si hii risasi, ajali ile isingemuua.”
“Bila shaka aliacha njia na kuingia kwenye mfereji baada ya kupigwa risasi.”
“Ndiyo hivyo.”
“Sasa mtatutayarishia ripoti yake kamili.”
“Tutawatayarishia.”
“Sawa.”
Alipotoka hospitali ya Muhimbili, Msembeko alirudi makao ya polisi na kuonana na mkurugenzi wa upelelezi.
“Inspekta Temba ameshazinduka?” Mkurugenzi wa upelelezi akamuuliza Msembeko.
“Si vile tulivyodhani mkuu.”
Mkurugenzi huyo akamkazia macho Msembeko.
“Ni vipi?”
“Temba ameuawa.”
“Eti nini, Temba ameuawa?”
“Alipigwa risasi kabla ya kuingiza gari kwenye mfereji. Madaktari wamegundua risasi juu ya sikio lake la kushoto.”
Mkurugenzi wa upelelezi alitulia kwa sekunde kadhaa akapumua kabla ya kuuliza.
“Madaktari wamegundua risasi ya silaha gani?”
“Risasi ya bastola.”
“Kumbe huo ndio mchezo uliopita. Wakati ule wanalipita gari alilokuwa anaendesha walimpiga risasi vile walivyoona anafuatilia habari ya kutekwa kwa yule msichana?”
“Natumaini mkuu umelielewa suala zima.”
“Sasa ninabaini kuwa kikundi kilichomteka huyu msichana ni cha hatari na kimejipanga kukabiliana na lolote.”
“Ni katika dakika za mapema tu mpelelezi anauawa.”
“Sasa utakwenda wewe Sinza kumuona yule msichana aliyeelezwa kuwa alizaa na Simon Kumbo. Akueleze mahali aliko mzazi mwenzake. Lazima atakuwa anajua yuko wapi.”
“Na yeye anastahili kukamatwa?”
“Wewe ni kachero, huna haja ya kufundishwa kila kitu.”
Wakati Msembeko anainuka kwenye kiti, mkurugenzi wa upelelezi alimwambia.
“Unapokwenda Sinza kuwa kamili kamili. Chukua bastola yako uijaze risasi. Kuwa macho na kila mtu ukijua kuwa na wewe unafuatiliwa.”
“Sawa mkuu.”
**********
Kifo cha Temba kilikuwa kimempa fundisho Msembeko. Akichanganya na onyo alilopewa na mkurugenzi wa upelelezi, Msembeko alikuwa amepata somo muhimu la kuzingatia katika upelelezi wake.
Wakati anaendesha kwenda Sinza, maneno ya mkurugenzi wa upelelezi yalikuwa yakipita kwa kujirudia katika akili ya Msembeko: “Unapokwenda Sinza kuwa kamili kamili. Chukua bastola yako uijaze risasi. Kuwa macho na kila mtu ukijua unafuatiliwa.”
Tangu alipoondoka makao ya polisi mara kwa mara aliigusa bastola yake aliyoitia ndani ya koti kuhakikisha kwamba ilikuwapo. Macho yake wakati wote yalikuwa kwenye kioo cha kutazamia nyuma kuangalia kama kulikuwa na gari au bodaboda iliyokuwa inamfuata.
Alijiambia huenda ilikuwa kasoro ndogo tu iliyosababisha Temba auawe. Huenda hakuwa makini wakati akiendesha au alijisahau kiasi cha kusababisha mtu aliye kwenye gari jingine ampige risasi.
Alipofika klabu ya Tamasha, Msembeko aliliegesha gari kwenye eneo la maegesho. Watu mmoja mmoja aliowaona wakiingia na kutoka katika lango la klabu hiyo walimpa matumaini kwamba harakati zilikuwa zikiendelea ndani ya klabu mchana huo.
Aliposhuka kwenye gari alitembea kuelekea kwenye lango la klabu hiyo kwa hatua madhubuti huku macho yake maangavu yakimulika kila upande.
Aliingia kwenye lango hilo akaelekea upande wa kulia kulikokuwa na ukumbi wa baa. Aliwakuta watu wachache wakinywa bia. Alikwenda moja kwa moja kaunta akakaa kwenye kigoda na kumwambia mhudumu aliyekuwa nyuma ya kaunta ampe soda ya Coca Cola.
Alipopatiwa soda aliyoagiza alimuuliza mhudumu huyo.
Suzana yuko wapi?”
“Suzana alishaacha kazi.”
Msembeko akagutuka.
“Aliacha lini?”
“Ni muda sasa. Inafika mwaka.”
Msembeko alipiga funda la Coca Cola na kulimeza. Mwili ukamsisimka.
“Yuko wapi hivi sasa?” Alimuuliza mhudumu huyo.
“Nilisikia alipata kazi kwenye Super Market moja Kariakoo.
“Unaifahamu Super Market yenyewe?”
Msichana akatikisa kichwa.
“Siifahamu, sijawahi kufika lakini ni Kariakoo.”
“Kuishi?”
“Nafikiri anaishi kule kule.”
“Wapi?”
“Bunju.”
“Sijawahi kufika nyumbani kwake na sidhani kama ninaweza kupafahamu.”
“Kwani mna uhusiano?”
“Zamani.”
“Sasa unataka kupasha kiporo?”
“Ikiwezekana.”
“Utaweza kumpiku Simon?”
“Yuko na Simon hadi sasa?”
Inaendelea...